Kitaifa
Ufaransa, Kenya vinara kuleta watalii Tanzania
Dar es Salaam. Nchi za Ufaransa, Italia na Marekani zimekuwa vinara wa kuleta wageni wengi wa kimataifa nchini katika kipindi cha Januari hadi Februari 2023 kutoka nje ya Afrika.
Huku kwa nchi za ndani ya Afrika, Kenya na Burundi zikiongoza. Hata hivyo katika kipindi hicho watalii wa kimataifa wameongezeka kwa asilimia 49 mwaka huu ikilinganishwa na mwaka 2022.
“Wageni wa kimataifa wamefika 290,896 mwaka huu katika kipindi cha Januari na Februari kutoka wageni 195,483 mwaka 2022 katika kipindi kama hicho,”
Katika ripoti iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha kwa nchi Ufaransa iliongoza kuleta watalii 25,837 ikifuatiwa na Italia iliyoleta watalii 18,556 na Marekani walikuwa 16,567.
Nchi nyingine ni Ujerumani (15,705), Poland (12,369) na Uingereza (10,657). Kwa upande wa nchi za Afrika, Kenya inaongoza kwa kuleta watalii 29,615 ikifuatiwa na Burundi (16,832), Rwanda (7,627) na Malawi (6,563).
Nchi nyingine ni Uganda (6,511) na Afrika Kusini ilileta watalii 5,196.
Wanakuja kufanya nini
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa wageni wengi walikuja nchini kwa ajili ya mapumziko na sikukuu na kutembelea ndugu na marafiki.
“Waliokuja kutalii na kupumzika walikuwa 263,934 sawa na asilimia 90.7, kwa ajili ya kutembelea ndugu na marafiki walikuwa 16,307 sawa na asilimia 5.6 na waliokuwa wanapita kwenda nchi nyingine walikuwa 6,035 (asilimia 2.1),” imesema ripoti hiyo.
Pia, taarifa hiyo inasema waliokuja kwa ajili ya biashara walikuwa 3,418 sawa na asilimia 1.2.
Aidha, katika wageni hao wa kimataifa asilimia 39.2 waliingia nchini kupitia Zanzibar, ambapo ni sawa na wageni wawili kati ya watano wa kimataifa walipitia Zanzibar.
Ongezeko hilo la wageni wa kimataifa linakuja kipindi ambacho Tanzania inafanya jitihada mbalimbali za kuongeza watalii hadi kufikia milioni tano mwaka 2025.