Kitaifa

CAG abainisha madudu fedha za Uviko-19

Moshi. Ripoti ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika fedha za Uviko-19 imebainisha madudu kadhaa, ikiwemo kwamba bidhaa zenye thamani ya zaidi ya Sh50 bilioni zilizolipiwa fedha hazijapokewa.

Septemba 7, 2021 Tanzania ilipokea mkopo wenye masharti nafuu wa Dola 567.25 milioni (sawa na Sh 1.29 trilioni) kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambazo zilielekezwa sekta za afya, elimu, maji na utalii na mazingira.

Mbali na sekta hizo, sehemu ya fedha hizo ilipelekwa katika sekta za ulinzi wa jamii, nishati, uwezeshaji uchumi, uratibu na usimamizi ambapo Tanzania Bara ilitumia Sh1 trilioni na Zanzibar Sh230.1 bilioni.

Baada ya kupata fedha hizo, Oktoba 10, 2021 Rais Samia akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19 jijini Dodoma, aliwataka viongozi wa ngazi mbalimbali kuanzia mawaziri hadi wakurugenzi kutumia vizuri fedha hizo, akisisitiza kuwa hatakuwa na huruma na mtu katika fedha hizo.

“Kwa wale wanaotaka kuzijua rangi zangu halisi, wajaribu kudokaa fedha hizi au wabadilishe matumizi yake bila maelewano,” alionya Rais Samia

Hata hivyo, katika ripoti hiyo ya CAG iliyotolewa Januari 31, mwaka huu imebaini kuwepo bidhaa zenye thamani ya zaidi ya Sh50 bilioni, hasa vifaatiba ambazo hadi kufikia Novemba 2022 (zaidi ya mwaka mmoja) vilikuwa havijapokewa na taasisi husika au kupokewa ambavyo havikuagizwa.

Kulingana na ripoti hiyo iliyotiwa saini na CAG Charles Kichere, taasisi 21 zililipa Sh17.92 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba, lakini hazikuwa zimepokea vifaa hivyo hadi Novemba 2022.

Mbali na hilo, ripoti hiyo iliyochapishwa katika tovuti ya ofisi ya CAG, inaitaja Wizara ya Afya kuwa ililipa Sh18.85 bilioni kwa kampuni ya magari ya Toyota Tanzania na Unicef kwa ajili ya ununuzi wa magari, lakini hadi Novemba 2022 magari hayo yalikuwa hayajapokewa na wizara hiyo.

Halikadhalika, Bohari ya Dawa (MSD) iliagiza vitenganishi na dawa vyenye thamani ya Sh962.64 milioni kutoka kwa watoa huduma watatu bila mkataba na hakuna kilichopokewa hadi wakati wa ukaguzi huo Novemba mwaka jana.

Aprili 2022 kwa mujibu wa ripoti hiyo, Wizara ya Afya iliingia mkataba na kampuni ya Zenj Motors wa ununuzi wa magari 12 ya wagonjwa yenye thamani ya Sh1.97 bilioni kwa ajili ya hospitali za Zanzibar ambao haukutekelezwa ipasavyo.

Chini ya mkataba huo, magari hayo yalitakiwa yawe yamefikishwa wizarani ndani ya siku 90 lakini hadi Novemba 2022 (zaidi ya mwaka mmoja), magari hayo yalikuwa hayajapokewa na hakuna ushahidi wa kuongezewa muda.

Kwa upande wake Wizara ya Afya ya Zanzibar iliingia mikataba saba na wazabuni ya kuwasambazia vifaa kwa ajili ya hospitali nane, yenye thamani ya Sh10.41 bilioni, lakini hadi Novemba 22, 2022 hakuna kifaa hata kimoja kilichokuwa kimepokewa.

Pia, ripoti imebaini Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi iliipa Comfix Engineering zabuni ya vifaa vya uvuvi vyenye thamani ya Sh139.5 milioni na vilipaswa kukabidhiwa Julai 23, 2022 lakini hadi Novemba 23 mwaka jana havikuwa vimepokewa.

CAG anasema katika ripoti hiyo Shirika la Umeme Zanzibar (Zesco) liliingia mkataba na Vuka Timbers Februari 3, 2022 wa kulipatia nguzo 10,000, lakini hadi Novemba mwaka jana walikuwa wamekabidhi nguzo 1,089 huku zilizosalia (asilimia 89) hazikuwa zimepokewa.

Wizara ya Nishati na Shirika hilo la Umeme walilazimika kukubaliana kuongeza muda wa makabidhiano kwa miezi mitatu hadi Desemba 2022, lakini nguzo hizo bado hazikukabidhiwa hata baada ya muda wa nyongeza kuisha.

 

VAT kwa bidhaa zenye msamaha

Katika ripoti hiyo, CAG anaeleza kuwa Hospitali ya Ocean Road ya jijini Dar es Salaam iliipa kampuni ya Anudha Limited zabuni ya kusambaza na kufunga vifaatiba vya huduma ya dharura kwa hospitali mbalimbali.

Hata hivyo, ankara iliyowasilishwa haikuwa imeonyesha bei hiyo inajumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) lakini wakati taasisi ya Ocean Road inamlipa mzabuni, ilijumuisha na Sh333 milioni za VAT, licha ya kuwa na msamaha wa kodi.

Halikadhalika, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) ililipa VAT inayofikia Sh166.61 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali vya ujenzi wa miradi ya maji wakati mamlaka hiyo ilikuwa tayari na msamaha wa kodi.

Bidhaa kinyume cha mkataba

Katika ripoti hiyo, CAG amebaini Taasisi ya Ocean Road na Hospitali ya Rufaa ya Amana, waliingia mkataba na kampuni ya Anudha Limited wa kutoa huduma ya vifaatiba kwa ajili ya hospitali, lakini vifaa vilivyotolewa havikukidhi vigezo vilivyotakiwa.

Si hilo tu, Hospitali ya Lugalo, ilinunua vifaa tiba vyenye thamani ya Sh3.67 bilioni bila maelekezo mahususi ya mtumiaji, kwa kuwa Wizara ya Afya ilikuwa imeziagiza Ocean Road na MSD kununua vifaa hivyo.

Pia, ripoti hiyo ya kurasa 169 imesema tathmini iliyofanywa katika mabomba yaliyotumika katika mradi wa kusambaza maji wilayani Rombo wa Njoro II hayakuwa yanalingana na yale yaliyoonyeshwa katika michoro.

Halikadhalika Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iliingia mkataba wa kununua na kufunga vifaa vya kidijitali vyenye thamani ya Sh69.8 milioni, lakini vigezo vilivyokuwa zimewekwa havikutimizwa na mzabuni aliyepewa kazi hiyo.

Kuchelewa kwa miradi

Katika ripoti hiyo, CAG anasema Hospitali ya Ligula RRH mkoani Mtwara iliingia mkataba wa ukarabati wa majengo, yakiwemo uangalizi maalumu (ICU) na nyumba za wafanyakazi, lakini hadi ukaguzi unafanyika miradi hiyo ilikuwa haijakamilika.

CAG ameeleza pia licha ya kutengwa Sh5.72 bilioni kwa ajili ya kujenga vyuo 23 vya ualimu, vyuo 10 ujenzi wake ulikuwa haujakamilika kwa asilimia 100 kufikia Oktba 2022, mradi ukiwa umechelewa kwa siku 113.

Kazi zilizokuwa zimebaki ni pamoja na kupiga rangi, kufunga umeme na ununuzi wa samani, na pamoja na hayo kulikuwa hakuna fedha za kukamilisha kazi hizo katika vyuo vinane. Chuo cha Ngorongoro kilikuwa na Sh61.83 milioni.

Kupitia ripoti hiyo, CAG amebainisha kuwa Oktoba 2021 alitembelea miradi yenye thamani ya Sh471.23 milioni iliyotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) lakini alibaini kuwepo na nyufa kwenye majengo.

Madarasa bila matumizi

CAG ameeleza katika ripoti hiyo kuwa madarasa 138 yaliyokamilika katika mamlaka 10 za Serikali za Mitaa yenye thamani ya Sh2.78 bilioni yalikuwa hayatumiki kutokana na kukosekana kwa samani na vyoo.

Pia kulikuwa na ucheleweshaji katika kuchagua wanafunzi kwa ajili ya shule husika.

CAG alisema Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa) iliingia mkataba na kampuni za Osaju na Shamjo wa kujenga pampu 35 kuvuta maji Pemba na Unguja kwa thamani ya Sh2.68 bilioni, lakini hadi ukaguzi unafanyika, pampu 17 zilikuwa hazijatengenezwa.

Bugando yaguswa

Katika ripoti hiyo, CAG alisema Hospitali ya Bugando ya jijini Mwanza ilitoa zabuni saba za ununuzi wa vifaatiba vyenye thamani ya Sh3.95 bilioni kwa kampuni moja ya Computech ICS Ltd, licha ya kuwapo washindani wengine.

Hiyo ilikuwa ni kinyume cha maelekezo ya Wizara ya Afya kupitia barua ya Februari 2, 2022 iliyowashauri kuhakikisha mzabuni mmoja haleti ukiritimba kwa wengine ambao wana sifa zinazofanana na zake.

Ushauri na mapendekezo

CAG amependekeza taasisi ya Ocean Road ihakikishe Sh333 milioni zilizolipwa kimakosa kama VAT zinarejeshwa na pia Wizara ya Afya ihakikishe kodi ya zuio ya Sh33.7 milioni ambayo haikukatwa, inakatwa na kuwasilishwa TRA.

Kuhusu malipo ya Sh17.92 bilioni zilizolipwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya hospitali ambavyo vilikuwa havijapokewa wakati wa ukaguzi, wahusika wavifuatilie ili vipatikane.

Katika ripoti hiyo, CAG ametoa mapendekezo kuhusu Sh18.85 bilioni zilizolipwa kwa Toyota Tanzania na Unicef kwa ajili ya ununuzi wa magari, akiitaka Wizara ya Afya kufuatilia suala hilo ili magari hayo yakabidhiwe.

CAG ameushauri uongozi wa hospitali ya Bugando kwamba siku zijazo, ihakikishe inazingatia maelekezo ya Wizara ya Afya ili kuepuka ukiritimba unaojitokeza katika kutoa zabuni nyingi kwa mzabuni mmoja.

Katika majumuisho ya ripoti hiyo, CAG alisema maoni na mapendekezo yake yana lenga kuisaidia Serikali kuboresha jitihada zake katika kutoa fedha, usimamizi mzuri na ufanisi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwamo ya Uviko-19.

Pia ametaka taasisi zinazohusika na manunuzi, kuhakikisha zinazingatia miongozo iliyowekwa na sheria ya PPRA ya 2011 na kanuni zake na kuhakikisha zinatumika mbinu sahihi za manunuzi na kuhakikisha kunakuwa na ushindani wa haki.

Kuhusu usimamizi wa matumizi ya fedha, CAG alisema ili kuimarisha udhibiti wa ndani, taasisi za Serikali zinapaswa kuhakikisha zinapata idhini sahihi kabla ya matumizi, utunzaji wa vocha za malipo na nyaraka mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi