Kitaifa
Wabunge wawekwa ‘kitanzini’ bajeti ijayo
Dodoma. Wakati vikao vya Bunge la Bajeti ya 2023/2024 vikianza leo, baadhi ya wananchi wametaka wabunge kujielekeza katika kutatua changamoto ya ugumu wa maisha kutokana na bei za bidhaa kuwa juu.
Mengine wanayoyatarajia ni uimarishaji wa demokrasia kwa kupanga bajeti ya mchakato wa Katiba mpya, nyongeza ya mishahara na utatuzi wa changamoto ya ukosefu wa ajira, kuongeza mikopo na maeneo ya kufanyia biashara kwa machinga.
Wakati vikao vya bajeti vikianza, wananchi wamekuwa na kilio cha ugumu wa maisha kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa mbalimbali hasa vyakula nchini.
Taarifa ya mwenendo wa bei za bidhaa muhimu kwa Februari mwaka huu iliyotolewa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji inaonyesha bei ya unga wa mahindi ilikuwa kati ya Sh1,500 na Sh2,000 kwa kilo.
Bei ya mchele ilionyesha kwa kilo ilikuwa kati ya Sh2,500 hadi Sh3,500 wakati maharage yaliuzwa kati ya Sh2300 hadi Sh4,000 huku unga wa ngano ukiuzwa Sh2,000 hadi Sh2,500.
Sukari iliuzwa kwa kati ya Sh2,700 na Sh3,000, mafuta ya kupikia ya alizeti yakiuzwa kati ya Sh4,750 na Sh7,800 kwa lita moja, mafuta ya mawese (korie na safi), yakiuzwa kati ya Sh4,500 na Sh7,250.
Kilio cha ugumu wa maisha kilisikika pia kwenye mkutano wa Bajeti ya mwaka 2022/2023, ambapo wabunge walilalamikia upandaji wa bei za vyakula, vifaa vya ujenzi, mafuta ya petroli na dizeli na kutaka Serikali kuchukua hatua za kuwapunguzia makali ya maisha wananchi.
Waliitaka Serikali kuweka ruzuku katika mafuta ya petroli na dizeli na kuongeza jitihada za uwekezaji katika uzalishaji wa mazao yanayoagizwa kutoka nje ya nchi, ili kuwapunguzia wananchi mzigo.
Ili kukabiliana na ugumu huo, Serikali ilitangaza hatua ilizochukua kuwa ni kuweka ruzuku kwenye mafuta ya petroli na dizeli ya Sh100 bilioni kila mwezi.
Aidha, Serikali ilipunguza tozo za miamala ya simu, kuweka ruzuku katika mbolea na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za vyakula zinazoagizwa kwa wingi kutoka nje ya nchi ikiwemo mafuta na sukari.
Pia, katika kukabiliana na kupanda kwa bei ya vyakula Serikali ilitoa vibali vya kuingiza mchele kutoka nje ya nchi ambapo hadi kufikia Machi, 2023 tani 90,000 za mchele zilitarajiwa kuwasili nchini.
Walichokisema wasomi
Akizungumza na Mwananchi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alisema Watanzania wanataka kuona ni namna gani bajeti hiyo itakuja kupunguza gharama za maisha kwa sababu bei ya vitu imepanda kwa kiasi kikubwa kutokana na sababu mbalimbali.
Alizitaja sababu zilizofanya gharama za maisha kupanda ni ukame, kupanda kwa bei ya mafuta duniani na vita ya Ukraine na Urusi.
“Kwa vyovyote vile kwa bajeti inayokuja tunatarajia namna itakavyopangwa ili kuleta unafuu kwa maisha ya Mtanzania wa kawaida. Ndio maana kule Kenya watu wanaandamana Serikali ishushe bei ya unga. Kule kwao unga ni kiashiria gharama za kawaida ziko juu hasa kwa mwananchi wa kawaida,” alisema.
Anachokisema Loisulie kuhusu Kenya, kuna maandamano kila Jumatatu na Alhamisi yaliyoitishwa na Kiongozi wa Azimio Kwanza, Raila Odinga yanayolenga kuishinikiza Serikali ya Rais William Ruto pamoja na mambo mengine kushusha gharama za maisha.
Kuhusu kuimarisha demokrasia nchini, Dk Loisulie alisema Watanzania wanatarajia kuwa mkutano huu utajadili masuala ya demokrasia ikiwemo mchakato wa Katiba mpya, uchaguzi na masuala ya haki za kibinadamu.
“Watu wanatarajia kuona hii bajeti ina chochote ambacho kitakuja kutekeleza jambo linalohusiana na demokrasia. Kwa sababu bajeti ni kielelezo cha utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika mwaka husika,” alisema.
Katika mchakato wa Katiba, tayari Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro ameshaeleza bajeti yake itakuwa na nyongeza ya Sh9 bilioni, ili kwenda kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuukwamua mchakato wa Katiba mpya.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dk Nasibu Mramba aliungana na Dk Loisulie aliyesema wengi wanatarajia mkutano huu wa bajeti uwezeshe kupungua ama kusimama kupanda kwa bei za bidhaa.
“Vitu vimepanda sana nchini. Wanatarajia (Watanzania) kuona kuna hatua fulani za kupunguza huo mfumuko wa bei…Hayo ni matarajio, lakini uwezekano ukiangalia haupo kwa sababu visababishi havina suluhisho la muda mfupi lakini mwananchi anatarajia aone hivyo,” alisema.
Kuhusu upatikanaji wa ajira na nyongeza ya mishahara, Dk Mramba alisema watu wanatarajia kuona kwamba fursa ya ajira zinaongezeka kwa sababu wapo watu wengi mtaani hawana ajira na pia wafanyakazi wanataka kuona kunakuwepo na nyongeza ya mishahara.
Nini wabunge wafanye
Mwenyekiti wa machinga mkoani Dodoma, Bruno Mponzi aliwaomba wabunge kuishauri Serikali kuongeza mikopo yenye masharti nafuu kwa machinga, ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi kwa kukuza mitaji yao.
“Bajeti iongezwe kwa ajili ya kujenga maeneo ya wajasiriamali, najua kuna baadhi wameanza lakini waendelee kujenga ili vijana wengine wanaokosa ajira wapate fursa za kujiariji kwenye ujasiriamali,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Kukuza Utawala Bora na Uwazi Tanzania, Edwin Soko aliwataka wabunge kutazama maeneo yanayogusa vitu vingi kama mafuta ya petroli na dizeli kwa kupunguza tozo na ushuru, ili kupunguza bei ya bidhaa nyingine.
Alisema ili kupunguza bei ya vyakula, wabunge waishauri Serikali kuweka vivutio mbalimbali katika sekta ya kilimo nchini, hatua itakayowezesha wakulima kulima kwa wingi.
“Serikali ipunguze tozo katika miamala ya kieletroniki na riba benki kwa sababu kwa takwimu za sasa watu wengi wanatumia mifumo midogo ya pesa, wanahamisha fedha kutoka kampuni moja hadi nyingine na benki. Kwa hiyo ukipunguza tozo utawafanya hawa kutuma fedha kwa gharama rahisi. Waangalie pia suala la ujenzi wa miundombinu,” alisema.
Alitaka Serikali kufikiria kuongeza kodi katika pombe na sigara ili ongezeko hilo lisaidie kuziba mapengo kwenye maeneo mengine ambayo yanaonekana hivi sasa.
Alisema katika bajeti hili Bunge linapaswa kujielekeza katika vitu vinaathari kwa vitu vingine kwa kupunguza kodi na ushuri ili viweze kuleta mabadiliko kwa Watanzania.
Mkazi wa Buguruni jijini Dar es Salaam, Mariam Juma alisema wabunge ni wawakilishi wa wananchi, “wanajua uhalisia huku mtaani, kwa hiyo bajeti wanazokwenda kuzipitisha wakaangalie uhalisia wa huku. Suala la ajira, vyakula ni kilio.”