Connect with us

Kitaifa

Samia asema nchi haitauzwa

Dar es Salaam. Sakata la makubaliano ya ushirikiano wa uendelezaji maeneo ya bandari nchini baina ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai limeendelea kuibua mjadala huku Rais Samia Suluhu Hassan akisema, “Tanzania haiuziki”
Rais Samia alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na waliojitokeza kumpokea jijini Mwanza alipowasili kuanza ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo na kushiriki tamasha la kimila la Bulabo, linalowakutanisha machifu wote nchini.

Mkuu huyo wa nchi alitumia dakika zisizozidi tano kuwasalimia na kuwashukuru kwa mapokezi makubwa kwenda kushiriki tamasha hilo leo, ambalo miaka miwili iliyopita lilimsimika na kumpa jina la Chifu Hangaya.

Akihitimisha hotuba yake fupi Rais Samia alisema, “salamu moja kubwa ni kwamba mama huyu ni Mtanzania, atafanya kila analoweza kufanya Tanzania iendelee.

“Tanzania ni moja, haigawanyiki wala haiuziki. Kwa hiyo ndugu zangu mama ni Mtanzania, maendeleo yetu ndiyo muhimu, kila linalofanyika ni kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania,” alisema huku akishangiliwa na wananchi.
Akizungumzia maneno hayo ya Rais Samia, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) Dk Paul Loisulie alisema, kauli ya Rais Samia imelenga kutuliza upepo unaovuma katika nchi kutokana mkataba wa Dubai na Tanzania ambao umeibua hisia mseto kwa wananchi kudai nchi imeuzwa.

“(Rais) anafahamu joto lililopo katika nchi, kwa hiyo ameibuka kuhakikisha joto linatulia, jambo la pili amewahakikishia watu hakuna baya litakalotokea kwenye huo mkataba.

Kwa ujumla kauli yake imelenga kwenye mkataba wa DP World kwa sababu mkataba umejadiliwa kwa hisia kubwa sana,” alisema.
Wakati Rais Samia akieleza hayo, jijini Dar es Salaam viongozi wa dini kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) walikutana kujadili suala hilo na kuipa jukumu Serikali.

Mkutano wao uliofanyikia makao makuu ya TEC, Kurasini na kuhudhuriwa pia na timu ya wataalamu wa Serikali ikiongozwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.

Mwisho wa kikao hicho, viongozi hao wa dini waliitaka Serikali kwenda kwa wananchi kufafanua vifungu vilivyoibua mjadala ili kuwatoa hofu na kurekebisha kasoro zitakazobainika kwenye mkataba kati ya Tanzania na Dubai.
Jumamosi iliyopita, Bunge lilipitisha azimio hilo licha ya mjadala na ukinzani mkali nchini, ukiwahusisha wananchi wa kada tofauti wanaohoji kuhusu uwekezaji huo wa bandari na wengine wakilitaka kutoupitisha.

Uwekezaji huo utahusisha Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na Kampuni ya Dubai Port World (DPW) inayomilikiwa na Serikali ya Dubai.
Baada ya majadiliano yaliyomalizika jioni, Katibu Mkuu wa TEC, Padri Charles Kitima alizungumza na waandishi akisema baadhi ya viongozi wa dini walikuwa hawajui kampuni ya DP World ilipatikanaje, lakini Serikali imeeleza kwamba ilimtafuta mwekezaji waliyedhani ni mbobezi katika biashara ya bandari.
“Viongozi wa dini wamehimiza kwamba hayo waliyoogea na sisi, waende wakayatoe kwa wananchi wakielezea hofu za wananchi, kuwa kipengele hiki tunakijibuje, kipengele hiki tunakijibuje, wananchi wajisikie kuridhishwa,” alisema.

Padri Kitima alisema tangu Tanzania ipate uhuru, wananchi waliaminishwa kwamba maliasili zote ni zao, kwa hiyo mtu anapoitumia kinyume na matarajio ya raia wote, wananchi hawawezi kukubali. Alisema wameomba hilo lisipuuzwe kwa sababu ndivyo walivyoambiwa.

“Kwa hiyo tumeomba Serikali ikawape wananchi maelezo vizuri, wakiwapa na mifano. Hata huu mkataba wa Inter Governmental Agreement (IGA) si wa kwanza, kumbe ilishakuwepo, hata kupangisha, Ticts alipangishwa miaka mingi.

“Hayo ni mambo ambayo tungependa Serikali iwape wananchi ufafanuzi mzuri. Bado tunachukua maoni ya wananchi yanayowakera, tuna wataalamu wetu watatuandikia moja baada ya jingine na Waziri (Profesa Mbarawa) amesema tuwapelekee,” alisema kiongozi huyo wa TEC aliyezungumza kwa niaba ya viongozi wa dini.

Alisisitiza Serikali imewahakikishia kwamba pamoja na Bunge kupitisha mkataba huo, bado unarekebishika, kwa hiyo vile vifungu tata wameona wavifanyie kazi.

