Kitaifa
BoT yashtuka uhaba wa dola
Dar es Salaam. Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema kuna ugumu kwa nchi kuweka kando matumizi ya dola na Tanzania inachukua hatua mbalimbali kukabiliana na upungufu wa sarafu za kigeni.
Alisema hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa zinaifanya Tanzania kuwa salama dhidi ya changamoto ya upungufu wa sarafu za kigeni ulioathiri nchi nyingi.
Miongoni mwa mataifa yaliyoathirika na upungufu wa dola ni Ghana, Misri, Zimbabwe, Nigeria na Kenya, ambayo baadhi yanafikiria kuweka kando matumizi ya dola katika biashara zake.
Hivi karibuni wakati wa mdahalo wa wadau wa sekta binafsi barani Afrika uliofanyika jijini Nairobi, Rais wa Kenya, William Ruto alitoa wito kwa mataifa ya Afrika kuwa na mfumo wao wa malipo na kuweka kando matumizi ya dola.
“Hivi karibuni nilikuwa na mazungumzo na Rais wa benki ya AfriExim, wametengeneza mfumo ambao wafanyabiashara wetu wanaweza kununua kwa kutumia sarafu za ndani.
Tukitumia mfumo huo hatuna haja ya kutafuta dola, wafanyabiashara wetu watajikita zaidi katika kusafirisha bidhaa na huduma na sio kuhangaika na kupata sarafu fulani ili kurahisisha malipo,” alisema Ruto.
Akizungumza na Mwananchi, Tutuba alisema licha ya akiba ya fedha za kigeni kupungua nchini, hakuna changamoto hadi sasa.
Alisema Tanzania kila siku inauza hadi wastani wa dola milioni mbili, kiwango ambacho hakifikiwi na nchi yoyote katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hadi Mei, mwaka huu, Tanzania ilikuwa na akiba ya fedha za kigeni ya Dola bilioni 4.88 zinazotosha kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi minne na nusu, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Hata hivyo, alisema kiwango hicho kimepungua kutoka dola 6.38 bilioni zilizokuwa zinatosha kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi 6.6.
“Tofauti na uchumi wa nchi nyingine, sisi tuna bahati bado mzunguko wa dola upo katika hali nzuri, tunapata fedha nyingi za kigeni kwa sababu mauzo yetu nje ya nchi yanakwenda vizuri, utalii unafufuka sasa na fedha za mikopo na misaada kutoka nje ya nchi zinaongezeka,” alisema Tutuba.
Alisema Tanzania na mataifa mengine huko duniani, mzunguko wake wa dola zinazoingia katika uchumi uliathiriwa na mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19, vita vya Russia na Ukraine na mabadiliko ya tabianchi yaliyoathiri shughuli za kiuchumi na kuharibu miundombinu.
“Uviko-19 na vita vya Russia na Ukraine viliathiri mnyororo wa usambazaji, hivyo watu wakatumia dola zaidi kupata mahitaji yao. Mabadiliko ya tabianchi yalisababisha ukame na mafuriko katika baadhi ya maeneo, hivyo watu kulazimika kuagiza vyakula na vifaa nje ya nchi, yote hayo yanahitaji dola,” alisema Tutuba.
Vilevile suala la kupungua kwa ukwasi wa fedha za kigeni katika mataifa mengi, lilitokana na hatua iliyochukuliwa na Marekani katika kukabili mfumuko wa bei, hatua hizo zilivuta dola zilizokuwa nje ya Marekani kurejea kwa kuwa ndani ya Taifa hilo fedha zilikuwa zinapunguzwa kwenye mzunguko.
Marekani iliongeza riba ya mikopo inayotolewa na Benki Kuu kutoka asilimia 1 hadi 4.75 ndani ya muda mfupi.
“Ukiangalia sababu zote zilizofanya kupungua kwa ukwasi wa dola katika nchi nyingi ni zile ambazo sisi hatuna uwezo nao, lakini bahati nzuri bado tupo pazuri na tumechukua hatua ya kudhibiti athari hasi zinazoweza kujitokeza baadaye endapo hali itaendelea,” alisema gavana huyo.
Kilichofanyika
Gavana Tutuba alisema pamoja na hatua ambazo zitasomwa na Waziri wa Fedha na Mipango katika hotuba yake ya bajeti wiki ijayo, tayari kuna hatua zimechukuliwa, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ununuzi wa bidhaa za ndani kwa zile zinazopatikana na kuongeza uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya matumizi ya ndani na mauzo nje ya nchi.
“Tunalenga kupunguza utegemezi wa kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje, bidhaa zinapopatikana hapa ndani tunapunguza msukumo wa kutakiwa kuwa na dola za kutosha kwa ajili ya manunuzi ya nje,” alisema Tutuba, ambaye kabla ya nafasi aliyonayo sasa alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Alisema bodi ya wakurugenzi ya BoT ikiongozwa naye hivi karibuni ilianza kutembelea maeneo ya kimkakati yanayotazamwa kuongeza thamani ya mauzo ya Tanzania nje ya nchi, hivyo kuongeza mapato ya fedha za kigeni.
“Bodi ikiongozwa nami tulitembelea maeneo ya kimkakati ya viwandani, maeneo ya uongezaji wa thamani ya madini na mashamba makubwa, leo lilikuwa ni kuangalia mahitaji ya wawekezaji hao, nini wanahitaji kuongeza uzalishaji na mauzo ya nje, tulitaka kujua kama kuna eneo lolote, hususani la kifedha wanahitaji tuwashike mkono,” alisema Tutuba.
Alisema lengo ni kuongeza uzalishaji wa ndani na thamani ya mauzo nje ya nchi, hivyo BoT imefanya mipango ya kuwawezesha wenye uhitaji kupitia dhamana ya benki na viwango vitatofautiana kati ya bidhaa moja na nyingine.
“Mfano tulitembelea kiwanda cha sukari cha Bakhresa Bagamoyo, akianza uzalisha yule anapunguza nakisi iliyokuwepo, hivyo hatutumii tena fedha za kigeni kununua kiwango hicho cha sukari. Vilevile tulitembelea kiwanda cha kuchenjua dhahabu, hicho kikianza kitakuwa kinatoa dhahabu kamili kwa asilimia 80, hivyo thamani ya mauzo itaongezeka,” alisema Tutuba.
Alisema hatua hizo na zile zilizochukuliwa hivi karibuni na chombo hicho kikuu cha fedha nchini juu ya udhibiti wa ubadilishaji wa fedha zinalenga kuiepusha Tanzania katika Changamoto ya kupungua kwa ukwasi wa dola.
Tutuba alisema Tanzania ipo katika mfumo wa soko huria kibiashara, tabia iliyokuwa imeanza kuzuka kwa watu kuingiza sokoni dola kwa kiwango cha kubadilishia wanachotaka wao ungeathiri utulivu wa soko na kuleta uhaba wa dola na kudhoofisha shilingi.
“Mtu alikuwa anakuja na dola laki 5 anasema anaziuza kwa bei bei ya Sh2,400 badala ya Sh2,350 iliyopo sokoni, akikutana na uhitaji watu wananunua, akitoka hapo akija tena atataka auze kwa Sh2,500 hadi 2,800 kadiri soko linavyoitikia, tukasema hapana, ni lazima soko lidhibitiwe ili hata hao madalali wa nje wanapokuja wakute utaratibu,” alisema.
Alisema hatua ya kutaka kila muuzaji afuate utaratibu itasaidia kudhibiti dola bandia, lakini vilevile kuonyesha nchi kuwa haikubaliani na utakatishaji wa fedha.
Aliongeza kuwa BoT inaendelea kusisitiza wenye mitaji kuomba leseni ya kuendesha biashara ya kubadilisha fedha badala ya kutumia njia zisizofaa kibiashara.
Kuikacha dola
Tutuba alisema kuna ugumu wa kuweka kando matumizi ya dola, huku akitaja athari za kufanya hivyo kwa uchumi, akisema sarafu ya dola inatumiwa katika biashara za kimataifa kutokana na sifa ilizonazo, kubwa ikiwa ni kutabirika kwake.
“Dola inachangia asilimia 83 ya thamani ya miamala yote inayofanywa kwa ajili ya biashara za kimataifa, inaaminiwa sawa na watu kila mahali na ina sifa kubwa nyingine ya kutumika kama hifadhi ya ukwasi, kwani katika benki kuu zote duniani dola zilizohifadhiwa ni asilimia zaidi ya 60 ya fedha zote za kigeni,” alisema.
Kuhusu makubaliano ya nchi na nchi kutumia sarafu zao, alisema ni jambo la kuwa nalo makini, hususani kama urari wa biashara kati ya nchi zinazofanya makubaliano hauendani.
“Ndiyo maana unaona sisi tumetulia, kama nchi inaagiza zaidi kuliko inavyouza nje, tofauti ya urari wa biashara itatakiwa kulipwa, hata hivyo inalipwa kwa fedha za kigeni ambayo huenda ikawa dola. Hili suala la kuenda nalo kwa umakini sana,” alisema Tutuba.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Thobias Swai alisema Dola inakuwa lulu kwa,kuwa imepewa thamani hiyo, ukipatikana mbadala wake msukumo wa uhitaji wake utapungua.
Alisema inawezekana kwa nchi kuacha au kupunguza matumizi ya sarafu hiyo inayokubalika kwa wengi duniani lakini muhimu ni kuwa mbadala wake ambao unaaminiwa (sarafu inayoweza kutumika na kukubalika sokoni).
“Mbadala wa haraka kwa mataifa ni kuwa na sarafu ya kidijitali kama inayosimamiwa na Benki Kuu. Kukiwa na utaratibu huo nchi haitakuwa na sababu ya kuhifadhi dola au sarafu nyinginezo za kigeni kwa ajili ya kujihakikishia manunuzi ya nje,” alisema.