Kitaifa
Serikali mbioni kuunganisha kitambulisho kimoja
Dodoma. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeanza kufanya mawasiliano na Taasisi nyingine zenye vitambulisho ili kuona uwezekano wa kuainisha taarifa zilizomo katika vitambulisho tofauti kwa lengo la kuwa na kitambulisho kimoja.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Ijumaa Aprili 14, 2023 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini ambaye amesema mpango huo utawezesha kupunguza utitiri wa vitambulisho vingi kwa wakati mmoja kwa mtu mmoja.
Sagini ameeleza hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mwanakwerekwe, Hassan Haji Kassim ambaye amehoji ni lini Serikali itaweka utaratibu wa kuwa na kitambulisho kimoja chenye taarifa zote za huduma ndani ya kadi moja.
Naibu Waziri amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), inatengeneza vitambulisho vya Taifa kwa kutumia teknolojia ya ‘Smart Card’ ambapo kitambulisho kinakuwa na ‘chip’ inayokiwezesha kutumika kwa matumizi mbalimbali.
“Kitambulisho hiki kinaweza kutumika kama Pochi ya Fedha ya Kielektroniki (E-Wallet), ATM Card kwa ajili ya kutoa fedha kutoka mashine ya ATM, huduma za Bima ya Afya, Kitambulisho cha Mpiga Kura na mengineyo,” amesema Sagini.
Kiongozi huyo amesema baada ya mwafaka utakapofikiwa, wananchi watajulishwa rasmi lini utaratibu huo utaanza kutekelezwa.