Connect with us

Kitaifa

Mkataba bandari waibua vigogo

Dar es Salaam. Wadau mbalimbali wamependekeza uwazi wa kutosha uzingatiwe wakati Serikali ikitaka kuingia kwenye mikataba ya kimataifa na maoni yanayotolewa na wananchi kuhusu mkataba wa uendelezaji na uboreshaji wa bandari baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai yafanyiwe kazi.

Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam jana wakati wa mjadala wa kitaifa ulioandaliwa na Kampuni ya Media Brains kuhusu kulinda na kuendeleza umoja wa kitaifa wakati wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi hapa nchini.

Juni 10, mwaka huu Bunge lilipitisha azimio kuhusu pendekezo la kuridhiwa kwa mkataba huo kwa lengo la kuanzisha ushirikiano katika uendelezaji wa maeneo ya bandari nchini.
Kabla na baada ya mkataba huo kuridhiwa na Bunge, uliibuka mjadala maeneo mbalimbali kwamba kuna vifungu vinaibana Serikali.

Hata hivyo, Serikali mara kadhaa imetoka hadharani kutoa ufafanuzi kuhusu maeneo yanayoonekana kuwa na sintofahamu kupitia makundi mbalimbali.
Jana, mjadala huo uliwakutanisha wafanyabiashara, wanasiasa, wanaharakati na waandishi wa habari kwa lengo la kuangazia masuala tofauti na hoja ya mkataba huo ilichukua nafasi kubwa.

Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz alieleza kusikitishwa kwake na mjadala kuhusu mkataba wa kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai, akisema ni sura ya mjadala ambao umekuwa wa kisiasa badala ya kujadili hoja.

Alisema jambo hilo halina afya kwa Tanzania, badala yake wajadiliane na kukosoana katika misingi ya hoja bila kuleta misuguano kwa misingi ya umoja na uzalendo.
“Sina tatizo na mijadala, sina tatizo na watu kukosoa jambo. Kilichonisikitisha ni sura ya mjadala wenyewe umekuwa na sura ya kisiasa na hata viongozi wenyewe wakahusisha na udini,” alisema Rostam.

Alisema huko nyuma Watanzania walikubaliana kwa Serikali isijitie kufanya biashara na kazi hiyo ifanywe na sekta binafsi na Serikali ibaki kama mdhibiti wa shughuli za biashara nchini.
Rostam alisema Watanzania wanapaswa kuwashukuru waasisi walioweka misingi kwa Watanzania kuishi pamoja kwa umoja, licha ya tofauti zao za kidini, kikabila au kikanda.

“Hapa katikati tulipata msukosuko kidogo, kwa mara ya kwanza watu wakaanza kuulizana unatoka kabila gani. Tumefika huko, sasa tunaishi kwa umoja bila kujali tofauti zetu,” alisema mfanyabiashara huyo.

Alisema mambo hayo hayatokei kwa bahati mbaya, bali ni kwa uongozi thabiti wa Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume. Alisema wao ndiyo walimfanya yeye akiwa na ngozi nyeupe kuonekana kama wananchi wengine huko mkoani Tabora.

Alisisitiza inawezekana ndani ya muda mfupi mambo yakabadilika kukawa na machafuko kama nchi za jirani zinazotuzunguka.

Hata hivyo, Rostam alikubali kwamba uwazi ni jambo muhimu katika suala la mikataba na alishauri kwenye mikataba ijayo jambo hilo lizingatiwe, ili kuondoa hali ya kutoaminiana.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula alisema kwa uzoefu wake wa kutumia bandari ya Dar es Salaam kwa miaka 18, inahitaji maboresho makubwa ili iweze kuhudumia mzigo kuanzia unakotoka hadi kumfikia mwagizaji moja kwa moja na kuongeza ufanisi kwa Taifa.

“Shughuli ya bandari lazima udhibti mnyororo mzima wa biashara, usipofanya hivyo utajikuta nje ya biashara. Unatakiwa kudhibiti mzigo kuanzia unapotoka, ufike hapa nchini na kuhakikisha unamfikia mlengwa,” alisema Ngalula ambaye pia ni mmiliki wa kampuni ya usafirishaji ya Bravo Group.

