Connect with us

Kitaifa

Simanzi ajali yaua 13 siku ya Pasaka

Songea. Imekuwa Pasaka ya majonzi kwa familia za watu
13 baada ya ubovu wa barabara na utelezi uliosababishwa na mvua
zinazoendelea kunyesha mkoani Ruvuma, kutajwa kuwa chanzo cha ajali iliyoondoa uhai wao.

Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia jana katika Kijiji cha Namatui wilayani Songea.

Ajali hiyo ambayo pia imejeruhi watu wawili ilitokea baada ya gari
walilokuwa wakisafiria kutumbukia mtoni wakati wakitoka mnadani katika
Kijiji cha Ndongosi, barabara ya Ndongosi eneo la Songea Vijijini.

Hayo yalielezwa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco
Chilya alipokuwa akitoa taarifa ya ajali hiyo iliyotokea saa 3 usiku wa
kuamkia juzi katika daraja la Mto Njoka kwenye Kijiji cha Namatui.
Kamanda Chilya alisema ajali hiyo imehusisha gari aina ya Mitsubishi Fuso, iliyokuwa ikiendeshwa na Thobius Njovu.

Alisema watu hao ambao ni wafanyabiashara waliokuwa wanatoka mnadani katika Kijiji cha Ndogosi kwenda Namatui.

“Ajali hii imetokea saa 3 usiku na uchunguzi wa awali umebanini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni ubovu wa barabara na utelezi uliosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha, ndiyo umefanya gari hiyo kuteleza na
kutumbukia mtoni,” alisema Chilya.

Aliwataja baadhi ya waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni Happy Msemwa, Jafari Juma, Hidaya Salum, Jumasaid, Bihesha Yahaya, Mustafa Ally na Deograsia Mapunda.
Kamanda huyo aliwataja wengine waliotambulika kwa jina moja ni
Mwanaisha, Hamad, Simba na Mama Faraja huku akiwataja majeruhi Hamis Mbawala na Christopher Banda.
“Majeruhi wamelazwa katika Kituo cha Afya Mpitimbi na miili ya marehemu hao imehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Ruvuma,” alisema Kamanda Chilya.
Rais Samia, Mpango, Majaliwa watoa salamu za pole
Akizungumzia ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas alisema Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Philip Mpango na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wametuma salamu zao za pole kutokana na ajali hiyo.

“Viongozi hawa wametuma salamu zao za pole kwa wana Ruvuma wote, majeruhi na ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza maisha na wamewataka viongozi wa hospitali na polisi kutoa vibali kwa ndugu wanaohitaji kuwachukua wapendwa wao kwa ajili ya maziko,” alisema Thomas.

Alirudia rai iliyotolewa na kamanda wa polisi wa mkoa huo kuhusu ya tabia ya wananchi kupanda juu ya mizigo pindi wanapoisafirisha na magari ya mizigo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ruvuma, Dk Majura Magafu alipozungumza na gazeti hili kwa simu alisema amepokea miili ya watu 13, kati ya wanaume saba na wanawake sita.
Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi