Kitaifa
Matumizi ya kuni, mkaa vijijini ni asilimia 91-99
Dodoma. Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umejipanga kuhakikisha unawezesha upatikanaji wa nishati safi na salama katika maeneo ya vijijini ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo yamefikia asilimia 91-99.
Hayo yameelezwa Mei 27, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy wakati akitoa mada kwa wabunge kuhusu matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Mhandisi Saidy amesema kuwa nishati ya kupikia hutumiwa na watanzania wengi na kwamba msingi wa kuhamasisha, kuendeleza na kuwezesha matumizi ya nishati hiyo lipo kwenye Ilani ya Chama Tawala (Chama cha Mapinduzi – CCM) ya Mwaka 2020.
Amesema pia lipo kwenye Sera ya Taifa ya Nishati, Sera ya Taifa ya Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ambapo miongozo yote hiyo, inahamasisha matumizi ya vifaa bora, kwenye kutumia nishati safi, salama na endelevu kwa watu wote.
“Na sisi (Wakala wa Nishati Vijijini – REA),Sheria ya REA inatupa wajibu wa kuhakikisha tunawezesha upatikanaji wa nishati safi na salama kwa watu vijijini na si umeme tu, ni nishati zote”. amesema Mkurugenzi huyo.
Mhandisi Saidy amesema utekelezaji wa suala la nishati safi na salama ya kupikia, utaliwezesha Taifa kufikia Malengo la Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya Mwaka 2030 hususan lengo namba saba ambalo linahusu upatikanaji wa nishati safi na ya uhakika, nafuu na endelevu.
Amesema kuwa hali ya matumizi ya mkaa na kuni kwa watu wa vijijini ipo juu na kuongeza kuwa kati ya asilimia 91 hadi 99 wananchi wa vijijni, wanatumia nishati isiyo safi na salama.
Mkurugenzi huyo amesema Serikali itaendelea kuwaelimisha wananchi kutambua nishati safi na salama na nishati chafu na athari zake kiafya, kimazingira, kiuchumi kwa wale wanaotumia nishati chafu.
“REA itaendelea kuwezesha upatikanaji wa nishati safi na salama kwa Watanzania wa vijijini na si umeme tu,”amesema