Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Athuman Ngenya ikiwa ni siku 10 tangu shirika hilo lianze kufanya uchunguzi kuhusu poda hizo.
Aprili 4 mwaka huu, wazalishaji wa poda hizo walieleza dhamira yao ya kusitisha uzalishaji wake baada ya kushindwa kesi zilizofunguliwa na wateja wake 60,000 na kukubali kulipa fidia ya dola 8.9 bilioni baada ya kubaini kuwa kemikali ya talc inayotumika ilisababisha saratani kwa watumiaji.
Dk Ngenya aliwataka Watanzania kusitisha mara moja matumizi ya poda hizo mpaka pale TBS itakapotoa majibu kutoka maabara.
“Tumepeleka kwenye maabara ambayo haifanyi kazi kwa muda mfupi, kuna taratibu zake za kufanya uchunguzi, kwa hiyo tunategemea majibu tutapata kesho, sijajua ni muda gani lakini ndiyo yatatoka kwa namna ambavyo wanalishughulikia, Jumatatu tutawapa jibu kamili kama tuendelee nazo au tuziache kabisa,” alisema.
Dk Ngenya aliwatahadharisha Watanzania kwamba ni busara kuacha matumizi ya bidhaa hizo kwa sasa.
“Kama unatumia kwa mtoto wako kwa sasa weka pembeni kwa sababu ni kitu ambacho kina mashaka kwanini uendelee kukitumia? Wacha kikae dukani lakini usinunue siyo kikikaa dukani basi lazima ununue, hatujafikia hatua ya kuwaambia watu wa maduka waiondoe lakini tayari ni kitu ambacho kina hatihati,” alisema.
Baadhi ya maduka katika jiji la Dar es Salaam, yameonekana yakiendelea kuuza bidhaa hizo huku wauzaji wakieleza wazi kusikia taarifa hizo..
Mjadala bado umeendelea kuwa mkali kwa watumiaji wa bidhaa hizo, huku wengi wao kutoka maeneo ya jiji hilo wakisema wamekuwa wakitumia mafuta ya maji kwa ajili ya kuwakinga watoto wao na joto.
“Poda ilitumika zaidi zamani, miaka ya hivi karibuni matumizi yanapungua lakini bado asilimia kubwa ya kinamama wanazitumia,” alisema Neema John mkazi wa Ilala.