Kitaifa
Ndani ya Habari: CAG na waliojikopesha Sh41 bilioni NHIF
Dar es Salaam. Wakati ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere ikibainisha wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) walijikopesha Sh41.42 bilioni na kusuasua kuzilipa, menejimenti ya uongozi wa mfuko huo umetoa ufafanuzi.
Katika ripoti hiyo ya mwaka 2021/22, CAG Kichere anasema kuna kupungua kwa ukwasi wa mfuko huo unaochangiwa na mambo mengi, kutorejeshwa kwa mikopo ya watumishi wa NHIF.
“Nilibaini kuwa hadi Juni 30, 2022, NHIF ilikuwa na mikopo ya wafanyakazi ambayo haijalipwa Sh41.42 bilioni, kati yake Sh11.18 bilioni ikiwa mikopo mipya iliyotolewa 2021/22.”
CAG anasema mikopo hiyo ilitolewa bila kuzingatia mahitaji ya aya 1.4 ya sera ya mikopo ya wafanyakazi wa mfuko ambayo inahitaji mikopo kutolewa chini ya mfumo wa kukopa na kulipa,” anasema CAG.
Aliongeza: “Nilibaini kupungua kwa ukwasi wa fedha za mfuko huo, hata hivyo mfuko uliongeza ukomo wa mkopo kwa wafanyakazi, hii inatokana na mfumo usioridhisha wa usimamizi wa mfuko wa mkopo kwa wafanyakazi”.
Akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano NHIF, Angela Mziray alisema “mikopo inayotolewa kwa wafanyakazi wa mfuko ipo kisera kama ilivyo kwa taasisi nyingine za umma na binafsi kwa ajili ya motisha na inarejeshwa kila mwezi na watumishi kupitia mishahara yao pamoja na riba, pia ina bima ili kuhakikisha hakuna hasara,” alifafanua Mziray.
Hata hivyo, katika mapendekezo yake, CAG anasema NHIF itekeleze sera ya mikopo na kuanzisha mfuko wa kukopa na kulipa ili kuepuka kuathiri ukwasi wa mfuko.
Malipo hewa
Si mikopo tu, ripoti hiyo ya CAG imeonyesha NHIF ilivilipa vituo vya afya madai yasiyo ya kweli yanayofikia Sh14.46 bilioni kwa kipindi cha mwaka 2019/20 hadi 2021/22.
Mbali na hili, CAG amebaini watumishi 146 wakiwemo 129 wa vituo vya afya na wa mfuko huo walijihusisha na vitendo vya udanganyifu.
“Watumishi 146 wa NHIF na wa vituo vya afya walijihusisha na vitendo vya udanganyifu, lakini Kitengo cha Kupambana na Udanganyifu kiliripoti maofisa 17 tu wa mfuko waliojihusisha na vitendo vya udanganyifu kwa kamati za nidhamu,” anasema CAG.
Kuhusu suala hilo, Mziray alisema; “hapa 129 ni watumishi wa vituo vya matibabu, hawa NHIF tuliwaripoti kwenye mabaraza ya kitaaluma na watumishi wa NHIF 17 wameripotiwa kwenye kamati za nidhamu za Mfuko na Jumla ni 146.”
Vilevile, CAG anasema ripoti za kupambana na udanganyifu kati ya 2019/20 na 2021/22 zilibaini kuwepo na madai yasiyo ya kweli na yasiyo sahihi ambayo NHIF ilivilipa vituo vya afya.
“Kati ya Sh1.71 trilioni ambazo zililipwa kwa vituo vya kutolea huduma za afya kwa miaka mitatu ya fedha kuanzia 2019/20 hadi 2021/22, Sh14.46 bilioni zililipwa kwa madai ya uongo na yasiyo sahihi.
“Uchambuzi zaidi ulifanyika ili kupata malipo ya madai yasiyo ya kweli, katika vituo vya afya vya binafsi, Serikali na vile vya mashirika ya dini na kubaini vituo binafsi vya huduma ya afya vilikuwa na kiasi kikubwa cha madai yaliyolipwa yasiyo ya kweli ikilinganishwa na vya Serikali.
“Zaidi ya Sh10.38 bilioni zililipwa kwa vituo binafsi na madai katika vituo vya mashirika ya dini ilikuwa ni Sh2.49 bilioni na vituo vya Serikali ilikuwa Sh1.57 bilioni,” alisema CAG.
CAG alisema kumekuwa na ongezeko la madai yasiyo ya kweli na yasiyo sahihi kutoka Sh4.32 bilioni mwaka wa fedha 2019/20 hadi Sh4.55 bilioni kwa mwaka wa fedha 2020/21 na Sh5.59 bilioni katika mwaka wa fedha 2021/22.
Kufuatia hilo, Mziray alisema, “hiyo ya Sh14.46 bilioni ni madai yaliyowasilishwa na vituo vya huduma za matibabu yasiyo ya kweli, ambayo yamepatikana kwenye ripoti za udanganyifu baada ya mfuko kufanya uchunguzi. Na sababu za madai haya zimetajwa hapo kwenye ripoti.”
Hasara
Kwa upande mwingine, CAG alibaini mfuko huo ulipata hasara ya Sh205 bilioni kwa mwaka wa fedha 2021/2022, ikilinganishwa na hasara ya kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21 ambapo ni Sh104 bilioni.
Akifafanua hilo, Mziray alisema fedha hizo si hasara, bali nakisi iliyotokana na mfuko kuelemewa kwa kuhudumia wagonjwa wengi ikilinganishwa na kiasi kinachokusanywa.
“Nakisi ya Sh205 bilioni inatokana na kwamba mfuko unalipa fedha nyingi zaidi za huduma wanazopata wanachama wake kwenye vituo, kuliko michango wanachama wanayochangia.”
Alisema kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza ambayo awali hayakuwepo nchini ambayo gharama yake ni kubwa kuyatibia ni mojawapo ya NHIF kupata nakisi hiyo.
Katika ripoti hiyo, CAG alisema katika mfuko huo kumekuwa na mtiririko hasi wa fedha katika shughuli zake za uendeshaji ambapo michango inaongezeka kwa asilimia 12.9 wakati matumizi yanaongezeka kwa asilimia 24.6.
CAG anasema taarifa ya tathmini ya mfuko kujiendesha inaonyesha mapato ya matumizi yataendelea kuwa chini na mfuko utatumia ziada iliyokusanywa na hivyo kusababisha ukwasi kuwa hasi ifikapo mwaka 2025.
CAG anapendekeza kuangaliwa upya namna ya kuuboresha mfuko, kuongeza wanachama wa hiari na kuboresha kanzidata ya Tehama na kuboresha usimamizi wa watoa huduma za afya.
Akizungumzia matokeo ya ukaguzo huo, Mwenyekiti wa Chama cha watoa huduma za afya binafsi Tanzania (Aphta), Dk Egina Makwabe alisema vituo binafsi vinaonekana kutumia fedha nyingi katika udanganyifu kwa kuwa hata malipo, kwa asilimia kubwa yanakwenda huko.
Dk Makwabe alifafanua kuwa madai ya udanganyifu kwa mfuko yapo chini ya asilimia 2 ambayo ni ndogo, kwani kwa viwango vya dunia ni asilimia 5.
Hata hivyo alisisitiza hatua za Serikali kuelekea Bima ya Afya kwa Wote ni suluhisho kwa sababu wengi wakichangia si wote wataugua kwa wakati mmoja, hivyo huduma zitaongezeka na wengi watanufaika.