Connect with us

Kitaifa

Vipaumbele sita bajeti wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Dar es Salaam. Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Alhamisi Mei 4, 2023 imewasilisha mapendekezo yake ya bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 bungeni jijini Dodoma.

Akiwasilisha mapendekezo hayo, Waziri Dk Ashatu Kijaji ameomba kutengewa Sh119 bilioni kwa mwaka ujao wa fedha ikiwa ni ongezeko la asilimia 20 ikilinganishwa na Sh99.1 bilioni zilizotengwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Aidha, Kijazi ametaja maeneo makuu sita ambayo wizara hiyo itaenda kuyafanyia kazi mwaka ujao wa fedha maeneo hayo ni uwekezaji, biashara, maendeleo ya viwanda, mtangamano wa biashara, maendeleo ya biashara na maboresho ya mazingira ya biashara nchini.

Kuhusu suala la uwekezaji, Dk Kijaji amesema watahakikisha wanaboresha sera katika eneo hilo na kusimamia uanzishaji na uendelezaji wa miradi mikubwa nchini.

“Katika uwekezaji tutakamilisha maandalizi ya sera mpya na mkakati wake kuhusu uwekezaji na kuanza utekelezaji wake, kuratibu uanzishaji na uendelezaji wa miradi mikubwa ya uwekezaji yenye manufaa mapana kwa Taifa, kuratibu ufuatiliaji na kutathmini wa miradi ya uwekezaji na kuendelea kuratibu utatuzi wa migogoro na changamoto za uwekezaji nchini,”amesema.

Aidha, Dk Kijaji amesema wizara yake imejipanga kuratibu uanzishwaji wa maeneo maalum ya kiuchumi (Special Economic Zones), na uendelezaji wa miradi ya kitaifa ya Kielelezo (National Flagship Projects).

Miradi ya aina hii ni pamoja na Ukanda Maalumu wa Kiuchumi wa Bagamoyo na Tanga, Kukamilisha malipo ya fidia katika maeneo ya Ukanda Maalumu wa Kiuchumi wa Bagamoyo, Tanga, Manyoni, Nala na Ruvuma.

Kwa upande wa biashara Dk kijaji amesema kwa sasa vikwazo vingi vya kiuwekezaji vimetatutiliwa baina ya Tanzania na nchi nyingine ambapo kwa nchi jirani ya Kenya ni vikwazo 15 pekee vimesalia.

“Kwa Tanzania na Kenya, vimebaki vikwazo 15 ambavyo vyote vipo katika ngazi ya wataalamu kwa majadiliano ili vyote viweze kufutwa na wafanyabiashara waweze kufanya biashara bila vikwazo vyovyote,”amesema.

Aidha, Dk Kijaji amesema Wizara yake itajikita katika kuwainua wajasiriamali wadogo na wafanyabiashara ili waweze kupata elimu ya ujasiriamali kupitia mafunzo maalumu.

“Tutaongeza wigo wa huduma za SIDO kwa Wajasiriamali kupitia utoaji wa mafunzo ya biashara na ufundi pamoja na ushauri kwa kutumia Tehama. Tutaimarisha utendaji kazi wa shirika kwa kuongeza vitendea kazi hususan magari, kompyuta, vifaa vya mafunzo na samani,”amesema.

Pia, amesema wizara itaendelea kuhamasisha wananchi kuanzisha na kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali, vyama vya kuweka akiba na kukopa (SACCOS), benki za jamiii vijijini (VICOBA) na vikundi vingine vya kiuchumi.

Aidha, wizara itaratibu mpango wa uwezeshaji na uanzishaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo kwa kushirikisha taasisi za umma.

Katika bajeti hiyo ambayo Sh75.4 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwemo mishahara na Sh43.6 matumizi ya maendeleo, imetaja eneo lingine ambalo litatazamwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 kuwa ni maendeleo ya viwanda ambapo pia leseni za uchimbaji wa makaa ya mawe zitalipiwa.

“Katika eneo hili tutafanya utafiti wa kina wa kijiolojia (Geological study) na Kulipia leseni za uchimbaji katika mradi wa makaa ya mawe Muhukuru, kuendeleza kiwanda cha KMTC katika Mkoa wa Kilimanjaro na kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya msingi katika Kongani ya Viwanda – TAMCO,”amesema.

Kwa mujibu wa Dr Kijazi, wizara itaendelea kufanya utafiti katika kanda saba nchini ili kubaini fursa za uwekezaji na maeneo yenye viwanda na rasilimali zilizopo (Industrial Mapping).

Suala la mtangamano wa biashara, wizara imesema itaratibu majadiliano ya kibiashara kati ya nchi na nchi, kikanda na kimataifa.

Kusimamia na kuratibu utekelezaji wa mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika kwa Nchi za Bara la Afrika (AfCFTA), kuratibu uanzishaji wa Eneo Huru la Biashara la Utatu linalojumuisha Kanda za COMESA, EAC na SADC na kukamilisha utungaji wa Sheria ya Ahueni ya Athari za Biashara,”amesema.

Kuhusu suala la maendeleo ya biashara Dk Kijaji amesema watakagua na kutoa vibali vya bidhaa zinazotoka nje na leseni za ukaguzi wa magari yaliyotumika yanayoingia nchini

“Wizara itakagua na kutoa vibali 120,000 kwa bidhaa zitokazo nje ya nchi ambapo kati ya hizo vibali 40,000 ni kwa bidhaa zitakazokaguliwa nje ya nchi (PVoC) na vibali 80,000 ni kwa bidhaa zitakazokaguliwa nchini (Destination Inspection)

“Pia, tutafanya ukaguzi wa ubora na kutoa leseni za ukaguzi 46,000 za magari yaliyotumika yanayoingizwa nchini,”amesema.

Kwa upande wa maboresho ya mnazingira ya biashara nchini wizara imesema itaweka muundo wa ufuatiliaji na tathmini wenye ufanisi katika kukuza biashara, kuhamasisha na kuratibu majadiliano ya kisekta yanayopelekea maboresho ya mazingira ya biashara.

Vile vile, wizara itahakikisha majukumu ya mamlaka za udhibiti yanayoingiliana yanaondolewa na yanayofanana yanaunganishwa.

Mbali na maombi ya bajeti hii, Waziri ameliambia Bunge kuwa , katika bajeti mwaka wa fedha 2022/23, pesa zilizotolewa mpaka sasa ni asilimia 65 ya fedha zote zilizotengwa na serikali (Sh99.1 bilioni).

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi