Kitaifa

TPA yatoa ufafanuzi uwekezaji wa DP World bandari ya Dar

Dar es Salaam. Wakati mjadala kuhusu Azimio la Serikali ya Tanzania kuingia makubaliano na Serikali ya Dubai kwa ajili ya uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam ukipamba moto, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imekanusha baadhi ya mambo na kuwataka Watanzania kutosikiliza kile inachoita upotoshaji.

Ufafanuzi wa TPA umekuja ikiwa imepita siku moja tangu Kamati ya Bunge ya Miundombinu na uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ikipokea maoni ya wadau bungeni jijini Dodoma.

Taarifa ya TPA iliyotolewa jana Juni 6 kupitia mitrandao ya jamii, imesema madai kuwa Serikali ina mpango wa kuipa kampuni ya DP World ya Falme ya Dubai kandarasi yakuendesha bandari ya Dar es Salaam kwa miaka 100 siyo za kweli.

“Azimio la Bunge linalohusu mkataba ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaingia a Serikali ya Dubai wenye ukomo wa miezi 12 kwa ajili ya kutoa nafasi ambayo Serikali hizo mbili mbili zinaweza kushirikiana katika uboreshaji wa sekta ya bandari nchini Tanzania,” imesema taarifa hiyo.

TPA imefafanua kuwa ushirikiano wa nchi hizo mbili unalenga la kukuza ajira za Watanzania na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kupitia uwekezaji kwenye baadhi ya maeneo ya bandari ya Dar es salaam, maeneo huru ya kiuchumi na viwanda na mnyororo wa usafirishaji kwenda nchi jirani.

Wakosoa

Hata hivyo, baadhi ya wadau wamekosoa makubaliano hayo tangu manufaa yanayoelezwa hadi mchakato unaofuatwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Akiandika andiko lake mitandaoni, Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya ushauri wa Kitaalamu sekta ya uziduaji ya Fordia, Bubelwa Kaiza ametaka kuwe na umakini katika suala hilo.

“Utaalam na teknolojia ni mambo yanazonunuliwa sokoni. Thamani ya kiuchumi ya TPA ni kitu kikubwa cha karibu kwa nchi yetu katika bahari ya Hindi na maziwa Makuu ya Afrika. Hiyo ndiyo inaitofautisha Tanzania na nchi nyingine. Tukiisha kuipoteza thamani hii hatutakuwa na thamani tena,” amesema.

Amesema njia bora ya kuimarisha ufanisi TPA kwanza ni kubadilisha uongozi wake ili nafasi za juu za uongozi zijazwe kwa kuzingatia vigezo vya umahiri na matokeo ya ushindani katika soko la kazi.

“Bila kujali iwapo mtendaji mkuu na timu yake ya menejimenti ni raia wa Watanzania au wageni, maadam wameshindana na kudhihirisha umahiri wa kusimamia uendeshaji wa kazi za TPA.

“Mfumo na muundo wa TPA uwekwe bayana kuwa na CEO (ofisa mtendaji mkuu) na timu yake wawe na mamlaka ya kupendekeza, kwa mujibu wa sheria ya manunuzi, kununua na kutumia teknolojia na vifaa (machinery & equipment) vya kuendesha bandari kwa ufanisi pasipo kuingiliwa na mamlaka za serikali,” amesema.

Amesema kama serikali inaona kuna umuhimu wa kubinafsisha TPA basi iweke na kutangaza utaratibu wa kuuza hisa za TPA kwenye soko la mitaji la Dar es Salaam (DSE).

Kwa upande wake aliyewahi kuwa Meya wa Ubungo na kada wa Chadema, Boniface Jacob aliandika katika ukurasa wake wa twitter akikosoa kamati ya PIC kuitisha mkutano wa maoni kwa muda mfupi.

“Usanii ni Kamati ya Miundombinu na uwekezaji wa Mitaji ya Umma kutoa Short notes (taarifa ya muda mfupi) jana (juzi) kuwataka watu wenye maoni kufika Dodoma leo (jana) mchana, wakijua haiwezekani.”

Kwa upande wa Wakili Jebra Kambole aliandika katika Twiter, “Yaani Tangazo unatoa tarehe 5 June 2023, unataka maoni June 6, 2023, siku moja mtu ajiandae na kusafiri kuja Dodoma kutoa maoni? Siku moja?”

Mwingine aliyechangia mjadala huo Twiiter alikuwa Patrick Nandi aliyesema, “Ikiwa uongozi wa TPA umeshindwa kuwa effective (imara) na Waziri ameidhinisha…Mhe Rais Samia Suluhu Hassan, ikikupendeza vunja menejimenti/bodi.

“Maana haya mawazo ya makubaliano ya namna hii yanafitinisha Serikali na wananchi. DP World watachofanya ni uwekezaji tu; nini kinawashinda TPA kufanya?

“Wameshindwa kutumia e-government kuwa full in digital maana kwa Dubai port ndicho kikubwa ‘automation’. hili likipita Bungeni itakuwa historia yenye maswali yasiyojibika.”

Kwa mujibu wa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, Serikali imeichagua kampuni ya Kimataifa ya huduma za bandari Dubai Port World (DPW) kutoka Dubai kwa lengo la kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 233.7 katika kipindi cha miaka 10 ijayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi