Kitaifa
Mbunge ataka ripoti ya CAG ijadiliwe kabla ya kupitisha bajeti
Dodoma. Mbunge wa Ndanda (CCM), Cecil Mwambe ameshauri kanuni za Bunge zibadilishwa ili wabunge waweze kujadili Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kabla ya kupitisha bajeti nyingine.
Amesema hayo leo Aprili 12, 2023 wakati akichangia mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya waziri mkuu na ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.
Amesema ametoa pendekezo hilo kwa sababu bajeti inayolalamikiwa ni ile ambayo waliipitisha na kuna watu watapelekewa fedha za Serikali wakiwa bado wapo madarakani.
“Badala ya kusubiri hadi Novemba ambayo itakuwa ni miezi sita tangu fedha mpya zilizopopelekwa katika wizara tofauti ambazo nyingi zinalalamikiwa, watu wanalalamikiwa, tumemsikia mheshimiwa Rais naye akiwalalamikia watu,”amesema.
Ametaka watu hao wawajibike kabla ya kupelekewa fedha nyingine ambazo inawezekana wakaenda kuzitumia kwa mtindo ule ule kwasababu wanajua itakapofika Novemba tutawajadili na kuwaondoa.
“Tubadilishe mtindo wetu wa ufanyaji wa kazi hasa inapokuja ripoti nzito kwa sababu kuna haja ya kujadili ripoti ya CAG na kuona mapungufu kabla hatujapanga fedha katika maeneo yale yale ambayo kuna matobo makubwa ya matumizi ya fedha za wananchi,” amesema.