Connect with us

Kitaifa

Simulizi alivyokimbia vita Sudan

Dar es Salaam. ‘Usiombee vita’ ndivyo unavyoweza kusema baada ya mwanafunzi wa chuo kikuu cha kimataifa cha Afrika (IUA) kusimulia maswaibu aliyokutana nayo kwa siku 12 tangu kuanza kwa vita nchini Sudan.

Lutfia Mbaraka Juma (27) anasema tangu aliposikia kishindo cha kwanza cha risasi zilizorushwa mita chache kutoka kilipo chuo anachosoma Aprili 15, saa 2 asubuhi, hakuwahi kulala kwa amani mpaka alipowasili nchini juzi.

Anasema chuo hicho kimezungukwa na kambi za jeshi linaloenda kinyume na Serikali, ndiko yalikoanzia mapigano.

“Nilisikia kishindo cha kwanza saa 2 asubuhi na baadaye nikasikia milipuko mikubwa, nikafungua pazia kuangalia ni nini maana risasi kulia Sudan ni kawaida, ila nilishangaa kuona moshi mkubwa umetanda na moto unawaka huku majibishano ya risasi yakiendelea,” anaanza kusimulia mwanafunzi huyo.

Anasema hali hiyo ilimlazimu kupiga simu nyumbani (Tanzania) kumfahamisha baba yake kinachoendelea, kabla hajaanza kujihami.

Lutfia, anayesoma chuoni hapo kwa kipindi cha miaka sita, kubakiza miezi minne amalize shahada yake ya ‘Microbiology’, anasema baada ya dakika chache hali ilizidi kuwa mbaya na wanafunzi wakaanza kutoka nje ya vyumba vya hostel.

Anasema walifanya hivyo baada ya uongozi wa chuo kuwataka wafanye hivyo.
“Tulishushwa wote, wakatukusanya sehemu moja, waliokuwa wamelala walitoka na nguo za kulalia. Hatukujiandaa na kitu chochote, tukakusanywa na kupelekwa kwenye bwalo la chuo. Tulikaa pale na kulala palepale, walileta chakula na maji.

“Jumapili changamoto ikawa kuoga na kubadilisha nguo, tuliwaambia lazima waturudishe vyumbani walikataa, lakini baada ya mabishano wakafanya hivyo,” anasema na kuongeza:

“Tulipelekwa kwa makundi tukachukua vitu muhimu, tulipewa dakika tano pekee, ilikuwa ngumu sana. Tuliendelea kuishi pale bwaloni na Jumatano wanajeshi walitulia kidogo, sikukuu ya Eid El Fitri asubuhi mapigano yalianza upya,” anasema.

Lutfia anasema chuo hakikutoa taarifa yoyote zaidi ya kukusanya watu wa mataifa mbalimbali na hawakusema iwapo chuo kinafungwa, hivyo baadhi ya wanafunzi walianza kuondoka, wakiwemo wanafunzi wa Djibout.

Anasema Jeshi lilitoa saa 48 wasio raia wa Sudan watoke walikokimbilia na waende chuoni hapo, lengo likiwa waondoke nchini humo kwa amani.

“Walitoa masharti na ilikuwa lazima yafuatwe, masharti hayo ni pamoja na kutopiga kelele wala kuwasha taa za gari au pikipiki, lakini raia mmoja (sio raia wa Sudan) alikanyaga bati likapiga kelele, alipigwa risasi,” anasema.

Mpango wa safari
Mwanafunzi huyo anasema walipanga wasafiri Jumamosi, lakini kulikuwa na changamoto nyingi.
“Ilikuwa tuanze safiri Jumamosi ikashindikana, baadaye wakasema Jumapili, lakini bado ilishindikana. Changamoto kubwa ilikuwa fedha, hakukuwa na fedha hata balozi, Silima Kombo Haji alishindwa kupata kwa sababu benki zote zilikuwa zimefungwa, fedha za kigeni hakuna na wenye mabasi walikuwa wanataka fedha taslimu.

“Watanzania tuliokuwepo Sudan wengi ni wanafunzi, tatizo lilikuja balozi na wafanyakazi wengine walikuwa hata kama wana fedha zilikuwa za akiba, nyingi zilikuwepo benki. Fedha za kusafiria zilikuwa nyingi, nilisikia mabasi yalikodiwa kwa Dola 100,000 kutoka eneo moja kwenda jingine,” anasema mwanafunzi huyo.

Anasema wamiliki wa mabasi waliongeza bei ya usafiri maradufu, hivyo balozi, wafanyakazi wa ubalozi, wanafunzi na wafanyabiashara waliokuwepo Sudan waliamua kuchangishana, ili fedha hizo zipatikane waondoke na magari hayo ya kukodi.

“Kwa sisi wanafunzi kama mtu alikuwa na akiba ya dola 50 anachangia, hata kama una dola 15 ziliongezwa. Rafiki yangu alinipatia dola 100 niandike kwa jina langu, fedha ambazo tulipofika Airport Dar es Salaam zilirejeshwa.

“Fedha zilipopatikana tuliondoka Khartoum saa saba mchana kwa mabasi matano yaliyofungwa bendera ya Tanzania mbele. Hali ilikuwa inatisha, tunapita barabarani risasi zinarushwa ovyo, tumesafiri wakati mapigano yanaendelea.

“Wote tulijawa na hofu na baadhi tulikata tamaa tukijiuliza hivi tutafika kweli? Tutaiona tena nchi yetu? Kila mmoja alikuwa akiwaza lake, basi zima lilikuwa kimya, kila mmoja anaswali anavyojua mpaka tunafika mji wa Ghadara saa tatu usiku,” anaeleza.

Lutfia anasema Balozi Haji aliwaombea Watanzania hao walale katika moja ya kituo cha polisi. “Tulikubaliwa, lakini tulilala nje tena chini,” anasema.
Kulipopambazuka, waliondoka kwa usafiri mwingine kuelekea mpakani mwa Ethiopia. Safari hiyo ilichukua zaidi ya saa 16 hadi kuufikia mpaka wa Al-Fashaga Triangle.

Hapo walilazimika kubadili magari na wakapanda mabasi ya kawaida, mfano wa daladala baada ya kukosa mabasi makubwa.

Anaeleza kuwa wakati wote wa safari, balozi waliyeongozana aliwahudumia wote kwa chakula sawa na familia yake iliyokuwa na watoto, wafanyakazi wa ubalozi na wao wanafunzi.

“Hakukuwa na huyu ni nani wala nini. Tulipata chakula ilipowezekana, lakini nyakati nyingi tulikula biskuti na juisi mpaka tunafika boda ya Al-Fashaga kwa kuwa fedha walizohitaji watu wa mabasi zilikuwa nyingi mara mbili ya fedha tulizolipa awali,” anasema na kueleza walipofika mpakani hapo walimkuta Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia akiwasubiri.

Anasema aliwasaidia kugonga viza. Hata hivyo waliopanda mabasi mabovu walilala mpakani.
“Ambao walikuwa hawajavuka walilala chini mchangani na tuliobahatika kuvuka upande wa pili tulilala barabarani kwenye lami ambayo ilikuwa na joto kali,” anasimulia mwanafunzi huyo.
Anasema kulipopambazuka, walipanda mabasi mengine mpaka kiwanja kidogo cha ndege ambako walizikuta ndege za Ethiopia zilizowabeba mpaka Adiss Ababa walikoikuta ndege ya Tanzania ikiwasubiri kuwarejesha nchini.

Hata hivyo, Lutfia anasema mwanafunzi mmoja alipata ulemavu wa kupooza upande wa kushoto wa mwili wake. “Nishukuru Serikali ya Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan, Balozi wetu, wafanyakazi wa ubalozi wamefanya kazi kubwa.”

Hatima yake
Lutfia anasema katika muhula wale wa 10 wa masomo alitarajia kufanya mitihani Mei mwaka huu na mitihani yake ya mwisho ilikuwa aifanye Septemba mwaka huu, lakini mpaka sasa hajui hatima yake.

“Hatujui vita vitaisha lini maana wengi wanatamani vita viishe warudi masomoni, ila naiomba Serikali itie jitihada itusaidie watuchukue na tufanye mwendelezo wa chuo maana siku zinaenda.

Mama mkubwa wa Lutfia, Mwanaisha Khamis Maulid, mkazi wa Kijichi anasema tangu waliposikia nchi hiyo imekumbwa na vita, hawakuwahi kuwa na amani mpaka walipomuona binti yao Aprili 27.

“Simu yake ya kwanza ilitushtua. Taarifa za habari ndiyo zilitushtua zaidi, tunamshkuru baba yake mdogo alisaidia kufuatilia taarifa. Hatukuwa tukilala, muda wote tulikaa kwenye makochi na akikosekana mtandaoni tunakosa kabisa amani. Mpaka aliporejea ndipo tulitulia,” anasema.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi