Connect with us

Kitaifa

Matumizi hasi ya Tehama kuzalisha vilaza shuleni, vyuoni

Dar es Salaam. Wakati maendeleo ya teknolojia yakizidi kushika kasi, angalizo limetolewa kwa mifumo ya elimu kuongeza umakini katika kudhibiti ubora kutokana na tishio la matumizi hasi ya teknolojia hizo.

Angalizo hilo limetolewa katika kipindi ambacho Tanzania ipo katika maandalizi ya kuingia kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo msingi wake mkubwa ni teknolojia, ambayo matumizi ya akili bandia (Artificial Intelligence), yanatajwa kuchukua nafasi kubwa.

Hadi sasa tayari kuna programu rununu (apps) kadhaa ambazo zinaelezwa kutumiwa vibaya na wanafunzi kwa kunakili majibu katika kazi za kitaaluma ambazo zinatumika kuwapima viwango vyao vya uelewa.

Mojawapo ya programu ambayo inatajwa kuwa tishio zaidi kwa sasa ni Chat GPT inayoelezwa kuwa kimbilio la wanafunzi kutokana na uwezo mkubwa wa programu hii katika kujibu maswali na kuandika insha.

Siyo maswali pekee, programu hii inaweza kufanya chochote kulingana na maelekezo yako, wapo pia wanaoitumia kuandikiwa barua za maombi ya kazi, andiko la mradi, mawasilisho ya mada na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Athari zake

Akizungumzia hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Dodoma (Udom), Profesa Lughano Kusiluka alisema mapinduzi hayo yamekuja na changamoto ambazo zinaweza kuathiri mifumo mbalimbali, ikiwemo elimu.

Kuhusu programu ya Chat GPT alisema iliundwa kwa lengo zuri la kurahisisha upatikanaji wa taarifa na maarifa, lakini inatumika vibaya na wanafunzi, hivyo ni muhimu walimu kuwa makini kufanya ufuatiliaji.

“Chat GPT ni teknolojia nzuri, lakini matumizi yake yanaweza kuleta shida kwenye elimu yetu, huku vyuoni sasa hivi tuna shida, mwanafunzi anaweza kukuletea tasnifu imeandikwa vizuri na akapata A, ukiifanyia tathmini utagundua wala hakustahili kupata hiyo alama.

“Hii inatufanya vyuo vikuu na sisi tuone haja ya kuwekeza ili kuzibaini tasnifu zinazofanywa kwa njia hii, tuongeze umakini kwenye tathmini. Teknolojia hizi zipo na hatuna namna ya kuzikwepa. lakini tuhakikishe hazitumiki kushusha kiwango cha elimu yetu,” alisema Profesa Kusiluka.

Mkurugenzi mstaafu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Hassan Mshinda alisema teknolojia hiyo ni tatizo kwenye elimu kwa kuwa inawawezesha wanafunzi kufanya udanganyifu.

“Mtu anaweza kuandika tasnifu nzuri kabisa ya kurasa tano ndani ya dakika tano. Hata hivyo hatuwezi kupingana na maendeleo haya, lazima tuendane na kasi hiyo. Changamoto ni kwamba kama tutaenda taratibu kila siku tutakuwa nyuma, lazima kazi kubwa ifanyike kuendana na mabadiliko na maendeleo haya ya teknolojia,” alisema.

Hatari ya matumizi ya programu hizi si tu kwa vyuo vikuu, imebainika kuwa hata wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao wanazifikia simu janja na kompyuta, huzitumia kupata majibu ya maswali wanayopewa na walimu.

Inavyotumika

Siyo Chat GPT pekee, wanafunzi wenyewe walithibitisha kuwa zipo nyingine kadhaa kama Brainy na By Juicy.

“Naifahamu na nimekuwa naitumia, inarahisisha kuandika essay (insha), yaani ukiwa na swali lako unaandika tu kwa haraka inakujibu,” alisema mmoja wa wanafunzi wa sekondari ambaye jina na shule vimehifadhiwa.

Nini kifanyike?

Profesa Kulisuka alisema ili kuepuka athari hasi, ni muhimu kwa wanataaluma kwenda na kasi ya teknolojia hizo ili kubaini udanganyifu unapojitokeza.

“Maendeleo ya teknolojia hayakwepeki, hii itusukume na sisi kuendana na kasi hii kwa kuwekeza kupata teknolojia zinazoweza kubaini hili linapofanyika. Tuongeze umakini kwenye kufanya assessment (tathmini) ya hizi kazi za wanafunzi, ikiwamo tasnifu,” alisema.

Juni 2 mwaka huu, Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda aliwataka wenyeviti wa mabaraza ya vyuo kuhakikisha wanaopata shahada ni wale wanaostahili, lengo likiwa kusimamia ubora wa elimu nchini.

Alielekeza vyuo kutumia mifumo ya Tehama inayowezesha kubaini wanaonakili vitu.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi