Kitaifa
Sakata Tanga na Twiga Cement lazidi kuchemka
Dar es Salaam. Siku chache baada ya Serikali kutangaza kuwa kampuni ya Chalinze Cement ilifutwa kwa mujibu wa sheria, kutokana na kutoa taarifa za uongo wakati wa usajili wake, kampuni hiyo imedai haikupewa nafasi ya kusikilizwa.
Hayo yamesemwa na wakili wa Chalinze Cement, Melchisedeck Lutema wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu kutangazwa kufutwa kwa kampuni hiyo na msimamo wao juu ya kuendelea kupinga muunganiko wa kampuni za Tanga Cement na Twiga Cement kwa kile alichoeleza unavunja sheria na kukiuka ushindani.
Kauli hiyo pia imekuja ikiwa ni siku chache tangu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Ashatu Kijaji kulieleza Bunge kuwa kampuni ya Chalinze ambayo imekuwa kinara kupinga muunganiko huo, ilifutwa kisheria baada ya kubainika kutoa maelezo ya uongo wakati wa usajili na kushindwa kujieleza ndani ya siku 30 walizopewa.
Dk Kijaji alisema notisi ya kusudio la kufutwa kwa kampuni hiyo ilitolewa Januari 19, 2023, lakini hadi siku hizo zilipomalizika, hakukuwa na maelezo yaliyopokelewa.
“Anuani ya kampuni haipo kwenye usajili popote pale ndani ya Taifa kwa hiyo anuani ni ya uongo kwahiyo huwezi kumfikia kwa sababu hujui yuko wapi anuani za wanahisa alizozisajili hazipo, kwa hiyo ni wakufikirika. Mawasiliano ya simu yaliyosajiliwa sio ya mwanahisa aliyetajwa kwenye kampuni hiyo,” alisema.
Chalinze yajibu
Hata hivyo, akizungumza jana na waandishi wa habari juu ya suala hilo, Wakili Lutema alisema uamuzi wa kufutwa kampuni ulitolewa bila wao kusikilizwa.
“Chalinze Cement imefutwa bila wao kupewa nafasi ya kujieleza wala kuambiwa imekosea nini. Kampuni hii ilisajiliwa mwaka 2021 ndiyo maana ilifutwa, kwani haiwezekani kufuta kitu ambacho hakijasajiliwa,” alisema.
Alisema kampuni hiyo ilisajiliwa awali ili mambo yatakapokaa sawa iweze kuzalisha saruji, huku akieleza kuwa kusimama kwao kupinga muunganiko wa Tanga Cement na Twiga Cement kuko kwa mujibu wa sheria.
“Sheria inasema, kama kuna mtu anaona kilichofanyika kitaumiza ushindani au kuathiri maslahi yake anaweza kukata rufaa. Sheria haitaki hadi uwe mzalishaji, umiliki kiwanda cha saruji, ghala, au mifuko,” alisema.
Kuungana kwa Twiga na Tanga
Muunganiko unaozungumziwa ulianza Oktoba 2021, wakati Scancem International DA (Scancem), ambayo ni kampuni tanzu ya Heidelberg Cement AG inayomiliki Twiga Cement na AfriSam Mauritius Investment Holdings Limited, mmiliki wa Tanga Cement, zilipotoa taarifa ya pamoja kuwa zimekamilisha masharti ambayo awali Twiga angepata asilimia 68.33 ya hisa kutoka Tanga Cement.
Awali, Tume ya Ushindani (FCC) iliidhinisha uamuzi huo, lakini ulibatilishwa na Mahakama ya Ushindani wa Haki (FCT) katika uamuzi wake wa Septemba 23, 2022, baada ya Kampuni ya Chalinze Cement Limited na Jumuiya ya Kutetea Watumiaji Tanzania (TCAS) kukata rufaa kupinga uamuzi huo.
Lutema alisema wao wamekuwa wakipinga muunganiko huo, kwa sababu unavunja sheria ambayo unataka kampuni mbili zinapoungana umiliki wake wa soko usivuke asilimia 35 lakini kampuni hizo zitashikilia soko kwa asilimia 47.
Wakati haya yakiendelea, Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa uwekezaji mpya wa zaidi ya dola za Marekani milioni 400 utakaofanywa na Twiga Cement kwa Tanga Cement utaongeza uzalishaji wa saruji nchini, kukuza ajira na mapato ya Serikali kupitia kodi mbalimbali.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Ashatu Kijaji walipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Tanga Cement. Kikao hicho cha ndani kimefanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na watendaji wa kampuni hizo na baadhi ya viongozi wa Serikali.