Kitaifa

Majaliwa: tunapokea maoni, ushauri, hofu uwekezaji bandari

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kupokea maoni, ushauri na hofu zinazotolewa na wananchi kuhusu sakata la uwekezaji bandari huku akisistiza lengo la hatua hiyo ni kuongeza ufanisi wa bandari.

Majaliwa ameyasema hayo jana Jumanne, Juni 20, 2023 katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 40 ya chuo cha International Evangelism Centre kilichopo Sakila jijini Arusha.

“Serikali tunasikia, tunapokea maoni, ushauri na hofu walizonazo Watanzania. Tangu tulipoamua kupeleka azimio la kuanzisha mahusiano katika eneo la uchumi kupitia uwekezaji wa bandari kumekuwa na mjadala, wapo wanaoshauri, wanaobeza na wanaosubiri kuona matokeo,”amesema Majaliwa.

Majaliwa akieleza sababu ya Tanzania kuingia mkataba wa uwekezaji katika bandari na Dubai amesema lengo ni kuboresha tija na ufanisi na Serikali haina malengo ya kuuza bandari.

“Sisi tunapofanya biashara hiyo na watu wanalipa, tumejitahid kutangaza kwa upande wetu na meli zinakuja lakini bado uwezo (ufanisi na tija) ni mdogo na ndio maana foleni ni kubwa bandarini kwetu,”amesema.

Majaliwa ameongeza kuwa pamoja na maboresho yaliyofanyika, hali ya utendaji wa bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa ya kiwango cha chini ikilinganishwa na bandari shindani kikanda.

“Kwa mfano katika bandari yetu ya Dar es Salaam, wastani wa meli kusubiri nangani ni siku tano ikilinganishwa na wastani siku moja na nusu kwa bandari za Mombasa na Durban ambao ndio washindani wetu kibiashara,”amesema.

Hofu kupoteza wateja

Majaliwa amesema udhaifu huo uliopo katika bandari hiyo unasababisha meli kusubiri muda mrefu nangani na hivyo kuongeza  gharama, kwa siku moja ni takriban Dola za Marekani 25,000, sawa na takriban Sh58 milioni kwa siku.

“Kitendo cha meli kutumia muda mrefu kupakia na kupakua shehena gatini kwa wastani wa siku tano ikilinganishwa na siku moja inayokubalika kimataifa kinasababisha meli kubwa kutokuja katika bandari ya Dar es Salaam, hivyo tunaweza kupoteza wateja,”amesema.

DP World ilipatikanaje?

Aidha, Majaliwa alijibu swali linaloulizwa na wengi katika sakata hili la jinsi ilivyopatikana kampuni ya DP World ambayo itafanya uwekezaji katika bandari nchini.

“Mamlaka ya bandari ilipokwenda Dubai kwenye maonyesho ya biashara wakakuta kampuni mbalimbali za kusimamia bandari wakaawaangfalia wote na wakaona DP World anafaa kutokana na kuwa na uzoefu na kuendesha bandari nyingi ikiwemo uingereza,”amesema.

Wachumi wapewa nafasi kutoa ushauri

Majaliwa amesema kilichofanyika sasa hivi katika mkataba ni hatua ya awali kuruhusu utekelezaji na muda utakapofika wataalamu wa uchumi wataishauri Serikali katika mikataba hiyo ya utekelezaji.

“Wakati wa kuingia mikataba utakapofika wataalamu wa uchumi nchini wataishauri Serikali kuhusu muda wa uendeshaji wa uwekezaji huo, kwasasa wananchi tuendelee kuwa na subira,”amesema.

Sakata la uwekezaji bandari nchini lilizidi kupamba moto mara baada ya Bunge Juni 10, 2023 kuupitisha mkataba unaoruhusu makubaliano ya mahusiano baina ya Serikali na Tanzania na Dubai (IGA) ambapo maoni tofauti na kinzani yameibuka katika sehemu mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi