Kitaifa

Polisi kufyeka mtandao wa wafukua makaburi

Dodoma. Katika hali isyo ya kawaida watu wasiojulikana wamevunja kaburi la Aureus Kayombo (65), aliyezikwa kitongoji cha Kipondoda, Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida na kuchukua vitu alivyozikwa navyo marehemu, vikiwemo nguo na pete.

Matukio kama hayo yanaelezwa kutokea wilayani humo tangu mwaka 2019, ambapo Septemba 2021, mwili wa Julia Amasi (93), ulifukuliwa na kukutwa jeneza likiwa tupu, huku mwili ukiwa pembezoni mwa makaburi hayo.

Januari 2022, watu wasiojulikana walifukua kaburi la mtoto, Christian Santone na kuchukua mwili wake, kabla ya mwili huo kupatikana siku tatu baadaye ukielea kwenye kisima cha maji jirani na kitongoji hicho.

Akizungumza na Mwananchi, mdogo wa marehemu, Richard Kayombo alisema kaka yake alifariki dunia Machi 20 mwaka huu jijini Dar es Salaam na kwenda kuzikwa kwenye kijiji hicho Machi 25.

Alisema baada ya siku 14 huwa wana tabia ya kwenda kutembelea makaburi, hivyo ilipofika Aprili 4 walikwenda kutembelea kaburi la kaka yao na kukuta kaburi limechimbwa pembeni baada ya kushindwa kuvunja zege.

“Walioingia kaburini kupitia uwazi ulioachwa na wahalifu hao ni watu wanne wakiwa ndugu, daktari na polisi, walibaini marehemu alivuliwa nguo zote na vitu vyote alivyozikwa navyo ikiwemo pete na cheni,” alisema.

Alifafanua: “Tofauti na wanapofukua makaburi mengine huchukua viungo, kwa kaka hawakuchukua kiungo chochote”.

Alisema baadhi ya watu wanasema wahalifu wanaweza kuchukua nywele, lakini walioingia ndani ya kaburi wasingeweza kujua kama wamezichukua au la, kwa sababu mwili ulikuwa umeharibika sana.

Kayombo alisema kwa sababu wahalifu hao, hawakutoa mwili nje ya kaburi, walichofanya baada ya ukaguzi ni kuongeza uimara wa kaburi kwa kujengea tena tofali nyingine, “Ni kama tumejenga ukuta mwingine.”

Naye Mwenyekiti wa Kipondoda, Jackson Job alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. “Kwa sababu kaburi lilikuwa chini na maaskari walikwenda huko na sisi tulibaki juu, hivyo sifahamu wamechukua nini na nini. Tunasubiri hatua zitakazochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama,” alisema Job.

Akizungumzia tukio hilo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alisema uchunguzi wa polisi unaonyesha vilivyochukuliwa ni nguo, cheni, saa, pete na viatu vya marehemu.

Alisema uchunguzi wa polisi umebaini kuwa matukio ya ufukuaji makaburi yanasababishwa na mila potofu za kishirikina ambazo ni aibu na uhalifu.

“Tangu matukio hayo yaanze wilayani humo, tumeshakamata watu saba waliofanya mauaji na kufukua makaburi kwa lengo la kupata viungo na mali za marehemu. Mtandao huu upo mkoani Singida, lakini Jeshi la Polisi tumejipanga muda si mrefu tutamalizana nao na kuwafikisha mahakamani wahusika,” alisema Misime.

Historia fupi

Marehemu Aureus Kayombo, maarufu Chamah, wakati wa uhai wake alijulikana zaidi katika shughuli za ufundi magari, uchezaji na kufundisha mpira wa miguu. Ameacha mke, watoto watatu na mjukuu mmoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi