Connect with us

Kitaifa

Ahueni bei ya bando mbioni

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kampuni za simu nchini kuweka gharama nafuu ya vifurushi vya simu, ili wananchi wa vipato vyote wanufaike na huduma hizo.

Pia, Rais Samia aliziagiza halmashauri zote nchini kuondoa urasimu wa utoaji wa vibali vya ujenzi wa minara, ili minara ijengwe ya kutosha, kwani itasaidia kupunguza gharama hizo.

Rais Samia alitoa kauli hiyo jana jijini hapa, ikiwa ni moja ya maagizo saba aliyotoa kwenye hafla ya utiaji saini wa mikataba ya kupeleka huduma ya mawasiliano vijijini, huku akiupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuwa umefanya mageuzi makubwa kwenye sekta hiyo.

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari chini ya UCSAF iliingia mkataba na kampuni tano kwa ajili ya kujenga minara 758 ya mawasiliano vijijini ambayo kwa sehemu kubwa inakwenda kupunguza tatizo la kukosekana kwa mawasiliano, huku kata 58 zikikosa ukandarasi baada ya kuelezwa kuwa zina idadi ndogo ya wateja.

Mbali na hayo, mradi huo utanufaisha vijiji 4,708 vyenye watu milioni 8.5 katika kata 713 za wilaya 127 nchini.

Katika hotuba yake, Rais Samia alitaka watoa huduma kujali maisha ya watu, hasa wa vijijini ili wafikiwe na huduma za mawasiliano, ikiwemo kufunga teknolojia rahisi katika baadhi ya kata ambazo zilitajwa kuwa na wateja wachache, hivyo kampuni za simu kutoona umuhimu wa kuwekeza.

“Hizi kelele kwamba gharama za mawasiliano ziko juu, mwende mkalitazame, lakini minara hii inayojengwa iende ikasaidie kupunguza gharama hizo ili wananchi wanufaike na mawasiliano hayo, kwani ni sehemu ya maendeleo,” alisema Rais Samia.

Kauli ya Rais imekuja huku kukiwa na kelele kutoka kwa watumiaji wa mawasiliano, wakiwemo wabunge kulalamika gharama za kupiga simu na mabando ya intaneti ziko juu.

Aonya urasimu

Katika maagizo mengine, Rais Samia alionya kuhusu urasimu wa utoaji wa vibali vya ujenzi wa minara ambao hufanywa na halmashauri, akitaka ndani ya siku 30 vibali vitolewe ili ujenzi uanze.

Aliagiza umeme kupelekwa kwenye maeneo yote ambayo yatasimikwa minara, kwani kutasaidia kupunguza gharama za uendeshaji, ujenzi kukamilika kwa wakati na kampuni kurudisha hisani kwa wananchi baada ya faida.

“Kwa vijana, mtambue kuna uhuru wa mawazo na kujieleza, lakini tumieni vema mitandao kwa ajili ya maendeleo, kulinda utamaduni na mila za Mtanzania, hasa katika kujiendeleza kuliko kutumia mitandao kufanya mambo mengine yasiyo na tija,”alisema Rais Samia.

Kwa mujibu wa Rais, uwepo wa mawasiliano vijijini utasaidia kuongeza tija na uchumi kwa wananchi, kupunguza vifo vya mama na mtoto, kuimarisha usalama wa nchi na kupunguza pengo la usawa wa maisha kwa watu wa mijini na vijijini, kwani wote wataanza kutumia simu janja.

Aliwaagiza UCSAF na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kufanya kazi kwa karibu na kushirikiana ili wapunguze gharama, ikiwemo malalamiko kuwa upitishaji wa mkongo wa Taifa kwenye barabara unakuwa na gharama kubwa kuliko upitishaji wa vitu vingine.

Itakavyokuwa

Awali, Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba alisema jumla ya kata 713 katika wilaya 127, zinakwenda kunufaika na huduma hiyo ambapo vijiji 4,708 vyenye watu 8.5 milioni vinatarajia kufikiwa.

Mashiba alisema wanaendelea kuboresha mawasiliano nchini kwa kujenga vituo vya Tehama, hasa maeneo ya mipakani, lakini wameshaunganisha kwa wilaya zote za Zanzibar.

“Malengo mengine tunatamani kuwezesha redio jamii kila wilaya ili kusudi tuwe na maelewano na mawasiliano kila kona ya nchi bila kuleta tofauti kati ya mijini na vijijini,” alisema Mashiba.

Akizungumza na Mwananchi nje ya ukumbi wa Jakaya Kikwete ilipofanyikia shughuli hiyo, alisema hana hesabu kamili ya kiasi kitakachotumika kwenye ujenzi wa minara, lakini anatambua ruzuku ya Serikali ni Sh127.8 bilioni ambazo zimetolewa, huku wadau wakiweka fedha zao pia.

“Siwezi kuwa na jumla yote hapa, lakini kwa kweli ni fedha nyingi, ninachoweza kusema ni kwamba sisi Serikali tumetoa ruzuku ya zaidi ya Sh127.8 bilioni lakini mtambue wadau wameweka mkono wao humo,” alisema Mashiba.

Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema utekelezaji wa mikataba hiyo ni miezi 18 kuanza sasa na wanatarajia itakuwa hivyo, lakini akabainisha kuwa Watanzania 15 milioni walishafikiwa na mawasiliano.

Waziri alisema tangu kuanza kwa mpango huo, Serikali imeshatoa ruzuku ya Sh199.9 bilioni ambayo huwa ni asilimia 40 na watoa huduma hutoa asilimia 60.

Hata hivyo, alisema kata 58 hazijapata makandarasi wa kujenga minara kutokana na watoa huduma kuona kuna idadi ndogo ya wateja, hivyo hawakuomba kujenga huko.

Kwa mujibu wa Nape, gharama za kujenga mnara mmoja ni kati ya Sh300 hadi Sh350 milioni, jambo linalosababisha wachague maeneo ambayo yanakuwa na wateja wa kutosha. Alisema wamedhamiria ifikapo 2025 kila kijiji Tanzania kiwe na mawasiliano.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi