Kitaifa
Ummy awatoa hofu wananchi uwepo wa Uviko-19
Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka wananchi waondoe hofu kuhusu tetesi za uwepo wa ugonjwa wa Uviko-19 huku akiahidi kutoa taarifa rasmi ndani ya wiki moja.
Ummy ameyasema hayo kupitia andiko lake katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram leo Mei 14, 2023.
“Kuhusu tetesi za uwepo wa ugonjwa wa Uviko-19 nawaomba wananchi muondoe hofu. Tunachakata taarifa tulizokusanya kutoka Hospitali/Vituo mbalimbali ndani ya wiki hii tutatoa taarifa kama kuna ongezeko la magonjwa ya mfumo wa hewa au la,”ameandika Ummy.
Aidha, Ummy amesema takwimu za wagonjwa wapya wa Uviko-19 zinaonyesha wamepungua ikilinganishwa na kipindi kilichopita.
“Kwa taarifa za wagonjwa waliopimwa Uviko-19 wiki ya Mei 6 hadi 12, 2023 Watu sita kati ya 288 walithibitishwa kuwa na ugonjwa huo, hii ni pungufu ikilinganishwa na wiki ya Aprili 29, 2023 hadi Mei 5, 2023
Pia, Ummy amesema hakuna kifo chochote kilicho thibitishwa kusababishwa na ugonjwa huo na amesema wizara ya Afya inaendelea kufuatilia kwa karibu kwenye hospitali mbalimbali na watatoa taarifa kamili.
Andiko hilo la Waziri Ummy linakuja baada ya tetesi za kurudi kwa ugonjwa huo nchini huku ukihusishwa na vifo mbalimbali vya watu maarufu vilivyotokea hivi karibuni.