Kitaifa
Rais ataja kilichowang’oa vigogo Rita
Dar es Salaam. Ugomvi usiokwisha ulioshusha utendaji kazi katika ofisi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), ndicho chanzo cha Rais Samia Suluhu Hassan kutengua uteuzi wa viongozi wakuu wa taasisi hiyo.
Rais aliweka wazi hayo jana, alipowaapisha kabidhi wasii mkuu mpya na naibu wake katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma. Pia katika hafla hiyo aliwaapisha viongozi wengine aliowateua hivi karibuni.
Mbali na hilo, alisema utendaji mzuri wa aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Rogatus Mativila, ndiyo sababu ya kumpandisha kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tamisemi (Miundombinu).
Siku sita zilizopita Rais alimteua Frank Kanyusi kuwa Kabidhi Wasii Mkuu wa Rita, akichukua nafasi ya Angela Anatory, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa. Pia alimteua Irene Lesulie kuwa Naibu Kabidhi Wasii Mkuu, akichukua nafasi ya Lina Sanga.
“Kabidhi Wasii Mkuu na naibu wako nimewateua baada ya kuwaondoa viongozi wote wawili waliokuwepo pale, nilikuwa nategemea wananchi wapate huduma za kuridhisha ndani ya ile ofisi, lakini kilichokuwa kinatokea ilikuwa ni ugomvi.
“Nikasema labda kwa kuwa wote walikuwa kinamama ndiyo maana kulikuwa na ugomvi mkubwa, lakini ukiangalia kwa ndani kulikuwa na kutokutekelezeka kwa kazi vizuri, mwingine akisema huyu anakasirika, mwingine akirekebisha mwingine anachafua, kwa hiyo nikaamua kuwaondoa wote wawili watapangiwa kazi nyingine, sasa nendeni ninyi,” Rais aliwaagiza wateule wapya.
Aliwataka wakashirikiane kutoa huduma kwa wananchi akisema: “Ile ni ofisi kubwa, wananchi wanaitegemea, badala ya kujenga ugomvi humo ndani, nendeni kashirikianeni, angalieni wapi kumeharibika, wekeni sawa toeni huduma.”
Rais Samia alieleza kuwa kulikuwa na baadhi ya kesi ambazo zilifika ofisini kwake na kila alipojaribu kuwaambia walalamikaji warudi Rita, walikataa wakisema hapaendeki na hawajui kinachoendelea.
“Kama mlivyokula kiapo hapa mkashirikiane, nimewateua kuhakikisha mambo yanakuwa sawa,” alisema.
Kuhusu Mativila
Rais Samia alisema utendaji mzuri wa Mativila ndiyo sababu ya kumpandisha kuwa naibu katibu mkuu.
“Bado tunacheza drafti la kupanga Serikali na ndivyo inatakiwa kwa sababu maendeleo ni ‘adjustment’, ukiona mambo yanakwama hapa una-adjust hapa unakwenda mpaka unapata laini iliyo sawa. Kwa hiyo, bado tutaendelea kufanya hivyo mpaka tupate laini iliyo sawasawa katika kila sekta.
“Nimefanya teuzi hizi ndogo, Tamisemi nimemteua Mativila alifanya kazi nzuri sana akiwa Tanroads nikaona nimpandishe awe Naibu Katibu Mkuu Tamisemi (Miundombinu). Tamisemi ni dude kubwa sana, lakini watu ni wachache. Waziri, naibu waziri, katibu mkuu, manaibu lakini kisekta hawajaenea,” alisema.
Rais alisema: “Mwanzo tulifanya adjustment tukamteua naibu katibu mkuu anayekwenda kushughulikia Tamisemi yenye administration ya wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa wote walikuwapo kule na jinsi kazi inavyofanyika.
“Lakini Tamisemi hii sasa ina Tarura na Tanroads nayo inafanya kazi Tamisemi. Tamisemi hii inajenga na vituo vya afya, lazima tuwe na mtu maalumu atakayesimamia miundombinu. Nikahisi Injinia Mativila atatufaa.”
Alisema Mativila atakwenda kusimamia miundombinu yote itakayojengwa nchini chini ya Tamisemi na kuhakikisha inaendana na fedha inayotolewa. Alisema kiasi kikubwa cha fedha hutolewa, lakini hupotea.
Majukumu ya wateule wake
Katika hatua nyingine, Rais Samia amechambua kazi zitakazofanywa na viongozi aliowateua hivi karibuni, akiainisha majukumu ya kila mmoja.
Hivi karibuni, Rais Samia aliwateua viongozi mbalimbali, wakiwemo mabalozi na washauri wake katika masuala ya siasa.
Katika sekta ya maliasili na utalii alisema amemteua Kamishna wa Polisi, Benedict Wakulyamba kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, ili akashughulikie kero zinazosikika kwenye Jeshi Usu.
“Umekwenda utalii na maliasili sababu ni moja tu, kuna Jeshi Usu na kule tunasikia kesi za Jeshi Usu mara wameuana, mara wameua kuna mambo mengi huko.
“Sasa wewe ni mwanajeshi mwenzao, nenda kasimamie nidhamu ya Jeshi Usu, hiyo ndiyo kazi yako, kusimamia jeshi letu, hiyo ndiyo kazi yako mahsusi na atakayokupangia waziri wako au katibu mkuu wako,” alisema.
Akizungumzia hadhi ya ubalozi aliyopewa Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka alisema ni msaidizi wake wa karibu, hivyo amempa nafasi hiyo ili pale anapozongwa na majukumu ya kazi awe na uwezo wa kuwasikiliza wageni wake.
“Kuna wakati Rais anazongwa na kazi nyingi na kuna wageni wanataka kumuona Rais. Mtu asiye na hadhi ya ubalozi wanakuwa wanyonge kumuona, hivyo tumempa hadhi ya ubalozi Dk Kusiluka apate upeo mpana wa kufanya kazi zake, anipunguzie mzigo,” alisema.
Kuhusu mabalozi wawili aliowateua, akiwemo Dk Salim Othman Hamad, ambaye ni Msaidizi wa Rais – Siasa, amesema walikuwa washauri wa masuala ya siasa, hivyo amewateua ili mikutano inayofanyika kimataifa Tanzania iweze kushiriki haraka na hatua kuchukuliwa.
“Mambo ya siasa hayapo tu kwenye vyama, hata balozi zetu zilizopo hapa kuna mambo yanaitwa political diague ‘mjadala wa kisiasa’ ambayo Mambo ya Nje huwa wanafanya, kwa hiyo tungependa wanapofanya Dk Salim ofisi yangu iwe imeshiriki, tujue wamesema nini na kitu gani tuchukue na hatua za haraka tuchukue.
“Kwa hiyo tumempa ubalozi afanye hayo, lakini na yeye huwezi kujua mbele huko tunaweza kumtafutia kituo akaenda kutusaidia huko,” amesema.
Kwa upande wa Dk Kassim Mohamed Khamis, ambaye alikuwa Msaidizi wa Rais – Hotuba, kupata nafasi ya ubalozi, alisema amefanya kazi muda mrefu Umoja wa Afrika (AU) akiandika majarida na kufanya uchambuzi, hivyo kwa sasa atashughulika na uchambuzi wa mambo mbalimbali Ofisi ya Rais.
Rais Samia pia alitaja majukumu ya washauri wake ambao ni William Lukuvi, ambaye ni Mbunge wa Ismani (CCM); Abdallah Bulembo, mbunge mstaafu; Balozi Rajab Omar Luhwavi, aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji na Haji Omar Kheir, ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Waziri mstaafu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“Siasa tumeiachia chama, lakini kwenye chama kuna nenda rudi vuta, purura nini, lakini kama mnavyojua nimeteua Waziri, Ofisi ya Rais, Kapteni mstaafu George Mkuchika akiwa na kazi maalumu, sasa kazi yao ni kuoanisha siasa na maendeleo.
“Asingeweza kufanya kazi hiyo peke yake, nimewateua wenzake wazame huko chini atuambie siasa zetu zikoje, jamii ikoje na siasa. Watuambie nini kinakosekana na waje na mapendekezo kitu cha kufanya,” alisema Rais Samia.
Alichosema Dk Mpango
Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akizungumza katika hafla ya kuapishwa viongozi hao, amewataka kushirikiana na wakuu wao.
Aliwataka mabalozi kuhakikisha wanaimarisha kazi inayofanywa na Rais Samia ya diplomasia ya uchumi.