Kitaifa
Rais Samia aahirisha tena sherehe za muungano
Unguja. Wakati maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yakisubiriwa hapo Aprili 26 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan ameahirisha sherehe za gwaride na badala ameelekeza kufanyika kwa shughuli za maendeleo katika ngazi za mikoa.
Hii ni mara ya pili tangu Rais Samia aingie madarakani kufuta sherehe hizo na kuelelekeza zifanyike shughuli za kijamii ikiwemo usafi wa mazingira.
Taarifa ya kufutwa kwa sherehe hizo ilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akizindua ripoti ya pili ya machapisho ya sensa ya mgawanyo wa idadi ya watu kwa maeneo ya kiutawala na umri, katika ukumbi wa Dk Mohammed Shein, Mkoa wa Kusini Unguja.
Hata hivyo, Majaliwa hakutaja kiasi cha fedha kilichokuwa kimetengwa kwa ajili ya maadhimisho hayo wala mahali kitakakoelekezwa.
“Maelekezo ya Rais ya maadhimisho ya sherehe hizo za Muungano mwaka huu, zitafanyika katika ngazi ya mikoa kwa kufanya shughuli za kijamii, kiuchumi na kaulimbiu itakuwa, “Umoja na mshikamano ndiyo nguzo ya kukuza uchumi wetu.”
Alisema maadhimisho hayo yataanza kufanyika Aprili 17, hadi siku ya kilele Aprili 26 mwaka huu.
Waziri Mkuu alisema katika kipindi hicho, taasisi na mikoa ziendelee na uzinduzi wa miradi ya maendeleo sambamba na shughuli za kijamii, hasa upandaji wa miti, uchangiaji wa damu hospitali na vituo vya afya, usafi wa mazingira na mashindano ya michezo na uandishi wa insha kwa shule za msingi na sekondari nchini.
Pia, katika kipindi hicho, ifanyike kampeni ya kupiga vita unyanyasaji na ukatili wa kijinsia na kampeni ya kupambana na wanaotaka kumomonyoa maadili ya taifa.
Kwa sasa viongozi wa dini wamekuwa wakitumia nyumba za ibada kukemea vitendo vya utovu wa maadili na udhalilishaji hasa watoto. Pia, wabunge wamekuwa mstari wa mbele kuonya na kukemea vitendo hivyo, wakiitaka Serikali kuwa makini na kuchukua hatua.
“Tuendelee kufanya majadiliano maalumu na wazee maarufu na vijana kujua muugano wetu, pia iwepo mijadala na makongamano,” alisema Majaliwa.
Pia, alisema sherehe hizo zitafanywa vizuri kitaifa muungano utakapokamilisha miaka 60. Alitoa rai kwa wahusika wa pande zote mbili kuhakikisha wanasimamia maagizo hayo ya Rais.
Sensa ya watu
Awali, akizindua ripoti ya pili ya sensa ya mgawanyo wa idadi ya watu kwa maeneo ya kiutawala na kwa umri, Waziri Mkuu alitaja maeneo saba yaliyoimarika ikilinganishwa na sensa ya mwaka 2012.
Alisema matokeo kuhusu uwiano wa watu wanaohamia mijini, ripoti imebainisha kiwango cha watu wanaoishi mjini kimeongezeka kutoka asilimia 30, mwaka 2012 hadi asilimia 35 mwaka 2022. Hata hivyo, kasi ya uhamiaji wa watu mijini imepungua ikilinganishwa na mwaka 2002 hadi mwaka 2012.
Alisema kwa kipindi hicho, kasi ya watu kutoka vijijini kwenda mjini ilikuwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 4.8 kwa mwaka 2012 hadi mwaka 2022, huku Zanzibar ikiongezeka kwa asilimia 4.3.
Matokeo yanaonyesha idadi ya watu wanaoishi vijijini kwa Zanzibar ni karibu nusu ya watu wote waliohesabiwa Tanzania na Zanzibar mwaka 2022 ambao ni asilimia 49.
“Matokeo hayo ni kutokana na jitihada za Serikali kuboresha maisha ya wananchi vijijini kwa kutoa huduma za kijamii,” alisema Majaliwa.
Alisema kitendo hicho kinapunguza kasi ya wananchi wanaohamia mijini na badala yake wanaendelea kubaki vijijini kwa sababu huduma za kijamii zinapatikana huko.
Idadi ya watoto
Majaliwa alisema idadi ya watoto chini ya miaka 18, inaendelea kupungua kutoka asilimia 50.1 mwaka 2012 hadi asilimia 49 mwaka 2022 kwa upande wa Tanzania bara.
Alisema kwa Zanzibar, idadi inaendelea kupungua kutoka asilimia 49 hadi 47, licha ya kuwa muundo wa idadi ya watu kwa umri na jinsi ina watoto wengi zaidi wenye umri chini ya miaka 18 na wazee wachache wenye umri wa miaka 65.
Majaliwa alisema takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania wote wapo kwenye umri wa miaka 15 hadi 54. Alisema hiyo ni ishara nzuri kwa kuwa wingi wa watu wenye umri huo una uhusiano na kupungua kwa uwiano wa umri tegemezi.
Mawasiliano
Majaliwa alisema takwimu zinaonyesha asilimia 97.5 ya vitongoji, mitaa na shehia zimefikiwa na mitandao ya simu, kiwango hicho kinafanana na Tanzania bara wakati huo; kwa Zanzibar imefanya vizuri zaidi kwa kufikia asilimia 99 ya shehia ambazo zimefikiwa na mitandao ya simu.
Pia, zinaonyesha maendeleo katika kujenga mazingira wezeshi ya kutekeleza uchumi wa kidijitali, huku akiwataka wananchi watumie fursa hiyo ya mawasiliano inayoendelea kuboreshwa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kamisaa wa Sensa, Anne Makinda alisema wakati umefika kufanya kazi kitakwimu badala ya kuiachia Serikali pekee, huku akitaka takwimu hizo zitumike kwa watu kutafuta fursa badala ya kusubiri kutafutiwa.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Salum Kassim Ali alisema matokeo hayo ni muhimu kwa sababu yanasaidia Serikali katika utungaji sera na kupanga mipango yake ya maendeleo.