Kitaifa
Vumbi la Kongo, ‘Akayabagu’ zapigwa marufuku
Dar es Salaam. Dawa inayoongeza nguvu za kiume maarufu ‘Akayabagu’ pamoja na vumbi la Kongo zimepigwa marufuku kutumika kwa kile kilichoelezwa kuwa hazijathibitishwa ubora wake.
Hayo yamesemwa jana Ijumaa, Juni 23, 2023 na Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Profesa Hamis Malebo kupitia taarifa kwa umma.
“Baraza limepata taarifa ya uwepo wa dawa asili inayotumika kama kinywaji na jamii kubwa hasa wanaume ijulikanayo kwa jina la Akayabagu, hivyo liliamua kufanya uchunguzi wa uingizwaji, usambazwaji, ubora na usalama wa kinywaji hicho,” amesema.
Amesema kutokana na uchunguzi uliofanywa hivi karibuni, imegundulika kuwa, kinywaji hicho hakijawahi kusajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Profesa Malebo amesema kinywaji hicho ambacho kinadaiwa kuongeza nguvu za kiume, kimechanganywa na dawa ya kisasa aina ya Sildenafil (Viagra majina mengine Erecto ama Vega) jambo ambalo ni kinyume cha Sheria,
Watumiaji wamedanganywa na wahusika wanatia mchanganyiko wenye Sildenafil (Viagra).
Amesema kutokana na hali hiyo, hicho
siyo kinywaji cha tiba asili bali ni kinywaji chenye viagra.
“Kuanzia leo Juni 23, 2023, Baraza linapiga marufuku uingizaji, usambazaji, uuzaji na utumiaji wa kinywaji hiki kote nchini.
“Yeyote atakayekiuka agizo hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na atakayepatikana akiwa na kinywaji cha Akayabagu, atakuwa ametenda kosa na ataweza kushitakiwa kwa mujibu wa Sheria,” amesema Profesa Malebo.
Amesema baraza lina utahadharisha umma kuwa makini na matumizi ya dawa ambazo hazijasajiliwa kama vile vumbi la kongo kwani dawa hizo hazijapimwa ubora na usalama wake na mamlaka zinazotambulika kisheria.
Amesema kuanzia leo baraza pia linapiga marufuku uingizaji,
usambazaji, uuzaji na utumiaji wa vumbi la Kongo kote nchini.
“Yeyote atakayekiuka agizo hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Pia ikumbukwe kuwa, yeyote
atakayepatikana akiwa na vumbi la Kongo atakuwa ametenda kosa na atashitakiwa kwa mujibu wa Sheria.
“Mtumiaji anayo haki ya kuuliza na kufahamishwa taarifa ya dawa anazopewa kutumia na kuomba kuoneshwa cheti cha usajili wa dawa hizo. Baraza linaendelea kuikumbusha jamii kuacha tabia ya kutumia dawa hovyo kwani iwapo dawa sio bora na salama, zinaweza kuleta madhara ya kiafya kwa mtumiaji,” amesema Profesa