Kitaifa
Wadau kuhoji muswada wa habari kwa wabunge
Dar es Salaam. Wadau wanaopigania Haki ya Kupata Habari (CoRI) wanatarajia kukutana na wabunge jijini Dodoma ili kufafanua zaidi mapendekezo ya mabadiliko ya vipengele vya sheria viliyoachwa nje kwenye muswada wa habari uliowasilishwa Februari 10.
Miongoni mwa vipengele ambavyo CoRI wanapenda viingizwe kwenye muswada wa sheria kabla ya kujadiliwa ni pamoja na sehemu ya saba inayohusu adhabu na makosa yake ambapo walipendekeza kupungua adhabu hasa kwa makosa yanayohusu kitaalamu.
Wamependekeza serikali iondoe ukomo wa chini wa adhabu kwa vifungu vyote kwa kuwa inambana hakimu au jaji kuamua vinginevyo.
Wakizungumzia suala hilo mwisho wa wiki iliyopita, wajumbe wa CoRI wamebainisha kwamba sheria nyingi kwenye mataifa yaliyoendelea zinaweka ukomo wa juu wa adhabu kwa kuwa inatoa fursa kwa jaji au hakimu kutoa adhabu kulingana na mazingira ya kesi husika.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (Misa-Tanzania), James Marenga, MISA TAN amesema wabunge ndio watunga sheria, na muswada umefikishwa kwao, hivyo ni muhimu tukakutana nao.
“Tulianza na Serikali na wakatusikiliza, wakawasilisha kile walichowasilisha bungeni. Ni wa kati sasa na sisi kukutana na wabunge kwa ufafanuzi zaidi, naamini wabunge ni waelewa na watatuelewa,” amesema Marenga ambaye ni wakili wa kujitegemea.
Mjumbe w CORI ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena, amesema wanachofanya ni jambo la kawaida pale kunapokuwa na hatua za utungwaji wa sheria.
“Ni suala la kawaida pale panapokuwepo na hatua za utungwaji wa sheria, taasisi husika ikawa inatoa ufafanuzi zaidi juu ya kile inachopigania.
“Tumeona ni fursa kwetu sasa kukutana na wabunge ili kuwaeleza nini tunapigania na kwa nini. Nafasi hii tunapaswa kuitumia vizuri na ndio maana tupo hapa Dodoma,” amesema.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile amesema ni muhimu kwa CoRI kukutana na wabunge ili kushawishi baadhi ya vipengele ‘vilivyotelekezwa’ kwenye muswada huo.
“Tutazungumza na wabunge kuhusu athari zinazoweza kuifika tasnia ya habari kutokana na baadhi ya vifungu vilivyomo kwenye sheria na marekebisho yaliyofanywa na serikali ili watusaidie kurekebisha siku wakianza kujadili bungeni,” amesema.