“Sisi tutafuatilia na viongozi wa dini watahakikisha sauti za wananchi hazipuuzwi kwa sababu nchi hii ni mali ya Watanzania zaidi ya milioni 60,” alisema Padri Kitima.

Awali, wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Padri Kitima alisisitiza umuhimu wa wananchi kusikilizwa kwa kila wanachokisema badala ya kuwaona kama wasiojua chochote kwa sababu hii ni nchi yao na wao ndiyo wanaiweka Serikali madarakani.
Alisema wanaamini kwamba ardhi ya Tanzania ni ya wananchi wote na mtu atapewa kwa mujibu wa sheria zilizopo, hivyo Watanzania hawako tayari kuona mtu anapewa ardhi hiyo kwa upandeleo fulani.

“Tunaomba sana suala la ardhi wananchi wasikilizwe, sitoi pendekezo lakini mtakapokuwa mnajadili, ibara ya 8 ya mkataba huu, hilo liangaliwe.

“Muone vitu ambavyo wananchi hawajapenda ili kubalance (kuweka swa) kwamba hiki hawajapenda. Bandari ya Dar es Salaam tumeweka Sh1 trilioni, unampa mtu aje aendeshe, kwa nini sisi tusijenge uwezo wetu tukaendesha,” alihoji Katibu huyo wa TEC.
Alisisitiza uzoefu unaonyesha pale wananchi walipolazimishwa jambo hakuna amani, akitolea mfano nchi za Sudan na Somalia ambako zimetawaliwa na mapigano licha ya wingi wa rasilimali za mafuta na gesi mtawalia.

Padri Kitima alisisitiza kwamba ibara ya 4, 5, 6 na 8 (kwenye mkataba) ni muhimu sana, hivyo zinapaswa kuangaliwa kwa umakini.

“Pale unapoambiwa Serikali italazimika kuipa taarifa DP World kuhusu fursa nyingine zitakazopatikana, yaani huruhusiwi kuwaambia wengine, uwaambie kwanza wao.

“Serikali itawajibika kuwaondoa watu katika maeneo (DP World) wanayoyataka. Kwa hiyo akiamua Kanisa la St Joseph (lililopo karibu na bandarini) litolewe, Serikali itafanya.

Mambo kama hayo ndiyo watu wanataka waelimishwe,” alisema Padri Kitima.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma alisema viongozi wa dini wamepata ufafanuzi wa kina juu ya maswali ambayo wengi wamekuwa wakijliza huku wakitaka serikali itoe zaidi elimu kwa wananchi kuhusu mkataba huo na kampuni ya DP World.

“Tumepata majibu ya maswali mengi ikiwemo suala la je, bandari yetu imebinafsishwa, mkataba umeingiwa usio na kikomo cha muda maalumu, umezingatia masilahi ya nchi, yote hayo yamejibiwa na yale yote ambayo hatujaridhishwa na majibu yake tumeomba viongozi waendelee kutoa taarifa zaidi lakini elimu zaidi kwa wananchi ambao hawajui nini kinachoendelea ili jambo hili lifahamike.

‘Fikisheni ujumbe sahihi’

Profesa Mbarawa alisisitiza lengo la mkataba huo kuwa wa kuweka msingi wa majadiliano kwa kuzingatia masilahi ya Taifa.

Alisema mkataba huo umeweka msisitizo kwenye mambo muhimu kama vile ajira kwa Watanzania, ukomo wa mkataba wenyewe pamoja na ulinzi wa Taifa.

Alisisitiza wakati wa utekelezaji wa mkataba huo, watazingatia masuala mbalimbali kama vile kuweka bayana ukomo wa mkataba, muda wa marejeo ya utekelezaji, mikataba itasainiwa kwa usimamizi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mifumo ya kampuni ya DP World itasomana na mifumo ya Serikali.

Katika hatua nyingine, Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi amesema ni muhimu Serikali ikiri kukosea na kufanyia kazi dosari zinazopigiwa kelele na wadau mbalimbali kwenye mkataba huo.

Askofu Niwemugizi alisema pamoja na Bunge kuridhia makubaliano hayo huku likiwaomba wananchi iwaamini, imani hiyo haiwezi kuondoa sifa ya binadamu kukosea hivyo ni lazima awepo mtu wa kuonyesha makosa. Alisema mkataba baina ya Tanzania na DPW ulisainiwa mwaka jana Oktoba lakini mwaka huu ndio ukaonekana kuwepo kwa haja ya Bunge kuridhia ndipo ianze kutumika jambo ambalo alidai linakanganya.

“Naomba wenye sifa waufikishe mjadala huu kwa Mhimili wa Mahakama. Ingawa huko nako, itategemea kama mhimili utakuwa na ujasiri wa kutomtazama usoni anayewateua waamuzi,” alisema.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi