Kitaifa

Walimu kufanya mtihani kabla ya ajira

Dar es Salaam. Ule mtazamo kuwa taaluma ya ualimu ni chaguo la mwisho baada ya kukosa fursa nyingine unakaribia ukingoni, baada ya Serikali kutangaza utaratibu mpya katika ajira za taaluma hiyo.

Utaratibu huo, kwa mujibu wa Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda utahusisha, ili uajiriwe kuwa mwalimu utapaswa kufanya mtihani wa kupima uwezo wako.

Kwa sasa, ajira ya ualimu inahusisha kutuma maombi katika tovuti maalum ya maombi ya ajira, kisha anayepata nafasi hufanyiwa usaili kisha kupangiwa eneo la kazi.

Utaratibu mpya wa ajira za ualimu, umetangazwa leo, Juni 16, 2023 na Profesa Mkenda wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa walimu walioshinda shindano la kwanza la stadi za kufundisha kuhesabu na hisabati, lililoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).

Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, utaratibu huo utaanza kufanyika katika ajira mpya za taaluma hiyo.

“Wakati wa kutangaza nafasi mpya za ualimu, wakitaka kupata kazi, watafanya mtihani haijalishi tayari umesoma, kwanza itatuondolea matatizo.

“Kuajiriwa kuwa Mwalimu utafanya mtihani, utaona matokeo, tutaangalia idadi inayohitajika tutachukua waliofaulu tutawaajiri,” ameeleza.

Utaratibu huo, amesema inalenga kurudisha hadhi ya taaluma ya ualimu, isitazamwe kuwa chaguo la mwisho baada ya kukosa nyingine.

Hata hivyo, amesema utaratibu huo hautafuta mchakato wa usaili, akisisitiza utaendelea kama kawaida ili kupata walimu bora.

Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda amebainisha maandalizi ya muongozo wa kuchukua walimu wa kujitolea, huku akidokeza tafakari inafanyika kuona uwezekano wa kuanzisha mafunzo tarajali kwa walimu.

Amegusia baadhi ya masomo yanayotarajiwa kufundishwa kwa mujibu wa rasimu ya sera ya elimu, hayana walimu wa kutosha na aliahidi kulishughulikia hilo haraka.

“Tunahutaji tujaze nafasi hizo, lakini tutakwenda kujaza nafasi hizo,” alisema.

Akizungumzia tuzo hizo, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk Aneth Komba amesema ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa BUST unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).

Shindano hilo, amesema lilianza Aprili mwaka huu na video za walimu kutoka halmashauri 26 zilikusanywa zikiwa na maudhui ya kufundisha Hesabu na kuhesabu.

“Shindano hilo liliwalenga walimu wa awali na msingi wanaofundisha kuhesabu na hisabati. Mahiri za kufundisha za kufundisha zilizochaguliwa ni Geometri, Aljebra, namba kamili na takwimu,” amesema.

Umahiri wa matumizi ya teknolojia, mawasiliano mazuri na wanafunzi, mbinu za kushawishi wanafunzi kupenda somo ni miongoni mwa vigezo vilivyoangaliwa.

DK Komba amevitaja vigezo vingine ni tathmini ya kupima iwapo wanafunzi wameelewa, huku Mei 22 ndiyo iliyokuwa siku ya mwisho ya kupokea kazi.

Kwa mujibu wa Dk Komba, video 99 zilikusanywa na kufanyiwa tathmini kwa awamu tatu hadi kupatikana video 18.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi