Kitaifa
Ni lala salama ya kulia au kucheka
Dodoma. Wakati mjadala wa bajeti kuu ya Serikali ukielekea ukingoni, wabunge wameitwisha mzigo Serikali wa kufanya marekebisho ya maeneo mbalimbali ambayo yameonekana kero kwa Watanzania katika bajeti ya mwaka 2023/24.
Maeneo matano hata hivyo, ndiyo ambayo wabunge waliyashupalia kwa kutoa hoja, likiwamo suala tete la uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam.
Maeneo mengine yaliyovutia mjadala kwa wabunge ni kuporomoka kwa bei ya alizeti, bei ya mahindi, kuongezwa kwa Sh100 kwenye mafuta ya petroli na dizeli na ongezeko la Sh1,000 kwenye saruji.
Mjadala wa bajeti hiyo ulioanza Juni 19 baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kusoma bajeti akiliomba Bunge kuiidhinishia Sh44.39 trilioni, sasa upo katika hatua za lala salama, kwa kuwa unatarajiwa kuhitimishwa Jumatatu Juni 26, 2023 kwa wabunge kuipigia kura.
Saruji, petroli kuongezwa Sh1,000 na 100
Wakichangia mijadala kwa nyakati tofauti, baadhi ya wabunge walihoji kuongezwa kwa Sh1,000 kwenye saruji, wakiitaka Serikali kufikiria upya kwa sababu litawafanya watu wa chini kushindwa kumudu ujenzi wa nyumba bora.
Pia wabunge walisema kuongeza Sh100 katika mafuta ya petroli na dizeli kutasababisha ugumu wa maisha kwa Watanzania.
Suala hilo lilizungumziwa na wabunge kama Kunti Majala na Salome Makamba (Viti Maalumu) na Mrisho Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini.
“Mmeongeza Sh1,000 katika saruji, hivi mnataka tukakae katika nyumba za udongo? Ninafahamu kuwa sekta ya nondo, saruji ni biashara kubwa, lakini tusiwasahau Watanzania wa kawaida wanaotumia rasilimali hizi kujiboreshea mazingira yao ya kawaida,” alisema Makamba.
Mafuta ya kupikia
Kuporomoka kwa bei ya alizeti kuliwaibua wabunge wengi kwenye mjadala huo, wakitaka Serikali kutoshusha ushuru kwa mafuta ya alizeti yanayotoka nje ya nchi.
Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima, alisema wananchi walihamasishwa kulima alizeti, lakini bahati mbaya sana bei imeshuka ambapo kilo moja inauzwa kwa Sh500.
“Uandaaji tu wa kilimo unazidi hiyo fedha. Kabla ya Uviko- 19 kodi ya mafuta kutoka nje ya nchi ilikuwa ni asilimia 35, sasa ni asilimia 25 bado ni changamoto, turudi kwenye asilimia 35,” alisema.
Alishauri pia kuwepo kwa vibali vya uagizaji wa mafuta kama ilivyo katika sukari ili kusaidia kutoporomoka kwa bei ya zao hilo.
Hata hivyo, katikati ya mjadala huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alijibu hoja hiyo na kusema hawajapandisha wala kushusha kodi ya mafuta yanayoingizwa kutoka nje.
“Nataka nitoe taarifa kwamba sio kwamba tumeshusha, tumebakiza ya mwaka jana (2022/23) kwa ajili ya kukabiliana na gharama za maisha, kwa maana hiyo wabunge wamesema hapa tupandishe sisi tumechukua hilo,” alisema Dk Mwigulu.
Hoja ya kuporomoka kwa bei ya alizeti iliungwa mkono na baadhi wabunge, wakiwamo Boniventura Kiswaga (Magu), Miraji Mtaturu (Singida Mashariki), Cosato Chumi (Mafinga), Kunti Majala (Viti Maalumu), Stanlaus Nyongo (Maswa Mashariki) na Ramadhan Ighondo (Singida Kaskazini).
Uwekezaji wa bandari
Juni 10, Bunge liliridhia azimio la makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji wa bandari nchini.
Hata baada ya kuridhiwa kwa mkataba huo, kumekuwa na mjadala mkubwa kutoka ndani na nje ya Bunge kuhusiana suala hilo.
Wakichangia bajeti hiyo, wabunge walikuwa na maoni tofauti, ikiwa ni pamoja na kupongeza Serikali, huku wakiitaka kutafakari yale ambayo yamekuwa yakisemwa na wadau.
Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Mayenga alisema imani yake na imani ya wengine, kuwa kwenye suala hilo kuna makosa yalitokea mahali.
“Mimi nasema nyakati kama hizi ambazo kila mtu anakuwa na ya kwake ya kusema, hatuna budi sisi kama wabunge kukaa chini na kutafakari yale ambayo yanasemwa na kuangalia ni kitu gani tunaweza kukisukuma ili Serikali iweze kufanya kazi,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby aliwataka Watanzania wasiogope wawekezaji, kwani kuja kwao kunawezesha kukua kwa uchumi wa Taifa, huku akisema mapato yanayopatikana hivi sasa ni madogo sana.
“Mwaka wa fedha 2021/22 bandari ilikusanya mapato Sh1.14 tilioni ambapo matumizi yalikuwa Sh805 bilioni, faida iliyopatikana ilikuwa Sh339 bilioni. Kwa hiyo ukiangalia yaani matumizi ni asilimia 73 faida ni asilimia 27, hilo ni tatizo,” alisema.
Wabunge wengine waliochangia katika eneo hilo ni pamoja na Subira Mgalu (Viti Maalumu), Hamis Tabasamu (Sengerema), Jerry Silaa (Ukonga) na Vedasto Manyinyi.
Sakata la mahindi
Wakichangia kuhusu kuporomoka kwa bei ya mahindi, wabunge walisema bei ya mahindi imeporomoka ambapo debe moja lililokuwa likiuzwa kwa bei ya Sh15,000, sasa linauzwa kwa Sh5,000, jambo linalowakatisha tamaa wakulima wa zao hilo nchini.
Wabunge hao walisema kuporomoka kwa bei ya mahindi kunatokana na Serikali kuzuia biashara ya usafirishaji wa mazao nje ya nchi.
Suala hilo lilijitokeza nyakati tofauti bungeni, wakati wabunge wakichangia na kuomba mwongozo ili shughuli ya mjadala ya bajeti hiyo iahirishwe ili waweze kujadili hoja hiyo.
Kutokana na hoja hiyo, Serikali kupitia Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe na Naibu wake, Antony Mavunde walilazimika kuomba taarifa ili kutoa ufafanuzi kuwa hakuna biashara ya mazao iliyopigwa marufuku na Serikali ila wafanyabiashara wanatakiwa kufuata utaratibu.
Licha ya ufafanuzi huo, joto la wabunge kuhusu soko la mahindi liliendelea, ambapo jana wawakilishi hao wa wananchi walisimamisha shughuli za Bunge na kuanza kujadili kuhusu usafirishaji nje wa mahindi na bei ya zao hilo kwa wakulima.
Mjadala huo uliibuliwa jana na Mbunge wa Momba (CCM), Condester Sichwale ikiwa ni siku moja tangu Mbunge wa Mbozi (CCM), George Mwenesongole aliposimamisha Bunge akitaka lijadili hasara wanayopata wakulima.
Mbali na Sichwale, wabunge wanane na mawaziri watatu walizungumzia sakata hilo kwa undani ambapo kila upande ulieleza faida na hasara ya kusimamishwa kwa wanunuzi walioitwa ni holela.
Hata hivyo, wabunge walipinga zuio la Waziri Bashe kuwa lilikuja katika kipindi cha haraka sana, wakamtaka afikiri upya ili ikiwezekana zuio hilo lianze mwakani.
Katika hoja yake, Sichwale alisema zuio la wafanyabiashara kutonunua mahindi limepeleka umasikini mkubwa kwa wakulima na kuwapotezea malengo yao, lakini kwa wanunuzi wameumizwa kwani limekuwa la ghafla.
“Mheshimiwa Spika, bei za mahindi huko kwa wakulima zilishapanda, lakini kutokana na katazo hili zimeporomoka kwa kiasi kikubwa. Waziri anasema maombi ya wanaotaka kununua na kuuza mahindi nje yanapatikana kwenye mtandao, jambo ambalo lina utata,” alisema Sichwale.
Mbunge huyo ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Tehama alisema kuwa, ndani ya mfumo wa maombi kuna changamoto kubwa kwa mtandao kutofanya kazi kama inavyotakiwa na akamuomba Bashe asitishe mpango huo hadi mwakani.
Mbunge wa Kiteto, Edward Ole Lekaita alisema tamko la Waziri Bashe limesababisha kushuka kwa bei ya mahindi.
Alisema wakulima walishafikia kuuza Sh90,000 kwa gunia moja, lakini sasa wanauza Sh55,000, jambo linalowanyonya wakulima.
Lekaita alimuomba Waziri kutumia nafasi hiyo kutangaza bei elekezi ambayo itakuwa ni ya juu kwa manufaa ya wakulima ili waweze kuondokana na unyonyaji.
Wabunge wengine waliochangia katika mjadala huo na kupinga kauli ya Waziri Bashe ni Sophia Mwakagenda, Yahaya Masale, Seleman Kakoso, Josephina Genzabuke, Deo Sangu na Aeshi Hilaly.
Hata hivyo, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma aliungana na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe na Dk Mwigulu (Fedha) waliokuwa waliunga mkono kauli ya Waziri Bashe, wakisema lazima utaratibu ufuatwe.
Akihitimisha hoja hiyo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson aliitaka Serikali kutambua kiasi gani cha mahindi kilichozalishwa Tanzania na kujipanga kununua mahindi, ambayo Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) una uwezo nayo ili yatakayobaki wakulima waachiwe wauze katika soko la ushindani.
Aliunga mkono hoja ya kufuata utaratibu kwa madai kuwa, lazima Serikali ikusanye michango na tozo, kwani ilitumia gharama kubwa kutoa mbolea ya ruzuku mwaka jana, hivyo lazima itengeneze mazingira ya kuendelea kutoa ruzuku.
Katika majibu yake kwa wabunge, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliendelea na msimamo wake kuwa, Serikali haijazuia mahindi kusafirishwa nje, lakini msimamo utabaki vilevile kuwa, lazima wafuate sheria na walipe kodi halali.
Alisema Serikali imeshatoa Sh320 bilioni kuipa NFRA, kwa ajili ya kunua mahindi kwa kilo Sh600 hadi 800.
Waziri alisema wanaosafirisha mahindi kutoka kwa wakulima moja kwa moja siyo Watanzania, huku akieleza hatari iliyopo ya nchi kufungiwa kusafirisha zao hilo nje, baada ya kubainika kuwapo kwa shehena moja iliyopelekwa nchi jirani kuwa na unyevu, jambo linalosababisha mahindi kutokuwa na sifa stahiki.
Maoni ya wadau
Akizungumza na Mwananchi, Mtaalamu wa Uchumi na Mhadhiri wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dk Nasibu Mramba alisema kilio cha kupanda kwa bei za bidhaa, kinasababishwa na nishati na katika kipindi hiki ambacho bei ziko juu, kuongezwa kwa tozo ya Sh100 kwa kila lita ya mafuta ya dizeli na petroli, ni mzigo zaidi.
Alisema wazalishaji wa mafuta walitangaza kupunguza uzalishaji wa mafuta kwa lita milioni moja na kwamba wataendelea kupunguza.
“Kilio cha wananchi cha kupanda kwa bei ya bidhaa hakikupata ufumbuzi, lakini sasa kimechochewa na ongezeko hilo la tozo,” alisema.
Naye mchambuzi wa masuala ya uchumi na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Lutengano Mwinuka, alisema uwepo wa maghala ya kuhifadhia mahindi na alizeti, utakuwa msaada katika kukabiliana na changamoto ya kuporomoka kwa bei.
“Ghala linaongeza uhifadhi na uhifadhi unaongeza thamani ya bidhaa inayohifadhiwa. Kwa sababu wakulima wengi huuza mapema baada ya kuvuna, sasa ni vizuri kuhifadhi na kuuza baada ya muda kidogo,” alisema.
Pia Dk Mwinuka alielezea haja ya kuwa na kilimo chenye tija, kwa kile alichosema kuwa kama mkulima atamwagilia na kutumia mbolea, kuna uwezekano wa kupata mavuno mengi na kwa gharama nafuu, hali ambayo hata soko likiwa chini, bado linaweza kumlipa.