Connect with us

Kitaifa

Hivi ndivyo vituo 9 ‘Dege’ jipya ATCL litatua

Dar es Salaam. Muda mchache baada ya kuwasili kwa  Ndege mpya ya mizigo ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Ladislaus Matindi ametaja vituo tisa itakayotua ndege hiyo mara itakapoanza kazi ikiwemo Guangzhou nchini China.

“Ndani ya Afrika kwa zile ‘scheduled flight’ tutaenda Nairobi, Harare, Johannesburg, Kinshasa, Lubumbashi, na Lagos. Kwa bara la Asia tutaenda Mumbai, Dubai, na China,” amesema Matindi

Ndege hiyo aina ya Boeing B767-300F yenye uwezo wa kubeba  tani 51 ya mzigo kwa wakati mmoja na kuruka kwa wastani wa masaa saba hadi 10 bila kutua na inalifanya shirika hilo kufikisha jumla ya ndege 13 zinazosimamiwa na taasisi hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam, katika hafla ya mapokezi ya ndege hiyo iliyofanyika leo, June 03, 2023; katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, amesema baada ya kuwasili ndege hiyo wanategemea kuanza kufanya kazi kwenye vituo hivyo kwa safari za ratiba maalum na isyo mahalum hasa pale ambako kutakuwa na uhitaji.

Matindi amesema mpango wa ununuzi wa ndege za mizigo umelenga kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka na kuingia nchini hivyo kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa.

“Ujio wa ndege hii utasaidia kuongeza mnyororo wa thamani wa bidhaa za kitanzania na uwepo wa uhakika wa usafirishaji wa bidhaa na uwepo wa vifaa vya uzalishaji utaongeza thamani na kuzifanya kuwa shindani katika soko la kimataifa,” amesema.

Ameishukuru serikali kwa jitihada za kuliwezesha shirika hilo kuwa na ndege ya mizigo ili kama Taifa lifaidike na fursa zilizopo nchini.

“Kusafirisha minofu ya samaki, samaki wa mapambo na nyama kutoka mikoa ya kanda ya ziwa, Kaskazini na Kati, pia maua, na mbogamboga kutoka nyanda za juu kusini,” amesema.

Amesema eneo la kijiographia nchini linaipa fursa nzuri ndege za shirika hilo kuchukua mizigo ya nchi zingine jirani zinazohitaji kutumia usafiri huo.

Hata hivyo Matindi amesema kampuni hiyo katika kutekeleza mpango mkakati wake wa pili wa miaka mitano ya fedha inahitaji ndege 20 zikiwamo za masafa mafupi nane  masafa ya kati nane na masafa marefu tatu na ndege moja kubwa ya mizigo.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi