Kitaifa
Mabehewa ya ghorofa SGR yawasili
Dar es Salaam. Unaweza kusema ni kama Ulaya vile, na asiye na mwana aeleke jiwe, hii ni baada bandari ya Dar es Salaam kupokea, mabehewa sita ya ghorofa yakitokea nchini Ujerumani yatakayotumika katika reli ya mwendo kasi (SGR).
Kuwasiri kwa mabehewa hayo ambayo ni sehemu ya mabehewa 30 yanayotarajiwa, yana uwezo wa kuhudumia abiria 123 na 140 wa daraja la pili na la tatu, huku mabehewa 24 yaliyosalia na vichwa viwili, vitawasili nchini baada ya matengenezo yake kukamilika.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Shirika la Reli Tanzania (TRC) Jamila Mbarouk, mabehewa hayo yameboreshwa na kampuni ya Luckmier Transport & Logistic ya Ujerumani ambapo TRC inatarajia kuyapokea rasmi Juni 9, 2023.
“Mabehewa sita tayari yamewasili bandari ya Dar es Salaam, TRC inakusudia kuyapokea mabehewa haya sita siku ya ijumaa Juni 9, 2023, na yale 24 yaliyosalia, yatapokelewa mara tu yatakapowasili nchini ya kukamilika kwa ukarabati wake ambao unanfanywa na kampuni ya ya Luckmier Transport & Logistic ya Ujerumani,” amefafanua Jamila.
Siku ya Ijumaa June 2, 2023 Mwananchi Digital ilizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, kutaka kujua ni lini safari za Dar es Salaam hadi Morogoro zinatarajiwa kuanza baada ya kuwa zimeshindikana mwezi uliopita.
“Kutokana na changamoto zilizo nje ya uwezo wao, wamechelewa, mabehewa yanaendelea kuingia mengine tutapokea wiki hii au ijayo. Na kichwa cha kwanza tunatengemea kitaingia mwishoni mwa mwezi ujao,” alisema Kadogosa, alipokuwa akizungumza na mwandishi kwa simu.
Alisema mabehewa sita ya ghorofa moja yanatarajiwa kuwasili nchini wiki ijayo na yatakuwa na uwezo wa kuchukua watu 150 waliokaa.
Kadogosa alisema vifaa hivyo vinachelewa kuwasili kwa kuwa utengenezaji wake haufanywi na kiwanda kimoja, baadhi ya vitu vinatoka nchi tofauti, hivyo mnyororo wa usafirishaji kutoka nchi hizo umekuwa na changamoto kwa sababu nyingine zimekumbwa na mitikisiko ya kiuchumi na kijamii.
“Njia yetu mpaka sasa inapitika kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma kwa SGR, treni ya umeme inafika Morogoro bila tatizo, upande wa Morogoro mpaka Dodoma, miundombinu ya umeme ipo asilimia 99,” alisema Kadogosa.
Alisema mara baada ya kuwasili kwa vifaa vinavyosubiriwa itakuwa ni mwanzo wa safari hizo, kwani madaraja yanayoendelea kujengwa, ikiwemo la Vigunguti, daraja la Nyerere na daraja la Banana yako zaidi ya asilimia 95 na hivi karibuni yanakamilika,” alisema.
Februari 14, mwaka huu akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Kadogosa alisema ujenzi katika kipande hicho umefikia asilimia 97.91, kazi iliyokuwa imebaki ni ujenzi wa madaraja yanayokatiza kwenye reli yameongezeka tofauti na makadirio ya awali.
Alisema awali hawakuwa wameweka mpango wa njia za kupita wanyama katika maeneo ambayo reli imekatiza kwenye hifadhi, lakini sasa imeonekana umuhimu wa kujenga njia hizo.
Sababu nyingine ya kusogezwa mbele kwa safari hizo ni kuchelewa kuwasili vichwa vya treni, jambo ambalo liko nje ya uwezo wa shirika hilo.