Kitaifa
Mbarawa aeleza sababu Serikali kuichagua DP World
Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameeleza sababu za Serikali kuichagua kampuni ya DP World ya Dubai kuja kuendesha Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na uzoefu wa kampuni hiyo katika kazi.
Profesa Mbarawa amebainisha hayo leo Jumamosi Juni 7, 2023 wakati akitoa maelezo ya awali bungeni yakihusu mapendekezo ya kuridhia mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari Tanzania.
Amesema kutokana na changamoto za bandari zilizopo na kwa kuzingatia dhima ya Serikali ya kuboresha sekta ya bandari nchini ili kuongeza ufanisi na mchango wake katika mapato ya nchi, ajira na kuchagiza sekta nyingine za kiuchumi; Serikali ilifanya uamuzi wa kutafuta wawekezaji wapya wanaoendana na dhima ya Serikali.
Waziri Mbarawa amesema hatua hizo zilihusisha kupokea mapendekezo ya wawekezaji wakiwemo kampuni ya Hutchson (Hong Kong), Antewerp/Brugge (Belgium), PSA International (Singapore), DP World (Dubai), Abu Dhabi Ports (Abu Dhabi), Adani Ports and Logistics (Mundra-India), CMA-CGM (France) na Maersk (Denmark).
“Katika kupitia mawasilisho ya kampuni hizo pamoja na sifa zao kimataifa, Serikali iliamua kuanzisha majadiliano na DP World kwa kuzingatia uzoefu wake katika uendeshaji wa shughuli za bandari barani Afrika, Asia, Ulaya na Amerika ya Kaskazini na Kusini.
“Kampuni hii ina uzoefu na utaalamu wa kuchagiza mnyororo mzima wa usafirishaji kutoka maeneo ambayo bidhaa zinatoka mpaka kufika kwa walaji. Uendeshaji wa maeneo maalumu ya kiuchumi karibu na bandari, usafirishaji baharini na nchi kavu (kupitia njia ya reli), uwekezaji mkubwa katika maeneo mbalimbali ambayo imewekeza na pamoja kuajiri wazawa katika maeneo hayo,” amesema.
Profesa Mbarawa amesema kwa upande wa kampuni nyingine ambayo TPA ilipokea mapendekezo yao, yalionesha nia ya kuwekeza bandarini pekee na siyo kuchagiza mnyororo mzima wa usafirishaji.
Pia, amesema baadhi ya kampuni hizo hazina uzoefu wa kuendesha shughuli za bandari barani Afrika wakati Kampuni ya DP World inaendesha takribani bandari sita barani Afrika na zaidi ya 30 duniani kote kwa ufanisi mkubwa.
“Kwa kuzingatia nia ya Serikali kuvutia uwekezaji nchini, wakati wa maonyesho ya Dubai Expo 2020 Februari 28, 2022, hati za makubaliano takriban 30 zilisainiwa baina ya taasisi za Serikali ya Tanzania na sekta binafsi na taasisi za Serikali za Dubai kwa lengo la kuvutia uwekezaji nchini ili kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi.
“Moja kati ya hati ya makubaliano hayo ni baina ya TPA na DP World iliyolenga kuanzisha ushirikiano wa uboreshaji, uendeshaji na uendelezaji wa maeneo ya bandari nchini,” ameeleza waziri huyo.