Kitaifa
Bunge lapitisha azimio kuhusu mkataba na DP World
Dar es Salaam. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha azimio kuhusu pendekezo la kuridhiwa kwa mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kwa lengo la kuanzisha ushirikiano katika uendelezaji wa maeneo ya bandari nchini.
Pendekezo hilo lililowasilishwa bungeni leo Jumamosi Juni 10, 2023 limepitishwa na Bunge baada ya wabunge kupata fursa ya kuchangia na kuishauri Serikali kuhusu mkataba huo.
Kabla ya wabunge kuchangia, Waziri wa Ujenzi na uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alipata nafasi ya kuuelezea mkataba huo na manufaa yake kwa Taifa na kufafanua hoja zilizoibuliwa na wadau ikiwemo ya muda wa utekelezaji wake.
Kamati ya Bunge ya Miundombinu, pia ilitoa ushauri wake kwa Serikali ikiwemo kuzingatia suala la ukomo wa muda katika mikataba itakayoingiwa, jambo ambalo linalalamikiwa na wadau kwamba makubaliano hayo hayajaonesha ukomo wa muda.
“Waheshimiwa wabunge wanaoafiki hoja iliyowasilishwa kwetu na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kuhusu pendekezo la kuridhiwa kwa mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kwa lengo la kuanzisha ushirikiano katika uendelezaji wa maeneo ya bandari nchini, waseme ‘ndiyo’,” Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliwahoji wabunge.
Wabunge wengi walijibu “ndiyo”, huku kukiwa hakuna wabunge wasioafiki hoja hiyo, hivyo Spika Tulia ameeleza kwamba “nadhani walioafiki wameshinda” huku Bunge zima likipiga makofi baada ya azimio hilo kupitishwa.
“Nitumie fursa hii kutangaza kwamba Bunge limepitisha rasmi azimio kuhusu pendekezo la kuridhiwa kwa mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kwa lengo la kuanzisha ushirikiano katika uendelezaji wa maeneo ya bandari nchini,” amesema Spika Tulia.