Kitaifa
NHIF yavilipa vituo vya afya huduma hewa Sh14 bilioni
Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere imeonyesha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ilivilipa vituo vya afya madai yasiyo ya kweli kiasi cha Sh14.46 bilioni kwa kipindi cha mwaka 2019/20 hadi 2021/22.
Wakati fedha hizo zikipotea, CAG amebaini watumishi 146 wakiwemo 129 wa vituo vya afya na 17 wa mfuko huo walijihusisha na vitendo vya udanganyifu.
“Watumishi 146 wa NHIF na wa vituo vya afya walijihusisha na vitendo vya udanganyifu, lakini Kitengo cha Kupambana na Udanganyifu kiliripoti maofisa 17 tu wa Mfuko waliojihusisha na vitendo vya udanganyifu kwa kamati za nidhamu,” alisema CAG.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano NHIF, Angela Mziray alisema, “Hiyo ya 14.46bilioni ni madai yaliyowasilishwa na vituo vya huduma za matibabu yasiyo ya kweli ambayo yalilipwa na mfuko. Na hii kama ilivyoandikwa na ripoti ya CAG imepatikana kwenye ripoti za udanganyifu za baada ya mfuko kufanya uchunguzi. Na sababu za madai haya zimetajwa hapo kwenye ripoti.”
Kuhusu suala la udanganyifu uliofanywa na watumishi Angela alisema;
“Hapa 129 ni watumishi wa vituo na vya matibabu ambao ripoti inasema wameripotiwa kwenye mabaraza ya kitaaluma na watumishi wa NHIF 17 ambao wametipotiwa kwenye kamati za nidhamu za Mfuko. Jumla ni 146.
“Hapa 129 ni watumishi wa vituo vya matibabu hawa NHIF tuliwaripoti kwenye mabaraza ya kitaaluma na watumishi wa NHIF 17 ambao wameripotiwa kwenye kamati za nidhamu za Mfuko. Jumla ni 146,” amesema Angela.
CAG alisema katika ripoti za kupambana na udanganyifu kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2019/20 hadi 2021/22 zilibaini kuwepo na madai yasiyo ya kweli na yasiyo sahihi ambayo NHIF walivilipa vituo vya afya.
“Kati ya Sh1.71 trilioni ambazo zililipwa kwa vituo vya kutolea huduma za afya kwa kipindi cha miaka mitatu ya fedha kuanzia 2019/20 hadi 2021/22, Sh14.46 bilioni zililipwa kwa madai ya uongo na yasiyo sahihi.
“Uchambuzi zaidi ulifanyika ili kupata malipo ya madai yasiyo ya kweli, katika vituo vya afya vya binafsi, serikali na vile vya mashirika ya dini na ukaguzi ukabaini vituo binafsi vya huduma ya afya vilikuwa na kiasi kikubwa cha madai yaliyolipwa yasiyo ya kweli ikilinganishwa na vya Serikali.
“Zaidi ya Sh10.38 bilioni zililipwa kwa vituo binafsi na madai katika vituo vya mashirika ya dini ilikuwa ni Sh2.49 bilioni na vituo vya Serikali ilikuwa Sh1.57 bilioni,” alisema CAG.
CAG alisema kumekuwa na ongezeko la madai yasiyo ya kweli na yasiyo sahihi kutoka Sh4.32 bilioni mwaka wa fedha 2019/20 hadi Sh4.55 bilioni kwa mwaka wa fedha 2020/21 na Sh5.59 bilioni katika mwaka wa fedha 2021/22.
Mwenyekiti wa Chama cha watoa huduma za afya binafsi Tanzania (Aphta) Dk Egina Makwabe alisema vituo binafsi vinaonekana kutumia fedha nyigi katika udanganifu kwa kuwa hata malipo asilimia kubwa yanakwenda huko.
“Mfuko wa bima ya afya unalipa zaidi vituo binafsi siyo serikali kwa kuwa wagonjwa wenyewe wanapenda kutumia vituo binafsi kuliko vya Serikali, lakini changamoto kubwa NHIF ukikosea kidogo tu wanahesabu ni udanganyifu,” alisema.
Hata hivyo, Dk Makwabe alisema madai ya udanganyifu kwa mfuko yapo chini ya asilimia 2 ambayo ni ndogo, kwani kwa viwango vya dunia ni asilimia 5.
Kuwepo kwa malipo yasiyo ya kweli na yasiyo sahihi ya madai yalibainishwa kwenye viwango tofauti vya huduma za afya. Kwa mfano, mapitio ya kupambana na udanganyifu ripoti ilionyesha kuwa rufaa za kanda na mikoa, hospitali za wilaya na kliniki maalum zilikuwa na malipo yasiyo ya kweli na yasiyo sahihi ya zaidi ya Sh2 bilioni.
Ukaguzi ulibaini vituo vya afya vinavyomilikiwa na watu binafsi vilikuwa na kiasi kikubwa cha malipo yasiyo ya kweli ikilinganishwa na serikali na mashirika ya kiimani.
Hata hivyo, katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ripoti hiyo imebaini kuwepo kwa madai yasiyostahili na yasiyokuwa na dhamana yaliyofikia zaidi ya Sh501.3 milioni.
“Madai haya yalitambuliwa kupitia uhakiki uliofanyika kwenye vituo vya huduma za afya ndani ya kipindi kilichofanyiwa ukaguzi katika mikoa ya Mbeya, Mwanza na Dodoma,” imesema ripoti hiyo.
Pia, ripoti hiyo imebaini kuwepo kwa wanachama wasiostahili na wasiosajiliwa waliojipatia huduma za afya kuanzia mwaka wa fedha 2019/20 hadi 2021/2022 kwa gharama ya Sh3,539 milioni katika mikoa ya Ilala, Mwanza na Geita.
Pia, CAG kutofanyika ipasavyo kwa urejeshaji wa madai yasiyo halali, ambapo hadi kufikia Juni 2022, zaidi ya Sh12.1 bilioni zilizotokana na madai hayo zilikuwa hazijarejeshwa, huku pia kukiwa na madai yasiyo halali ya kiasi ya zaidi ya Sh804.02 milioni.
Zaidi ya hayo, mapitio ya Ripoti Kuu ya Mwaka ya CAG kwa Mashirika ya Umma ya Machi 2022 ilibaini katika mwaka wa fedha 2020/21 Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ziliwasilisha madai kwa NHIF kiasi cha Sh55.53 bilioni.
Kati ya hizo madai ya Sh3.87 bilioni (7%) yalikataliwa na NHIF huku mwaka 2019/20 kiasi kilikuwa Sh3.13 bilioni (4%).
Sababu za kukataliwa zilizotajwa ni pamoja na makosa ya hesabu, kukosa maelezo ya huduma zinazodaiwa kutolewa baada ya uthibitishaji wa madai, yasiyofaa kuweka alama za ugonjwa, kudai mara mbili, kesi zilizothibitishwa za ulaghai.
CAG alitaja vyanzo vingine kuwa kukosekana kwa barua ya idhini kutoka NHIF, nambari batili ya idhini, tabibu batili au saini ya mgonjwa, kutozingatia bei ya NHIF, kutozingatia mwongozo wa kawaida wa matibabu (STG).