Kitaifa
Faida za pete, sindano katika kinga ya VVU
Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wameishauri Serikali kuzikubali mbinu mpya za kukinga maambukizi ya Virusi vya Ukimwi zilizogundulika, zikiwemo sindano za PreP na pete ili kulifikia kundi kubwa la walengwa lililo hatarini.
Hatua hiyo, inadaiwa itaongeza fursa kwa Watanzania kuchagua njia rahisi kwao kati ya kutumia condomu, dawa kinga ya PreP (kidonge) au kuchoma sindano kila baada ya miezi miwili.
Pete inayovaliwa ukeni, imetajwa kuwa njia itakayosaidia kundi kubwa la wanawake wakiwemo wasichana ambao wanashindwa kufanya maamuzi pindi wanaume wanaokuwa nao katika mahusiano wanapokataa kutumia kondomu.
Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Tumaini Nagu alipoulizwa kuhusu njia hizo alisema, “kwa sasa bado, lakini wizara huwa tuna utaratibu wa kufanya mapitio ya miongozo, kwa sasa tupo kwenye mchakato wa kufanya uchambuzi wa miongozo ya kukinga maambukizi ya virusi vya Ukimwi.”
Wakizungumza katika mafunzo kwa vyombo vya habari yaliyolenga kutoa elimu kuhusu njia za kujikinga na maambukizi, wataalamu hao walisema njia hizo mpya zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizi. “Tanzania inahitaji kupata hizi mbinu mpya za kujikinga na maambukizi ya VVU, kwanza tutaongeza nafasi ya watu kuchagua njia sahihi, na itawawezesha wanawake na wasichana kujikinga pasipo wenzao wao kujua,” alisema Catherine Madebe, Meneja programu Mulika Tanzania.
Alisema mbinu hizo zinaongeza nafasi zaidi kwa wale ambao mbinu za awali ziliwapatia changamoto. “Hatusemi njia za awali, kama kondomu na zingine, zilikuwa hazifai, bali tunapokuwa na njia nyingi inasaidia watu kuchagua na kuona ni ipi itawafaa zaidi,” alisema Madebe.
Pete
Wataalamu wamesema matumizi ya pete ya kuzuia VVU (Dapivirine Vaginal Ring) kutashusha maambukizi kwa wanawake.
Pete hiyo ya silikoni inayovaliwa ukeni na kudumu kwa siku 28 hutoa dawa kinga ya dapivirine ambayo ni aina ya ARV inayoua VVU ukeni.
Pete hiyo inadaiwa ni rahisi kuivaa, inakinga virusi kwa asilimia kubwa na si rahisi mwenza kubaini iwapo mwanamke ameivaa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Dare, Dk Lilian Mwakyosi, alisema pete hiyo itakuwa mkombozi kwa wanawake na wasichana walio katika hatari ya kuambukizwa VVU.
“Hii ni njia mpya ya kuzuia maambukizi ya VVU tofauti na njia nyingi ambazo tumekuwa nazo kwa muda mrefu.
Kuhusu Sindano, Francis Luwole kutoka Compass Tanzania alisema pia ni njia mpya inayochukua wiki nane kabla ya muathirika kuhitaji dozi nyingine, pia ni rahisi kutumika badala ya tembe anazopaswa kumeza mtu kila siku.
“Sindano hiyo tayari imeshapendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) itumike baada ya kuihakiki na kutoa mwongozo Julai mwaka jana.