Kitaifa
Daraja la kuunganisha Zanzibar, Tanzania Bara mbioni kujengwa
Dodoma. Serikali imeanza mazungumzo kuhusu ujenzi wa daraja litakalounganisha Tanzania Bara na Zanzibar ili kurahisisha usafiri kwa pande zote mbili.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Ijumaa Aprili 28, 2023 na Naibu Waziri wa Ujenzi na uchukuzi, Geofrey Kasekenya ambaye amesema mazungumzo hayo yalifanyika Machi 11, 2023.
Naibu Waziri alikuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum Mwantumu (CCM), Dau Haji ambaye ameuliza Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja linalounganisha Tanzania Bara na Zanzibar.
Katika swali la msingi mbunge huyo ameomba Serikali kuharakisha mpango huo kwa kushirikiana na sekta binafsi au ikajifunze kutoka Mataifa ambayo yamefanikiwa.
Kasekenya amesema pande hizo mbili kwa pamoja walikutana na wawekezaji wa kampuni ya M/S China Overseas Engineering Group Company (COVEC) waliokuwa wameonesha nia ya kujenga daraja hilo.
Amesema yatokanayo na kikao hicho bado yanafanyiwa kazi kwa pande zote mbili Tanzania Bara na Zanzibar lakini amebainisha kuwa mpango wa ujenzi wa daraja hilo utahusisha sekta binafsi.