Alieleza kazi hiyo inahitaji mtu mwenye mtandao mkubwa duniani atakayetafuta mizigo huko na kuileta nchini, kisha kuifikisha kwa waagizaji moja kwa moja. Alisema mizigo ikiwa mingi, Serikali nayo itaongeza mapato yake ya kodi.

Akizungumzia umuhimu wa sekta binafsi, Ngalula alieleza ndiyo injini ya uchumi kwa sababu kupitia shughuli inazofanya, inatengeneza ajira nyingi.
“Hili la Bandari ya Dar es Salaam tuna nchi nane tunazopakana nazo, hiyo ni fursa kubwa, lakini tunapata nini katika hiyo fursa?” alihoji.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima alisema ni muhimu kukaribisha wawekezaji, huku Watanzania wakijengewa uwezo wa kuendesha bandari yao wenyewe.

“Watanzania tusijidharau tukadhani mwekezaji kutoka nje ndiyo anafaa. Tukaribishe wawekezaji tukiwa nasi tunajenga uwezo wetu,” alisema.
Alisema Watanzania wanapenda kwenda pamoja na hiyo ndiyo imekuwa nguvu yao kwa muda mrefu, hivyo hata katika sakata la bandari wanatakiwa kuelimishwa ili wote wawe pamoja katika uwekezaji wa rasilimali zao.

Alichokisema Ulimwengu

Mwanahabari mkongwe, Jenerali Ulimwengu alisisitiza juu ya sekta binafsi ya ndani kupewa kipaumbele katika miradi mikubwa huku akitaka wananchi kushirikishwa kuanzia hatua ya awali.

“Tumekuwa na michakato ya ubinafsishaji na uwekezaji wa mitaji mikubwa bila kuwa na uwazi. Mijadala unapojadiliwa na kikundi kidogo cha watu, wananchi wanakuwa na haki ya kuuliza nini kilifanyika.

“Ni muhimu kuwa na uwazi kwa kiwango kinachowezekana, ili kuondoa dhana kwamba kuna rushwa. Hakuna mahali penye rushwa kama serikalini kwa sababu ndiyo chombo chenye fedha nyingi, ndiyo inafanya uamuzi na ndiyo inaweza kutumia mabavu,” alieleza Ulimwengu.

…uwazi, ushirikishwaji
Akichangia mjadala huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Stephen Wasira alisisitiza umuhimu wa uwazi na ushirikishwaji wa wananchi huku akihoji mchakato wa kukusanya maoni kuwa wa muda mfupi na kwa watu wachache.
“Kuhusu mageuzi ya kiuchumi, mageuzi si sheria tu, bali ni fikra za watu, lazima washirikishwe na watoe maoni yao.

“Nilialikwa kwenda kutoa maoni, maoni ni kesho, taarifa napewa leo. Nikasema nipande ndege kesho ili niende Dodoma, huo muda wa kutoa maoni si utakuwa umekwisha?” alihoji Wasira.

Naye, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alishauri kuundwa kwa kampuni maalumu ya Watanzania itakayoingia ubia na kampuni ya DP World katika uendeshaji wa bandari hapa nchini na faida ziwe asilimia 50 kwa 50.

“Tumeambiwa hao DP World watatakiwa kusajiliwa Tanzania ili wasimamiwe kwa sheria za Tanzania, kwa mujibu wa sheria ili waweze kufanya kazi lazima kuwe na ushiriki wa wazawa kwa asilimia 35. Kwa hiyo nadhani tukifanya hivyo itamaliza hizi kelele,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa Shura ya Maimamu, Sheikh Ponda Issa Ponda alisema anakubaliana na hoja ya kuuboresha mkataba huo kwa kusikiliza maoni ya wananchi.
“Nakubali hoja ya kupitia na kuboresha mkataba huo kwa kusikiliza maoni ya wananchi. Ni kweli sisi wenyewe hatuwezi kuendesha bandari, tunahitaji kushirikiana na wenzetu, lakini lazima tukubaliane wote,” alisema Sheikh Ponda.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema alisema, chama hicho hakipingi uwekezaji huo wa bandari, lakini kinachohitajika ni uwazi katika jambo hilo.
Lema, ambaye ni mbunge wa zamani wa Arusha Mjini alisema Tanzania inahitaji wawekezaji wengi zaidi ya bandari na kwamba zinaweza zikaja teknolojia mpya za kusafirisha mizigo na bandari ikaonekana haina maana hivyo, fursa zinapaswa kutumiwa.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi