Kitaifa
Daladala Dar kila muda nauli yake
Dar es Salaam. Licha ya nauli halali zilizowekwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra), kuna nyakati abiria jijini hapa hulazimika kulipia usafiri mara mbili zaidi kuepuka adha ya kukaa vituoni muda mrefu.
Changamoto hii kwa watumiaji wa usafiri wa umma, maarufu daladala ni kubwa nyakati za asubuhi, jioni na usiku, ambapo katika baadhi ya maeneo abiria husubiri daladala kwa zaidi ya saa moja.
Kwa kuwa nyakati hizo huwa na abiria katika baadhi ya maeneo, hasa wanaokwenda nje ya mji wakitoka katikati ya mji kwenye shughuli zao za kila siku, makondakta hujitangazia nauli watakayo tofauti na iliyopangwa na Latra.
Kwa nyakati hizo, pia baadhi ya madereva huhama ruti walizopangiwa, kubeba abiria na kujipangia nauli wazitakazo.
Licha ya hayo, baadhi ya abiria ili kupata nafasi ya kukaa na kuepuka msongamano, hulazimika kupanda gari kabla halijafika kituo cha mwisho, hivyo hulipa nauli mara mbili, yaani ya kumalizia safari na kuanza nyingine ya kuelekea walikokuwa wanakwenda.
Magari mengine hupakia abiria kwa makundi, kwanza wale walio tayari kulipa nauli nje ya mfumo wa Latra ambao watakaa na baadaye watakaosimama ambao hulipa nauli rasmi ya Latra au pungufu ya waliokaa kulingana na uamuzi wa kondakta na dereva.
Wakazi wa Mbagala, Gongolamboto, Chanika na Goba wanaotumia usafiri wa daladala kwa kiasi kikubwa hufikwa na kadhia hii.
Latra imepanga nauli kwa mabasi ya Sh500, 600 na 700, lakini asubuhi, jioni na usiku abiria hutozwa Sh1,000 hadi Sh2,000.
Akilifafanua hilo, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Barabara, Johansen Kahatano alisema wananchi hawapaswi kulipa zaidi ya nauli elekezi, huku akiwataka kutoa ushirikiano kukomesha kadhia hiyo.
Alisema licha ya kufanya ziara katika baadhi ya vituo vya daladala kufuatilia suala hilo, baadhi ya watu wamekuwa na majibu yasiyoridhisha kwa maofisa wanaofanya ufuatiliaji, hivyo wanashindwa kuchukua hatua.
“Wakati mwingine mtu anakuambia sisi tunataka kwenda na hela ni yetu. Ikitokea kuna mtu yupo kwenye gari na hataki kulipa nauli zaidi ya anayolipa kila siku, abiria wako tayari kumchangia ili aendelee na safari au ashushwe.
“Abiria wanaweza kuripoti hata kwa kutumia namba yetu ya huduma ya bure kwa kutupa namba ya usajili wa gari na sehemu linakoelekea sisi tutaifanyia kazi,” alisema Kahatano.
Hali ilivyo
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini adha ya usafiri imekithiri katika vituo vya daladala vya Makumbusho, Stesheni, Buguruni na Gongolamboto.
Alhamisi moja katika kituo cha Stesheni abiria wanaokwenda Mbagala Rangitatu, walilazimika kulipa Sh1,000 kama nauli ili kupata usafiri badala ya Sh500.
“Ndiyo hali ilivyo, ikifika saa moja usiku hapa daladala nyingine zinapakia kwa Sh1,000, utachagua usimame hapa saa mbili hadi tatu au upande uende nyumbani kupumzika,” alisema Norah Mziwanda, mkazi wa Mbagala Kwa Kipati.
Alisema hali hiyo kwa sasa imezoeleka na kuongeza: “Ukiwa huna nguvu ni mtihani kupata hata huo usafiri, watu ni wengi huku gari zikiwa chache.”
Hali ni vivyo hivyo katika kituo cha daladala cha Makumbusho, ambako magari yanayofanya safari kwenda Buza na Mbagala hupakia abiria kwa Sh1,000.
“Ikifika saa moja au mbili usiku nauli hupanda kutoka Sh600 mpaka Sh700 au Sh800, wakati mwingine hufika hadi Sh1,000,” alisema Jonas Mnyaturu, mkazi wa Tegeta.
Wakazi wa Mbezi na Kimara wanaotoka Kariakoo nyakati hizo badala ya kulipa Sh600 hutozwa nauli ya kati ya Sh700 na Sh1,000.
Kwa abiria wanaosafiri kati ya Gongolamboto na Chanika hutozwa Sh1,000 badala ya Sh600 iliyoelekezwa na Latra.
“Tumeshazoea, ikifika saa 12 jioni nauli ni Sh1,000, utake utaenda usipotaka utabaki hapa,” anasema Salum Makame, mkazi wa Chanika.
Makame, anayefanya kazi Ubungo anasema kuna wakati hulazimika kutumia Sh2,000 kwa nauli kwenda nyumbani kwake badala ya bajeti yake ya Sh1,200 ya kila jioni.
“Nikipanda gari la Ubungo kwenda Gongolamboto wakati wa jioni nauli inakuwa Sh1,000, nikifika hapa ili nipande la Chanika nauli tena Sh1,000. Gharama za maisha zinaongezeka, hela inaweza kuonekana ndogo lakini kiuhalisia naumia,” anasema Makame.