Kitaifa
Mkutano wa Majaliwa, Wafanyabiashara Kariakoo waiva
Dar es Salaam. Wakati baadhi ya maduka katika eneo la Kariakoo yakiendelea kufungwa kwa siku ya tatu sasa, wafanyabiashara wa soko hilo tayari wamewasili ukumbi wa Arnaoutoglou jijini hapa kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa ajili ya kutatua changamoto zao leo.
Baadhi ya wafanyabiashara hao wa soko hilo maarufu nchini na Afrika Mashariki wamegoma kufungua maduka yao kuishinikiza Serikali kutatua kero wanazoita za kikodi zinazowakabili.
Miongoni mwa kero hizo wanazozidai ni sheria wasiyokubaliana nayo ya usajili wa stoo, kamatakamata ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kubambikiwa kodi kubwa.
Juzi Mei 16, 2023 Majaliwa alifika sokoni hapo kutuliza hali ya hewa baada ya wafanyabiashara hao kugomea kauli ya aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ya kuwaomba waende naye Dodoma kufanya kikao na Waziri Mkuu huku wao wakishinikiza kiongozi huyo ndio afike sokoni hapo.
Sakata hilo likiwa linaingia siku ya tatu, leo Jumatano Mei 17, 2023 nje ya ukumbi wa Arnaoutoglou baadhi ya wafanyabiashara wamejitokeza wakisubiri mkutano na Waziri Mkuu kwa ajili ya kujadili hatma yao
Wakati majadiliano ya wafanyabiashara hao yakiendelea nao askari wapo katika wapo eneo hilo wakilinda amani.