Kitaifa

Necta yaruhusu waliofutiwa matokeo kurudia mtihani

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza kuanza kwa mtihani wa marudio wa kidato cha nne kwa wanafunzi 337 ambao matokeo yao yalifutwa.

Wanafunzi hawa ni wale waliofanya mtihani mwaka 2022 na matokeo yao kufutwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo udanganyifu.

Aprili 11, 2023 Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitoa maelekezo kwa wanafunzi hao kuomba kurudia mtihani na baada ya ombi lao kukubaliwa mtihani huo utafanyika kuanzia Mei 2 hadi 15 mwaka huu.

Katibu Mtendaji wa Necta Dk Said Ally Mohamed amesema uamuzi wa watahiniwa hao kurudia mtihani umetokana na uchunguzi kuonyesha zaidi ya asilimia 60 ya waliofanya udanganyifu hawakupanga wao.

“Asilimia 60 ya watahiniwa waliofanya udanganyifu chanzo chake kilitokana na mipango iliyopangwa na kuratibuwa na vituo husika kwa kushirikisha wamiliki wa shule, wakuu wa shule, walimu na wasimamizi wa mitihani.

“Tayari Baraza limeshawasilisha kwa mamlaka husika taarifa kuhusu wote waliohusika kufanikisha udanganyifu huo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa,”amesema Dk Mohamed.

Katibu Mtendaji huyo ameeleza pia baraza limejiridhisha uwepo wa ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji mitihani kwa vituo vya shule ya sekondari Thaqaafa ya mkoani Mwanza na Twibhoki iliyoko Mara.

Kufuatia ukiukwaji huo Dk Mohamed ametangaza kuzifungia shule hizo kuwa vituo vya mitihani hadi pale baraza litakapojiridhisha kuwa ni vituo salama vya kufanyia mitihani ya kitaifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi