Kitaifa

Ripoti: Zaidi ya nusu ya Watanzania wanatumia intaneti

Dar es Salaam. Ripoti ya robo mwaka unaoishia Machi 2023 ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonyesha zaidi ya nusu ya Watanzania wanatumia huduma ya intaneti huku mtandao wa Facebook ukiongoza kwa matumizi makubwa ya bando.

Ripoti hiyo inayoonyesha mwenendo wa sekta ya mawasiliano nchini kwa kipindi cha Januari, Februari na Machi inaonyesha hadi Machi 2023 Watanzania milioni 33 walikuwa wanatumia huduma za intaneti ambayo ni sawa na asilimia 53.4 ya Watanzania wote.

Idadi hiyo ya watumiaji wa intaneti imeongezeka kwa asilimia 48 hadi Machi 2023 ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2018 iliyokuwa watu milioni 22.3.

Hata hivyo, mwenendo wa watumiaji wa intaneti nchini unazidi kuongezeka ambapo mwaka 2019 watumiaji walikuwa milioni 25.8 wakaongezeka hadi kufikia watumiaji milioni 26 mwaka 2020 na mwaka 2021 walifika milioni 29.1

Pia, takwimu zinaonyesha hadi mwaka 2022 watumiaji wa intaneti walikuwa milioni 31.2 ambayo ni sawa na asilimia 50.6 ya watu wote nchini kwa kipindi hicho.

Taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), iliyoishia Oktoba mwaka jana ilionyesha kulikuwa na simu janja milioni 17, sawa na asilimia 27 tu ya idadi ya watu milioni 61.7, hii inamaanisha watumiaji wengi wa intaneti takribani milioni 16 hawatumii simu janja kwa ajili ya intaneti.

Kwa upande wake profesa Abel Kinyondo wa Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amesema matumizi ya intaneti kwa jamii yana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.

“Unaangalia kwa upana wake kwa mfano kwenye matangazo watu binafsi wamepunguza bajeti za matangazo kwa njia zilizozoeleka na badala yake wanatumia mitandao ya kijamii, Tehama ina unafuu na mchango mkubwa kwenye uchumi,”amesema.

Naye, Christopher Boniface, mtalaamu wa Tehama kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) amesema Serikali inalazimika kuimarisha miundombinu ili kuchochea mchango wa sekta ya kidijitali katika uchumi.

“Kwa sasa Tehama ndio inaongoza uchumi wa dunia. Uchumi huu ndio unalazimisha dunia kuhamia dijitali, vikao, tangazo la kazi, taarifa za fursa vyote vinafanyika WhatsApp sasa hivi, kiuchumi imeokoa gharama,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi