Kitaifa
Rais Samia amtaka Jaji Mkuu kumulika mahakama za chini
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amedokeza uwepo wa dosari kwa watendaji wa ngazi za chini za mahakama, akitamka Jaji mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma kuelekeza macho yake katika ngazi hiyo ya chini.
Samia amesema hana wasiwasi na ngazi za juu za mahakama kwani jicho la kiongozi hutyo limekuwa karibu.
Kauli hiyo Rais Samia ameitoa leo Mei 23, 2023 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma wakati akiwaapisha majaji sita wa mahakama ya rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Maadili.
“Sina wasiwasi kwa ngazi za juu huku jicho lako lipo karibu zaidi, ngazi za chini wale watendaji wa mahakama tunahitaji macho makali zaidi ngazi za chini mambo bado yanendelea kufanywa hovyo hovyo,” amesema na kuongea;
“Tumesikia kesi ya Lindi kwamba wafugaji wamefanya makosa ya wazi wazi, Jaji akasema anaenda kutazama ili ajiridhishe, aliporudi akasema hawana makossa, sasa utajiuliza kuna nini hapo,” amehoji Rais Samia.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa nchi amesema kuwa kutokana na maamuzi hayo ya mahakama, Mkuu wa Mkoa huo aliyapinga jambo ambalo yeye ametafsiri kuwa ni dosari katika utendaji wa mhimili huo.
Kwa upande mwingine, Jaji Juma amesema pamoja na ongezeko la teknolojia majaji hao hawawezi kupunguza mzigo wa mashauri kama hawezi kufikiria upya utaratibu wa mashauri na taratibu ambazo mashauri yanapitia.
Hivyo, Profesa Juma amewataka majaji hao kutoa maoni yao ya muda ambao unaopashwa kutumika zaidi kwenye mashauri mahakamani.
“Ni jukumu letu sisi kutambua hilo tatizo la kupunguza muda unaotumika mahakamani, mfano katika mahakama ya rufani tuna zaidi ya mashauri zaidi ya 200 inayohusu mabenki,” amedokeza.
Na kuongeza: “Hayo ni mashauri mengi yanayoshikilia fedha za biashara, uwekezaji sasa bahati mbaya, utaratibu tulionao ni wa kila mtu kukimbilia mahakamani badala ya kutuma utaratibu wa kutatua migogoro kwa kutumia usuluhishi ambao kimsing unatumia muda mfupi Zaidi.”
Katika uapisho huo, majaji wa mahakama ya rufani waliopata nafasi hiyo ni Leila Mgonya, Zainab Buruge, Amour Said Khamis, Ben Hajji Sahaban Masoud, Gerson John Mdemu, Agnes Zephania Mgeekwa, Rose Agrey Temba ambaye aliapishwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili.