Kitaifa
Rais Samia, CCM wawaweka vigogo serikalini matumbo joto
Dar es Salaam. Ni matumbo joto. Ndivyo unavyoweza kusema kwa baadhi ya watendaji serikalini , wakuu na wenyeviti wa bodi za mashirika ya umma yaliyotajwa kuiingizia Serikali hasara.
Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wameitaka Serikali kufanya marekebisho ya muundo wa taasisi hizo kwa kuwa baadhi yake zililenga kutoa biashara lakini hivi sasa zinawekwa katika kundi la kufanya biashara.
Walisema bila ya kufanya tathimini ya kina ya kujua tatizo na njia za kulitatua hasara zitaendelea kuripotiwa kila kukicha.
Kwa mujibu wa ripoti Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2023/24 na ile ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zilizowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan siku chache zilizopita zilionyesha uwepo wa ubadhirifu na uzembe.
Katika ripoti hizo, taasisi 14 za umma zimetajwa kuiingizia Serikali hasara, jambo lililomfanya Rais Samia kutaka tathmini ifanyike iwapo kuna haja ya mashirika hayo kuendelea kuwepo .
“Yale mashirika yanayofaa yaendelee na yasiyo na tija yafutwe. Mashirika mengi yanachuma fedha kutoka serikalini lakini yenyewe hayaleti fedha,” alisema.
Kauli hiyo ya Rais Samia aliitoka Machi 29 mwaka huu, Ikulu jijini Dar es Salaam alipokuwa akipokea ripoti hizo, imepigiwa msumari na Kamati Kuu ya CCM iliyoketi juzi chini ya uenyekiti wa Samia, ikitaka hatua zichukuliwe kwa waliohusika kwenye ubadhirifu huo.
“Kamati Kuu imeelekeza Serikali kuchukua hatua thabiti kwa waliohusika na ukiukwaji wa sheria na kusababisha ubadhilifu wa mali na rasilimali za nchi.
“…imetoa maelekezo kwa Serikali kuwafuatilia watu wote wanaotumia dhamana zao za uongozi vibaya na kushindwa kuweka maslahi ya nchi na uzalendo mbele katika nafasi zao wanazozitumikia kuongoza wananchi, badala yake wanaweka maslahi yao mbele,” alisema Katibu wa Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema.
Maagizo hayo ya CCM inayounda Serikali, yanampa nguvu Rais Samia ambaye wakati akipokea ripoti hizo alionyesha kukerwa na viongozi wanaofanya ‘madudu’ hayo na alisema kumekuwa na upitishwaji mikataba mibovu inayoigharimu nchi, sambamba na kucheleweshwa kwa malipo kunakozalisha riba kubwa kwa Serikali.
Alisema licha ya kufahamika kila mkataba unavyopaswa kuwa, baadhi ya watendaji wanapitisha ambayo ina vifungu visivyostahili.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa waliozungumza na gazeti hili, wanaona kama maagizo hayo ya CCM kwa Serikali juu ya ripoti hizo za CAG ambazo zitawasilishwa bungeni katika vikao vinavyoanza kesho, zinawaweka katika mazingira tata ikiwemo kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Rais Samia wakati akipokea ripoti hizo alisema, ikiwa hatua za kisheria zitachukuliwa, zitawaogopesha wengine kucheza na nafasi wanazozihudumu.
Mashirika ambayo viongozi wake wako matumbo joto kulingana na ripoti hizo ni Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Shirika la Reli Tanzania (TRC), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Wakala wa Huduma za Manunuzi Serikalini (GPSA) na Mkulazi Holdings.
Greyson Mgonja ambaye ni wakili na mchambuzi wa masuala ya siasa, alisema uwajibikaji wa waliohusika katika ubadhirifu na uzembe ndicho kinachopaswa kufanywa ili kukomesha vitendo hivyo.
“Kama hatua hazitachukuliwa bado ubadhirifu utaendelea kujirudia ni vema waliotajwa katika ripoti hizo wakawajibishwa kwa kushitakiwa kwa uhujumu uchumi, mambo haya ya ovyo hayatajirudia,” alisema.
Akizungumzia hilo, Mchambuzi wa masuala ya siasa, Magabilo Masambu alishuku kuwepo kwa hujuma miongoni mwa wakuu wa mashirika hayo, akisema inawezekanaje wakiongoza ya umma yajiendeshe kwa hasara, lakini ya kwao binafsi yanajiendesha kwa faida.
Kwa mujibu wa Masambu, hakuna haja ya kuyafuta bali wajibu ni kuchunguza kwa kina kujua mzizi wa tatizo na hatua stahiki zichukuliwe.
“Wachunguzwe hao wanaoongoza kama hawana mashirika yao binafsi, maana ukiangalia utakuta ya kwao binafsi inawezekana kupata faida lakini hao hao kwenye mashirika ya umma yanajiendesha kwa hasara,” alisema.
Alisema kuna uwezekano wa mali za umma kutumika katika maslahi binafsi, akifananisha na kile kilichotokea mwaka 1995 wakati wa ubinafsishaji.
Alieleza wakati huo hakukuwa na kiongozi yeyote wa umma anayeruhusiwa kuwa na biashara binafsi.
Mdau wa maendeleo, Heri Mkunda alisema muhimu si kuchukua hatua kwa watendaji au shirika, kinachopaswa kufanywa ni uchunguzi wa kubaini mzizi wa tatizo.
Alisema mashirika hayo yalianzishwa kwa ajili ya kutoa huduma na baadaye yalibadilishwa na kutakiwa kufanya biashara, pengine shida inaanzia hapo.
“Mabadiliko hayo yanapaswa yaangalie upya muundo wa mashirika ili yajiendeshe kibiashara,” alisema.
Alisema ni muhimu kuyachunguza mashirika hayo kujua mzizi wa tatizo kuliko kuchukua maamuzi ya kuuondoa menejimenti au kufuta.
Kutokana na ubadhilifu huo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga, alitaka hatua za kinidhamu na kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika wote.
“Rais Samia asilalamike tena bali achukue hatua ili kuleta uwajibikaji katika taifa,” alisema.
Mchambuzi mwingine wa siasa, Mwalimu Samson Sombi alisema kufuta mashirika si muarobaini, bali ufanyike uchunguzi kubaini lilipo tatizo.
Hata wakati wa Mwalimu Julius Nyerere, alisema viwanda vingi vilianzishwa lakini vilikufa sio kwa sababu ya viwanda vyenyewe bali kukosekana uzalendo wa waliokuwa wanaviongoza.
“Pamoja na wazo zuri la Rais Samia la kutaka kufuta mashirika hayo, kufanyike uchunguzi kujua tatizo ni mashirika au watu wanaoyaongoza mashirika hayo, kwa kufuta si muarobaini wa kutatua tatizo,” alisema.
Ripoti ya CAG
Akisoma ripoti hiyo, CAG Charles Kichere alisema tathmini ya mwaka 2020/2021 na 2021/2022 inaonyesha mashirika 14 ya kibiashara yanayomilikiwa na Serikali yamepata hasara yakiwemo ATCL na TRC.
Uongozi wa ATCL upo tumbo joto baada ya hasara ya Sh36.1 bilioni iliyoipata katika mwaka wa fedha 2020/2021, hali hiyo ikajirudia mwaka ulioishia Juni 2022 likipata hasara ya Sh35 bilioni.
“Hatuwezi kwenda hivyo na nadhani hao wanaopokea hizo invoice wakazileta serikalini kwa raha zao kabisa, watupishe, hawafai kuwa kwenye hizo nafasi, kama wanafaa wangelifanyia kazi huko huko,” alisema.
Pia, viongozi wa TRC wapo tumbo joto baada ya shirika hilo katika mwaka wa fedha 2020/2021, kupata hasara ya Sh22.8 bilioni huku mwaka 2021/2022 ikipata hasara ya Sh31.29 bilioni kwa mujibu wa CAG Kichere.
Vigogo wa Mkulazi Holding, hawako salama kutokana na hasara ya Sh5.8 bilioni kwa mwaka 2020/2021 na mwaka 20221/22 ikirekodi hasara ya Sh14.3 bilioni.
Kulingana na ripoti ya CAG, mabosi ndani ya NDC hawako salama kwa kile kilichoshuhudiwa mwaka 2020/21 shirika hilo likipata hasara ya Sh26.3 bilioni na 2021/2022 likijikongoja kupunguza hasara hadi kufikia Sh11.9 bilioni.
Hatima ya vibarua vya mabosi wa TTCL nayo iko shakani baada ya kujiwekea malengo la kupata wateja 152,950 kwa kanda ya Dar es Salaam lakini wakashindwa kuyafikia na kuambulia wateja 40,626 sawa na asilimia 27.