Connect with us

Kitaifa

Biashara Tanzania, Ufaransa yaongezeka

Dar es Salaam. Biashara kati ya Tanzania na Ufaransa imekuwa kutoka Sh27.8 bilioni mwaka 2015 hadi Sh95.5 bilioni mwaka 2022.

Ukuaji huo wa biashara umetokana na ushirikiano kati ya mataifa hayo katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii.

Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam leo, Ijumaa ya Mei 5, 2023 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax alipofungua mkutano wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya nchi hizo.

Mbali na kukua kwa biashara, amesema hata idadi ya watalii kutoka Ufaransa imeongezeka na hivyo kuifanya kuwa nchi ya pili kuleta watalii nchini.

“Kumekuwa na ongezeko la watalii kutoka Ufaransa ambapo kwa mwaka 2022 Tanzania ilipokea watalii 100,600 kutoka Ufaransa na kuwa nchi ya pili kuleta watalii nchini Tanzania.

“Biashara imeendelea kukua lakini pia katika uwekezaji tunashirikiana, katika utalii Ufaransa imekuwa nchi ya pili kwa kuleta watalii kwenye taifa letu, haya yanatokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Tax, mkutano huo unalenga kuwawezesha Wafaransa kutambua fursa mbalimbali zinazopatikana nchini, kadhalika Watanzania kuzijua za taifa hilo ili kuzitumia kwa maslahi ya pande zote.

“Tanzania na Ufaransa zimekuwa zikishirikiana katika sekta za elimu, nishati, utalii, usafirishaji, ulinzi na usalama, Ufaransa wamekuwa wadau wakubwa katika ujenzi wa bomba la mafuta linalojengwa kutoka Uganda hadi Tanzania,” amesema.

Balozi wa Ufaransa nchini, Nabil Hajlaoui amesema kufanyika kwa mkutano huo ni uthibitisho kuwa Tanzania na Ufaransa zimekuwa na ushirikiano mzuri na imara.

“Tumekuwa tukikutana mara kwa mara na kujadili masuala ya kikanda na kimataifa ili kuimarisha maendeleo ya miradi kati ya nchi zetu mbili katika sekta mbalimbali hususan mabadiliko ya tabianchi, uwekezaji, utalii, uchumi wa buluu, usalama wa baharini na tumefanikiwa kujadili masuala yote vizuri kwa sababu uhusiano mzuri tulio nao,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Ulaya na Mambo ya Nje ya Ufaransa, Christophe Bigot amesema taifa hilo litaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuimarisha sekta za biashara na uwekezaji katika nishati, usalama wa baharini, utalii, uchumi wa buluu, michezo na utamaduni.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Makatibu Wakuu na Naibu makatibu Wakuu kutoka Wizara mbalimbali.

Mkutano wa kwanza wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Ufaransa ulifanyika mwezi Juni 2018 nchini Ufaransa.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi