Kitaifa

TBS yachunguza poda za watoto Johnson kusababisha kansa

Dar es Salaam. Wakati wazalishaji wa poda za watoto za Johnson&Johnson wakieleza dhamira yao ya kulipa fidia na kusitisha uzalishaji wa poda hizo kutokana na madai ya kusababisha saratani, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeanza kufanya uchunguzi huku bidhaa hizo zikionekana kutapakaa madukani.

Mwaka 2020, kampuni ya Johnson&Johnson ilitangaza kusitisha usambazaji wa poda hiyo nchini Marekani na Canada kutokana na kile ilichokiita “habari potofu” juu ya bidhaa hiyo, kabla haijatangaza rasmi juzi kuifuta ulimwenguni kote.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya kampuni hiyo Aprili 4 mwaka huu kushindwa kesi za muongo mmoja na nusu na kukubali kulipa fidia ya dola bilioni 8.9 (Sh20.8 trilioni) kutokana na kesi kuwa madini ya talcum yanayotumika katika poda hiyo na bidhaa nyingine yalisababisha saratani kwa watumiaji.

Poda ya Johnson&Johnson ni mojawapo ya chapa zinazotambulika zaidi za kampuni hiyo na wengi wa walalamikaji walidai kuwa talcum iliyotumiwa katika bidhaa hiyo ilikuwa na kemikali ya asbestosi, inayojulikana kusababisha saratani.

Kufuatia sakata hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Athuman Ngenya alisema baada ya kupokea taarifa hizo wameanza kufanya uchunguzi upya kwa sampuli za poda hizo zilizopo nchini.

“Tumeanza kufanya uchunguzi ili kubaini iwapo ni toleo lipi lenye kusababisha athari na iwapo tutajiridhisha na kubaini kwamba ni zote basi tutapiga marufuku kutokana na taratibu zilizopo,” alisema Dk Ngenya.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wamesisitiza kuwa haishauriwi watoto wadogo kupakwa poda, kwani kemikali ya ‘talc’ ambayo imekuwa ikitumika kutengeneza bidhaa za unga kama poda huleta madhara makubwa katika mapafu ya mtoto.

Daktari bingwa wa watoto kutoka Hospitali ya Aga Khan, Maria Bulimba alisema poda hizo zikiingia kwenye mapafu kuna chembechembe za kemikali ya talc ambazo ni hatari iwapo zitaingia katika mapafu ya mtoto.

“Poda, kitaalamu madaktari wa watoto tunazikataa, hata kwenye makubaliano ya mashirika ya watoto hatukubali kabisa kutumia poda aina yoyote kwa sababu kuna chembe chembe zinazoathiri njia zake za hewa,” alisisitiza Dk Bulimba.

Alisema wazazi wengi wamekuwa wakitumia poda ili maeneo ya mikunjo ya watoto yawe makavu na kuondoa majimaji lakini kitaalamu haikubaliki.

“Ijulikane kwamba bidhaa za poda zimetengenezwa kwa sababu hiyo, lakini kuna hizo chembe chembe zenye madhara ndizo zilizotufanya tuzizuie licha ya kwamba kwa sasa imebainika kusababisha saratani.

“Hizi chembechembe zinaweza kumletea shida mtumiaji kwenye mapafu na aleji za mara kwa mara, sababu ni unga na pia inaweza kuharibu ngozi kama ana kidonda, ngozi itazidi kuharibika,” alisisitiza.

Hata hivyo, Dk Bulimba alishauri kuwa badala ya mzazi kupendelea kumpaka poda mtoto watumie mafuta ya Vaseline au yoyote mazito kumpakaa na kumwogesha pindi anapohisi mtoto amepata jasho, bila kumpakaa poda.

Baadhi ya wazazi waliozungumza na gazeti hili kuhusu bidhaa hizo walionekana kutokuwa na uelewa kuhusu undani wa tatizo lenyewe.

“Watoto wote nimetumia hii poda, sasa nimepatwa na wasiwasi kwa sababu ya hiyo taarifa, bado ninapata ukakasi kama zina shida imekuwaje hao wenye viwanda wazisambaze?” alihoji Rebecca Mvangi, mkazi wa Iringa.

Zakutwa madukani

Hata hivyo, aina hiyo ya poda jana zimekutwa katika maduka kadhaa hapa nchini zikiendelea kuuzwa, huku wafanyabiashara wakiwa hawana taarifa na kuwa ni miongoni mwa poda zinazouzika zaidi ikilinganishwa na nyingine.

Hilo pia lilielezwa na mfanyabiashara wa duka moja la dawa jijini Dodoma, Fikiri Jumaa. “Bidhaa za Johnson&Johnson ndizo tunazouza zaidi, watu wanazipenda na ndizo ninazouza kwa sasa, sileti aina nyingine ya poda. Ingawaje wateja kwa sasa wanapungua lakini bado zina soko, ni bidhaa muhimu sana,” alisema Fikiri.

Sababu kufutwa sokoni

Kampuni ya Johnson & Johnson imefikia maamuzi hayo baada ya kukabiliwa na mafuriko ya kesi zinazodai bidhaa zake zilisababisha saratani hadi walalamikaji kufikia 70,000.

Poda hiyo iliyoanza kuuzwa miaka 129 iliyopita, ilitajwa kuhusu madhara hayo miongo kadhaa iliyopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi