Kitaifa
Siri ya wazazi kulala chumbani na watoto
Dodoma. Suala la watoto kulala na wazazi chumba kimoja linaelezwa kuwa ni chanzo cha kushuka kwa maadili ya Kitanzania, huku umaskini ukitajwa kuwa sehemu mojawapo.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa mambo, baadhi ya watoto hukaa macho usiku kuangalia nini kinachotokea kwa wazazi wao au kusikiliza wanachozungumza.
Viongozi wa dini, mila na wazazi waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wanakubali kuwa kulala na watoto ni kosa linalosababisha kuporomoka kwa maadili na utamaduni wa Mtanzania.
Changamoto hiyo imeibuliwa hivi karibuni baada ya Kamisaa wa Sensa ya watu na makazi, Anna Makinda kusema maadili ya Kitanzania yanazidi kushuka kila kukicha kutokana na mpangilio wa nyumba za watu kulala chumba kimoja na watoto wao.
Makinda alitoa kauli hiyo mwanzoni mwa Machi, mwaka huu mjini Babati mkoani Manyara, alipokuwa akifanya ukaguzi kwa wataalamu wanaofanya uchambuzi wa takwimu za makazi.
Alisema kumekuwa na ongezeko la watu kuzaliana, lakini wengi hawajui ni wapi watakwenda kuishi, jambo linalochangia kushuka kwa maadili kutokana na ujenzi wa nyumba duni ambazo huchangia mafuriko ya maji kutokana na msongamano wa makazi ya watu.
Kauli hiyo aliitoa ikiwa zimepita siku chache tangu spika huyo mstaafu alipoeleza kuwa kiini cha vijana wanaoitwa panya rodi kinatokana na vijana kukosa ajira na ni zao la ongezeko la watu nchini hivyo akataka liwe fursa.
“Watu wanazaliana sana bila hata kujua wanaweza kuishi wapi, hili nalo ni tatizo la nchi na linachangia maadili kushuka kila kukicha na kusababisha ongezeko la watu wasio na makazi, ni muhimu tukaliona hili,” alisema Makinda.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi ya watu nchini imeongezeka kutoka 44,928,923 waliohesabiwa mwaka 2012 hadi kufikia watu 61,741,120 kwa mwaka 2022, sawa na wastani wa ongezeko la asilimia 3.2 la idadi ya watu kwa mwaka.
Wakati idadi ya Watanzania ikiwa milioni 61.74, kuna jumla ya majengo milioni 14.3
Hata hivyo, wanaharakati na wanasaiokolojia wanasema umasikini ni chanzo kikubwa cha watoto kulala chumba kimoja na wazazi wao, hali inayosababisha mmomonyoko wa maadili.
Mila haziruhusu
Chifu Lazaro Chihoma wa kabila la Wagogo Wanyanzaga alisema katika tamaduni za Kiafrika mtoto kulala na mzazi wake mwisho ni miaka mitatu na akizidi isiwe juu ya miaka minne.
Chifu Lazaro alisema kauli ya Makinda iko sahihi na inapaswa kuungwa mkono na makundi mengine kwa sababu jambo alilozungumza lina ukweli kwa asilimia zote.
Alisema mtoto akifika miaka minne anatakiwa kuanza masomo kwa kuwa umri huo unamtosha kujifunza baadhi ya vitu na kuvitambua na ndiyo umri wa kuweza kukumbuka jambo lililofanyika jana au juzi akataka kuliiga.
Hata hivyo, alisema utamaduni wa zamani umeachwa na watu wengi wamekuwa wakiiga utamaduni wa kimagharibi wa kulala chumba kimoja na mtoto hata akifika miaka 10.
“Siyo kulala chumba kimoja tu, hata mkiwa vitanda tofauti bado ni kosa, hata zamani hatukufanya namna hii, licha ya kuwa tulikuwa na umasikini kuliko sasa, nashauri ikibidi kuwepo sheria ya kuzua jambo hili kabisa,” alisema Chihoma.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu suala hilo, Mwanasaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Erasto Kano alisema katika mazingira ya kawaida mzazi hawezi kulala chumba kimoja na watoto iwapo ana uwezo wa kupangisha vyumba zaidi ya kimoja.
“Sisi tunachokisema ni aina ya malezi wanayopewa watoto wetu, kwa tamaduni zetu haziruhusu mtoto na mzazi kulala pamoja kama si watoto wanaonyonyeshwa. Lakini kutokana na hali ya kiuchumi inalazimu hivyo lakini ukweli ni kosa,” alisema Dk Kano.
Alisema wakati mwingine anaweza akaliongea jambo kama vile watu wote wana maisha na mazingira sawa, lakini jambo hilo sio la kimaadili bali anachokiona ni suala hilo limekaa zaidi kwenye msukumo wa kiuchumi kwa wahusika wenyewe.
Dk Kano alisema mwalimu wa kwanza wa watoto ni wazazi na kitu cha kwanza wanaiga kutoka kwa wazazi wao na hivyo wawili hao wakipigana au kufanya mambo mengine, inakuwa rahisi kwa watoto hao kuiga kinachotokea.
“Endapo wazazi watakuwa katika maadili yasiyotakiwa, watoto wanayachukua moja kwa moja kwa sababu wazazi ni kama kioo chao na hujifunza kwa kuwatazama na kuiga matendo yao,” alisema msomi huyo.
“Ndiyo maana mkikaa kwa muda mrefu pamoja, tabia za asili huibuka bila kujali iwapo kuna watoto ama la, unaweza kuvua nguo ukabaki kifua wazi, jambo unaloweza kuliona ni la kawaida lakini linaleta mmomonyoko wa maadili.”
Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Jitihada za Maendeleo, (Wajiki) Janeth Mawinza aliunga mkono hoja ya Dk Kano akisema watoto wamekuwa wakishuhudia yanayofanywa na wazazi wao ndani ya vyumba hivyo bila kujali, ndiyo maana wakitoka wanakwenda kujaribu kwa wenzao.
Janeth alisema watoto wanaona na kushuhudia yanayoendelea na baadaye wakitoka ndani kwao wanahadithia na kuyatenda na kila mmoja anataka kusikia hadithi hizo ili akafanye kwa vitendo.
Kwa mujibu wa Janeth, ukatili unazidi kuwa mkubwa kwa sababu wengi wanajifunza hayo tangu utotoni na kunakosekana mbadala wa jinsi gani wanaweza kuwa sehemu ya suluhisho.
“Lakini tukilitazama kwa upande wake wa pili nako ni shida, hivi mtu hana uwezo na analala chumba kimoja na watoto wake, sisi tunataka awatoe watoto wakalale kwingine, hicho ni chanzo cha kusababisha wafanyiwe vitendo vya ukatili mahali waliko nje ya vyumba hivyo, kwa hiyo unakuta hakuna usalama kwa watoto pande zote,” alisema Janeth.
Athari zilizowahi kutokea
Mwanaharakari huyo alisema waliwahi kuwaibua watoto waliomshtaki mzazi wao kwa kulala nao chumba kimoja na usiku baba yao na mkewe (mama wa kambo) wakawa wanaendelea na mambo yao wakati watoto hao walikuwa kidato cha kwanza na pili.
Janeth alisema watoto hao walikwenda kushtaki katika baraza la kata kuwa hawawezi kuendelea kuvumilia vitendo vilivyokuwa vikifanyika usiku na hivyo iliamuliwa baba akawapangishie chumba chao ama warudishwe kwa mama yao mzazi.
Jesca Kaombwe alisema umri wa mtoto kulala na mzazi wake ungepaswa kuwa mwisho miaka mitatu, vinginevyo kuwepo na sababu za msingi.
Jesca alitolea mfano wa tukio la mwaka 2014 Wilaya ya Bahi ambako baba mzazi alikuwa akilala na mtoto wake hadi mwisho wa siku alikutwa na ujauzito na alipoulizwa alimtaja kuwa baba yake ndiyo mhusika.
Jesca, ambaye amekuwa mshauri wa wasichana wanaoacha masomo kwa sababu mbalimbali, alikumbushia habari hiyo iliyowahi kuandikwa na gazeti hili Septemba 28,2016.
Habari hiyo ilimtaja Omari Mjanja wa Kitongoji cha Chiwela, Kijiji cha Ilindi wilayani Bahi ambaye alimpa ujauzito binti yake wa pili kumzaa lakini alipoulizwa alisema kuwa alikuwa na utaratibu wa kulala na binti yake chumba kimoja, lakini siku ya tukio alirudi akiwa amelewa ndipo akajikuta kitandani kwa mwanawe na kufanya mapenzi.
Tulipoanza kupotea
Mwanasaikolojia mwingine kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya Tiba, Teddy Jany alisema kipindi cha nyuma, mfumo mzima wa tafsiri ya maisha ni nini na namna gani unatakiwa kuishi na vitu gani ambavyo mtoto unatakiwa kuvifanya vilikuwa vinafundishwa kuanzia utotoni hadi mtu anapokuwa mtu mzima.
Teddy alisema mfano wa malezi ya zamani, mtu aliyekuwa anasimamia malezi alikuwa ni mama aliyekuwa akibaki nyumbani kulea watoto na alibeba jukumu la tabia zinazotakiwa kufuatwa kwa watoto.
“Kipindi cha nyuma watoto wengi walikuwa wanawakimbia baba zao kwa kuwaogopa. Ilikuwa nadra kusikia mtoto wa darasa la kwanza analala na wazazi wake. Lakini kwa sasa imekuwa ni tofauti kwa sababu ya uzungu tumeanza kuwa na mapokeo ya tamaduni mbalimbali, ikiwemo zile za magharibi,” alisema.
Kingine alitaja utandawazi, kwamba watu wamekuwa wakishuhudia kupitia tamthilia mbalimbali mtoto wa mataifa ya kizungu akifungua milango ya wazazi wake na kwenda kulala, katika kitanda cha wazazi, jambo linalokwenda kinyume na maadili ya Kitanzania.
