Kitaifa

Ripoti: Wanawake wengi walioolewa hawataki kuongeza watoto

Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umebaini kuwa wanawake wengi walioolewa hawatamani kupata mtoto mwingine katika kipindi cha karibuni.

 Utafiti huo unaoitwa ‘Utafiti wa Afya, Viashiria na Malaria’ wa mwaka 2022 ulihusisha wanawake 9,252 walioolewa na wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 ambapo ulibaini wanawake wanne kati ya watano hawapo tayari kupata mtoto mwingine karibuni.

Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha asilimia 24.1 ya wanawake walioolewa ndio wapo tayari kupata mtoto mwingine katika kipindi cha miaka miwili huku asilimia 35.2 hawapo tayari kwa sasa labda miaka miwili zaidi.

  • Adaiwa kumuua mwanafunzi mwenzake chuoni akimdai fedha

  • Watoto 1600 wafelishwa kukwepa gharama Muheza

“Asilimia 19.4 ya wanawake walioolewa hawataki kabisa kupata mtoto mwingine, asilimia 13 hawajaamua bado kuongeza mtoto huku asilimia 3.1 wamefunga kizazi hivyo hawawezi kupata mtoto,”inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Pia, ripoti hiyo imesema asilimia 2.2 ya wanawake hao wanahitaji mtoto mwingine ila hawajaamua bado lini wapate na asilimia tatu ni wagumba.

Mariamu Salim mkazi wa Makumbusho amesema wanawake wengi hawataki kuongeza watoto kwasababu ya umaskini na kushindwa kuzimudu ndoa.

 

“Wanawake wengi ndoa zinatushinda na unakuta watoto ulionao unahangaika nao kuwatimizia mahitaji yao kwa sababu mara nyingi wanaume wa siku hizi hasa wa mjini hawajali familia,”amesema.

Christina Joseph mkazi wa Mbezi Makonde amesema kitendo hicho kinasababishwa na kupungua kwa uaminifu ndani ya ndoa nyingi.

“Uaminifu ndani ya ndoa nyingi umepungua na watu wengi wanatamani kutoka ndani ya ndoa, hivyo mwanamke anakuwa hana mapenzi tena na mume wake.

“Pia wapo ambao wanaogopa kupitia maumivu katika mchakato wa kuzaa kwa hiyo anakuwa na uoga.

Kwa upande wake, Geoffrey Nsokya ambaye ni mwanasaikolojia amesema wanawake wengi hawana hisia za upendo kama ilivyo zamani kutokana na mtindo mpya wa maisha.

“Kwa sasa wanawake wengi ni watafutaji, mtindo wa maisha umebadilika hawasubiri tena kuletewa, hivyo kuwa na mimba kwake ni kama kunampotezea muda wa kufanya shughuli zake za kiuchumi,”amesema.

Licha ya utafiti huo kuonyesha utayari wa wanawake kupata watoto kuwa mdogo lakini pia uwezo wa wanawake kupata watoto nchini umepungua kutoka watoto sita mwaka 1999 hadi watoto tano mwaka 2022 kwa mwanamke mmoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi