Kitaifa
Watoto watatu kati ya 10 wapo hatarini kupata kisukari
Dar es Salaam. Kutokana na mtindo wa maisha na malezi kubadilika nchini na duniani kwa ujumla, watoto wenye umri kati ya miezi sita hadi miezi 23 wapo hatarini kupata ugonjwa wa kisukari, ripoti ya Utafiti wa Afya, Viashiria na Malaria imesema.
Ripoti hiyo ya mwaka 2022 iliofanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeonesha kundi hilo lipo hatarini kwa sasa kupata kisukari na kuongeza uzito uliopitiliza.
“Asilimia 30 ya watoto wenye umri wa miezi sita hadi 23 wanalishwa vinywaji vyenye sukari huku asilimia tisa ya watoto wenye umri huo wanalishwa vyakula visivyo na virutubisho muhimu,” imesema ripoti hiyo.
Takwimu hizo ni sawa na watoto watatu kati ya 10 wapo hatarini kupata magonjwa ya kisukari na moyo kutokana na aina ya vinywaji wanavyotumia katika umri huo.
Mwajuma mohammed mkazi wa mabibo jijini Dar es Salaam amesema tabia ya kuwalisha watoto wadogo vyakula hivyo vinasababishwa na kuiga utamaduni wa kigeni.
“Tunaiga vitu vingi kwenye utamaduni wa wenzetu, yani kila tunachokiona kwenye mitandao ya kijamii na sisi tunataka kukifanya hivyo kitu ambacho sio sahihi na kinahatarisha afya za watoto wetu,”amesema.
Mwajuma amesema, tabia ya kunyonyesha watoto inapotea kwa wanawake wengi kwasababu wanaogopa kuharibu mwonekano wao.
Kwa upande wake Daktari Zainabu Hussein kutoka Kituo cha Afya cha Shirika la Reli (TRC) Dodoma amesema mtoto katika umri huo ana uwezekano wa kupata kisukari endapo akitumia vinywaji vyenye sukari kupita kiasi.
“Katika umri huo (miezi sita hadi 23), mtoto anatakiwa kunywa juisi ya matunda, maziwa na vyakula laini kama mtori,”amesema.
Hata hivyo, ripoti hiyo pia imeonyesha watoto wadogo chini ya umri wa miezi sita wanaonyonyeshwa baada ya kuzaliwa wameongezeka kutoka asilimia 32 mwaka 1999 hadi asilimia 64 mwaka 2022.
Ripoti hiyo ya mwaka 2022 ilizinduliwa jijini Dodoma Januari 2023 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ikiwa ni ya saba tangu ianze kutolewa ambapo ripoti ya kwanza ilitolewa mwaka 1999 ikionyesha hali ya Afya, Malaria na Ukimwi nchini.