Alisema wazazi kulala chumba kimoja na watoto kunaweza kuwa ni sehemu ndogo ya kufanya maadili kushuka, lakini kunaweza kusababishwa na sababu mbalimbali.
Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu alisema tamaduni za zamani zimeachwa na sasa watu wanafuata mila na utamaduni wa nje, jambo alilosema linaweza kuwa na athari kubwa kwa siku za usoni.
Msambatavangu alisema kuna kila namna jamii kujirudi katika malezi ya watoto na kupunguza kinachoitwa ni ubize ili wasiathiri mambo mengine na kwamba bila kufanya hivyo, siku za usoni kunaweza kuwa na tatizo kubwa.
“Ukatili unaanzia hata kwa watoto wa kiume, kweli nilishasema kama hatutakuwa makini na mambo haya, tutegemee kuona vitu vya ajabu kwa siku za usoni na ikibidi hata kukosa mbegu za vijana wa kiume, mwisho wake utakuwa mbaya,” alisema Msambatavangu.
Aina ya malezi, mabadiliko ya teknolojia
Tedy Jany alisema maadili ni mchanganyiko wa tabia ambazo mtu anakuwa nazo na yametofautiana kutoka kwa mtoto mmoja kwenda kwa mwingine kulingana na aina ya malezi yanayopatikana kwenye familia.
“Ni aghalabu kupata mtoto anayesikia sauti moja kutoka kwa mzazi na akaendana nayo. Unakuta nyumbani anafundishwa kitu tofauti, kanisani au msikitini tofauti na shuleni tofauti, kwenye televisheni nako anasikia tofauti,” alisema.
Alisema mabadiliko ya kimaisha yanayoendana na sayansi na teknolojia yamechangia maadili yasibaki kama ilivyokuwa zamani kwa kuwa maisha pia yamebadilika kulingana na nyakati tulizo nazo.
Mtaalamu huyo alisema ni kazi ya mzazi sasa kuhakikisha kuwa mtoto anasimama katika mfumo wa maisha anaoutaka na kwamba kazi yake ni kuwa msimamizi na karibu na mtoto ili kufanya mtoto aishi kulingana na maadili anayoyataka.
Mtazamo watoto wa bweni
Teddy alisema mzazi anapokuwa karibu na mwanaye anaweza kufahamu tabia za mtoto na kama kuna mabadiliko ni rahisi kuyafanyia marekebisho mapema kuliko anapokuwa mbali naye.
“Ukiwa karibu naye utamuuliza sijakuona ukisali, sijakuona ukisalimia, hii itakusaidia kujua mtoto wako anaenda katika mazingira gani. Na kukiwa na msingi mzuri nyumbani kunamsaidia huyu mtoto anaposikia sauti nyingine kufikiria kuwa nyumbani alishaonywa kuhusiana na mambo hayo,” alisema.
Alisema kuwa mtoto kukaa bweni kunamnyima fursa mzazi kufanya mawasiliano na usimamizi sahihi kwa sababu wanakutana pengine baada ya miezi sita, ambayo kwa mtoto anayeishi na wazazi wake inatosha katika kushape tabia ya mtoto.
“Unapompeleka mtoto shule za bweni, tayari unaruhusu mtoto kupokea tabia anazokutana nazo katika shule na kusahau kwa sehemu kubwa mambo ya nyumbani, lakini anaporudi likizo muda atakaokaa, hautamtosha mzazi kumwezesha kuwa na maadili anayoyapenda yeye (mzazi),” alisema Teddy.
Anataja kuwa malezi ya mtoto kuna vitu viwili ambavyo ni adhabu na kumpongeza, lakini mwenendo wake hata muda wa kulala huwa anapangiwa tofauti na akiwa bweni, ambako wazazi huwa hawatambui hayo.
Jinsi ya kutatua
Mkazi wa Uhindini, George Faki aliwashauri wazazi kutengeneza familia watakayokuwa na uwezo wa kuihudumia kwenye mahitaji muhimu, ikiwamo malazi na hata chakula ili kuepuka kurundikana na watoto wao chumba kimoja.
George alisema jamii inapaswa kuweka utaratibu wa kuangalia kipato chao, muda sahihi wa kupata watoto, mazingira na idadi ya watoto watakaoweza kuwalea kulingana na uwezo walionao.
Naye John Gasper alisema Serikali itoe vipaumbele vya ajira kwa vijana wanaoanza maisha ambao wana familia ili wajitegemee kulipa kodi ya vyumba watakavyopangisha ikiwa wamedhamiria kunusuru mmomonyoko wa maadili unaotokana na kulala na watoto wao.
Hata hivyo, alitaja kukua kwa teknolojia na kuachwa watoto kuangalia maudhui yasiyofaa kunavyochangia kuongeza ufahamu wa watoto kujua nini kinaendelea wakati wa usiku.
“Zamani tulikuwa tunalala na wazazi wetu, lakini hujui chochote kinachoendelea, lakini sasa hivi watoto wanajua nini kitafanyika na wanakaa macho kuangalia au kusikiliza.
Kwa hiyo tuangalie maudhui ya kuwaacha watoto wetu waangalie na nini watajifunza kwenye maudhui hayo,” alisema.