Kitaifa
Usiri watanda ajali ya Naibu Waziri Tamisemi
Dodoma. Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), Dk Festo Dugange amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa mjini Dodoma akipatiwa matibabu baada ya kupata ajali ya gari.
Licha ya jitihada za kuwatafuta Waziri wa Tamisemi, Angellah Kairuki na Naibu wake, Deo Ndejembi pamoja na Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa lakini, hakuwa aliyekuwa tayari kuzungumzia taarifa hizo.
Hata hivyo, akihutubia wananchi wa Wilaya ya Chamwino, Dodoma kwenye uzinduzi wa majengo ya Jeshi la Zimamoto Aprili 26, 2023, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaambia mbunge wao Ndejembi hakuhudhuria hafla hiyo kwa sababu alipewa jukumu la kumuuguza naibu waziri mwenzake aliyepata ajali.
“Ndugu wananchi, naleta salamu nyingi kutoka kwa mbunge wenu Ndejembi (Deo) alitamani kuwa nanyi hapa, lakini tumempa jukumu la kuangalia matibabu ya naibu waziri mwenzake alipata ajali Jana,” alisema Majaliwa bila kumtaja naibu waziri huyo aliyepata ajali.
Taarifa za uhakika ambazo Mwananchi limezipata kutoka hospitalini hapo, zinaeleza Dk Dugange ambaye ni mbunge wa Wanging’ombe, mkoani Njombe alifikishwa hospitalini akiwa mahututi na kwa sasa hali yake inaendelea vizuri.
“Ni kweli majeruhi tuliyenaye ni Dk Dugange, alifikishwa hapa akiwa kwenye hali mbaya lakini tunamshukuru Mungu kwa sasa anaendelea vema,” kilisema chanzo chetu.