Kitaifa
HESLB: Wanafunzi zingatieni mambo haya saba kuomba mkopo
Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetaja mambo saba muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2023/2024 kwa waliomaliza kidato cha sita pale dirisha litakapofunguliwa.
Pia wamesema mwombaji anatakiwa kuhakiki cheti chake cha kuzaliwa kwa kufuata maelekezo ya Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita) au Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA).
Kwa upande mwingine, mwombaji pia atatakiwa kuandaa nakala ya kitambulisho cha mdhamini wake, ambacho kinaweza kuwa kimoja kati ya kitambulisho cha uraia (Nida), kadi ya mpiga kura, leseni ya udereva, pasi ya kusafiria, au kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi.
Vilevile HESLB imeweka bayana kuwa, mwombaji anatakiwa kuandaa picha ndogo za rangi (passport size) na mdhamini wake, pamoja na namba yake ya Nida, na pale ambapo mwombaji hana namba hiyo, bado haitamzuia kuwasilisha maombi ya mkopo huo.
Aidha, Bodi hiyo imewafahamisha waombaji wa mikopo hiyo, kwamba watakua na muda wa kutosha wa siku 90 kwaajili ya kutuma au kuomba mkopo, huku dirisha likitarajiwa kufunguliwa mwezi Julai, 2023.