Connect with us

Kitaifa

Usiyofahamu kuhusu mmiliki wa Precision Air

Rombo. Wakati jamii ikiomboleza kifo cha mwanzilishi na mwenyekiti wa bodi ya Kampuni ya Shirika la Precision Air, Michael Shirima, imeelezwa namna alivyothubutu kujiuzulu kazi na kwenda kuchoma nyama.

Shirima (80), mzaliwa wa Rombo mkoani Kilimanjaro, alifariki dunia Juni 9, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa tangu Juni 8, mwaka huu.

Msemaji wa familia, Abdallah Singano alisema mwili wa Shirima utasafirishwa kutoka Dar es Salaam Jumatatu kwenda Arusha, utaagwa Jumanne na kusafirishwa kwenda Rombo kwenye maziko yatakayofanyika Jumatano.

Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda, akizungumzia maisha ya Shirima alisema ameacha historia nzuri kwa Taifa kwa kuwa alikuwa mtu asiyekata tamaa, licha ya changamoto alizopitia.

Profesa Mkenda ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, alisema kitabu alichoandika Shirima na kukizindua mwaka 2022 ‘On my father’s wings’ kinaelezea historia ya maisha yake na uamuzi mgumu aliochukua wa kujiuzulu Shirika la Ndege la Tanzania mwaka 1979.

“Niliwahi kumuuliza ni kwa nini aliacha kazi Air Tanzania, aliniletea barua zake kwa nini alitaka kujiuzulu na mpaka leo nina nakala yake, alivyoona shirika linayumba na kuwatahadharisha kwamba litakufa wakiendelea vivyo hivyo, hawakumsikiliza, hivyo akaamua kujiuzulu.

“Alipofika nyumbani mke wake alishtuka sana, lakini wakati huo walikuwa wanakaa nyumba ya Serikali, alikuwa hana kazi, ikabidi aondoke akatafute mahali pa kujishikiza yeye na familia yake, baadaye alianza kufanya biashara ya kuuza nyama choma kidogo kidogo,” alisema Mkenda.

“Alitafuta mkopo akaanza kununua mafuta ya pamba na alipata lori akaanza kuchukua mafuta kutoka Mwanza kuja kuuza Moshi. Wakati anafanya biashara hiyo akagundua Mwanza kuna ujenzi mwingi, lakini mbao zipo upande wa Moshi, akawa anachukua mbao Moshi na kupeleka Mwanza na kurudi na mafuta, alifanya kazi ngumu.”

Alisema kwa kushirikiana na mtu mwingine aliyemtaja kwa jina la Kisinani walianza biashara ya kupeleka kahawa nje ya nchi na siku moja rafiki yake huyo alimwambia kuna mtu anahitaji ndege ndogo kwa ajili ya kufanya kazi shambani.

“Hivyo akaanza na ndege ndogo ya kukodi, baadaye akanunua nyingine, ndivyo alivyoendelea mpaka alipofikia leo,” alisema Profesa Mkenda.

Alisema atamkumbuka Shirima kwa namna alivyokuwa mtu wa dini na hata alipofikwa na changamoto za biashara alikuwa akifunga novena siku tisa akiomba.

Rais aomboleza

Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter ameandika, “Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Michael Ngaleku Shirima, mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Precision Air.

“Baada ya utumishi wake kwa umma kwa zaidi ya miaka 30 amekuwa sehemu muhimu katika biashara ya anga na shughuli za kijamii katika nchi yetu. Natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki.” Mwenyezi Mungu amweke mahali pema. Amina.”

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi