Kitaifa

Rais Samia ateua viongozi wa Taasisi za umma, yumo Profesa Makubi

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa Taasisi za umma akiwemo Profesa Abel Makubi ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Juni 8, 2023 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus, uteuzi huo umeanza Juni 6, 2023.

Katika uteuzi huo, Rais Samia amemteua Profesa Makubi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa (Moi) akichukua nafasi ya Dk Respicious Boniface ambaye amemaliza muda wake. Dk Makubi aliwahi pia kuwa Mganga Mkuu wa Serikali.

Vilevile, Rais Samia amemteua Omar Issa kuwa Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST). Issa anachukua nafasi ya Makamu wa Rais mstaafu, Dk Mohamed Ghalib Bilal ambaye amemaliza muda wake.

Katika uteuzi huo, amemteua pia Abdulhamid Yahya Mzee kuwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC). Dk Mzee ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, anachukua nafasi ya Marten Lumbanga ambaye amemaliza muda wake.

Rais Samia amemteua pia Dk Edwin Mhede kuwa mwenyekiti wa bodi ya Benki ya NMB kwa kipindi cha pili.

“Uteuzi huu umeanza Juni 6, 2023,” inaeleza taarifa hiyo ya Ikulu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi