Kitaifa
Watano wajeruhiwa ajali ya basi Mbalali
Mbeya. Watu watano wamejeruhiwa na kukimbizwa katika Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya (MZRH) kwa matibabu baada ya basi la Kampuni ya Abood kupata ajali katika Kijiji cha Mswisi Wilayani Mbarali Mkoa hapa.
Kwa Mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Denis Mwila amesema leo Jumapili Aprili 23, 2023 kuwa ajali hiyo imetokea majira ya saa moja asubuhi katika barabara kuu ya Tanzania na Zambia (Tanzam) .
Amesema kuwa taarifa za awali zinaeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi hilo ambaye amekimbia baada ya ajali kutokea, kutaka kulipita gari lingine lililokuwa mbele yake na kusababisha ajali hiyo.
“Tunashukuru Mungu hakuna kifo hata kimoja zaidi ya watu watano kupata majeraha wakiwepo wanawake wawili na wanaume watatu ambao wamekimbizwa kupatiwa matibabu katika Hosptali ya Rufaa ya Kanda (MZRH),” amesema Mwila.
Aidha Kanali Mwila ameonya vitendo vya madereva wa mabasi ya mikoani kutotii sheria za usalama barabarani na kwamba Jeshi la Polisi lifanye jitihada kumpata dereva wa basi hilo ambaye amekimbia.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya Simu mkazi wa Inyala, Zamda Mickdadi ameomba Jeshi la polisi kuweka utaratibu wa kusindikiza mabasi ya mikoani kutokana na tabia ya kukiuka sheria za usalama barabara kwa kuendesha mwendo kasi .
“Sisi wananchi tunaona mambo mengi barabarani kimsingi mabasi ya masafa marefu ni shida na hata kwenye vivuko vya watembea miguu hawasimami hususani muda ambao askari wa usalama barabarani hawapo,” amesema.